Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.
BAADA ya kikosi cha Azam FC kuzidi kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL), Nahodha wa timu hiyo, Agrey Moris, ameweka wazi kuwa kwa sasa wanachoangalia ni kushinda mechi zote zilizo mbele yao.



Azam FC imekaa vema kwenye msimamo baada ya kuichapa African Lyon mabao 2-1 na kufikisha jumla ya pointi 21 kwa mabao yaliyofungwa na Yahya Zayd, Abdallah Kheri huku lile la Lyon likitupiwa na Hood Mayanja.

“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kupata ushindi katika mchezo huu (African Lyon) kiukweli mechi ilikuwa ngumu, African Lyon nawapongeza wamecheza vizuri ila naipongeza pia timu yangu tumeweza kujitolea kupata pointi tatu kuhakikisha tunapata matokeo katika mchezo wa leo (jana),” alisema.


Alisema timu hiyo kuendelea kupata ushindi kunazidi kuongeza morali kikosini. “Kila unaposhinda mchezo inaongeza morali katika timu, sisi tunachokiangalia ni kushinda kila mchezo uliokuwepo mbele ili tutajua mwisho katika ligi tupo katika nafasi gani,” alisema.


Nyota huyo aliyedumu kwa takribani miaka tisa ndani ya kikosi hicho, alizungumzia mechi tatu zijazo wanazoenda kucheza ugenini na kudai kuwa zitakuwa ngumu lakini watahakikisha wanajipanga na kupata matokeo.

“Kusema kweli mechi za ugenini ni ngumu ukiangalia pia kwa sababu ni viwanja vibovu ninavyosema hivyo nadhani watu wengi watakuja kusema ooh mmeanza kucheza mpira viwanja gani lakini ukiangalia hali ya viwanja vyetu haiku vizuri na ukingalia timu kama ilivyo Azam mechi zote watu wanavyokuja wanakamia kwa kutaka matokeo.

“Ila huu ni mpira ndivyo ulivyo tunatakiwa na sisi tujipange kuhakikisha tunashinda kila mchezo uliokuwa mbele yetu,” alisema.

Mechi hizo tatu za ugenini, Azam FC itacheza dhidi ya JKT Tanzania (Oktoba 24), Singida United (Oktoba 28), Kagera Sugar (Novemba 4) kabla ya kurejea nyumbani kukipiga na Mbao Novemba 08 mwaka huu.

Aidha Moris alizidi kuwavuta mashabiki wa Azam FC kujitokeza kwa wingi kuwasapoti kwenye mechi wanazocheza kwani timu sio wachezaji tu na benchi la ufundi bali mashabiki nao wana nafasi yao.

“Mashabiki waendelee kuisapoti timu kwa sababu tunawategemea sana, mpira sio wachezaji wa ndani tu na benchi la ufundi, mashabiki wana nafasi yao kubwa katika mpira waendelee kuisapoti timu na sisi tutawapa wanachokihitaji,” alisema.

Azam kwa sasa wanaongoza ligi kwa alama 21 wakifuatiwa na Yanga wenye alama 19 ma katika nafasi ya tatu mabingwa watetezi Simba wakiwa nafasi ya tatu kwa alama 17 sambamba na Singida United.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...