Na Greyson Mwase, Songwe
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amewataka wachimbaji wa madini  wanaoendesha shughuli zao za uchimbaji wa madini ya chokaa na ujenzi katika  kijiji cha Nanyala kilichopo katika Wilaya ya Mbozi iliyopo mkoani Songwe kuendelea na shughuli zao wakati wakisubiri  suluhu ya  mgogoro baina yao na kiwanda cha saruji cha Mbeya.
Naibu Waziri Nyongo aliyasema hayo tarehe 17 Oktoba, 2018 alipokuwa akizungumza katika mkutano na wachimbaji wadogo  uliofanyika katika kata ya Nanyala wilayani Mbozi mkoani Songwe ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika  mkoa huo  yenye lengo la  kukagua shughuli za uchimbaji wa madini,  kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.
Katika ziara yake Nyongo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Songwe, John Palingo, Afisa Madini Mkazi katika Mkoa wa Mbeya, Sabai Nyansiri, Afisa Madini anayesimamia wilaya za Songwe na Chunya, Athuman Kwariko, Afisa Madini kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mbeya, Ndege Bilagi, vyombo vya ulinzi na usalama vya wilaya pamoja na waandishi wa habari.
Nyongo alifafanua kuwa, awali maelekezo yalitolewa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ya kutaka viongozi kutoka katika mikoa ya Mbeya na Songwe kukaa pamoja na kuhakikisha wanamaliza mgogoro wa ardhi kati ya  wakazi wa Songwe na Mbeya na kiwanda cha kuzalisha saruji nje ya mahakama jambo ambalo linafanyiwa kazi kwa sasa.
Alielekeza viongozi kutoka katika mikoa husika kuhakikisha wanashughulikia mgogoro wa ardhi kati ya mikoa miwili na kiwanda cha saruji cha Mbeya kwa wakati huku wananchi wanaojishughulisha na shughuli za uchimbaji madini wakiendelea na shughuli zao kama kawaida katika maeneo husika.
Aliendelea kusema kuwa, jukumu kuu la Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini ni kuhakikisha wanatoa leseni za uchimbaji wa madini kwa kuzingatia sheria na kanuni za madini na kusisitiza kuwa leseni ya uchimbaji wa madini ni tofauti na  hati ya ardhi kwa kuwa inahusisha madini yaliyopo chini ya ardhi.
 Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia mbele) na Meneja wa Kiwanda cha chokaa cha Lime Africa kilichopo katika Kata ya Nanyala Wilayani Mbozi Mkoani Songwe, Fredy Msindo (kushoto mbele) pamoja na msafara  wakiendelea na ziara katika eneo la kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika mkoa wa Songwe yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini tarehe 17 Oktoba, 2018.
 Meneja wa Kiwanda cha chokaa cha Lime Africa kilichopo katika Kata ya Nanyala Wilayani Mbozi Mkoani Songwe, Fredy Msindo (katikati) akielezea shughuli zinazofanywa na kiwanda hicho kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo pamoja na msafara wake.
 Kutoka kushoto Afisa Madini Mkazi katika Mkoa wa Mbeya, Sabai Nyansiri, Afisa Madini kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mbeya, Ndege Bilagi na Afisa Madini anayesimamia wilaya za Songwe na Chunya, Athuman Kwariko wakinukuu maelekezo yaliyokuwa yanatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) katika mkutano wake na wachimbaji wadogo uliofanyika katika kata ya Nanyala wilayani Mbozi mkoani Songwe .
 Sehemu ya wachimbaji wa madini ya chokaa na ujenzi kutoka katika kata ya Nanyala wilayani Mbozi mkoani Songwe, wakifuatilia ufafanuzi uliokuwa unatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani)
Diwani wa Viti Maalum kutoka Tarafa ya Iyula iliyopo Wilayani Mbozi mkoani Songwe, Messiah Swella akiwasilisha kero yake kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) katika mkutano huo.

KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...