Kutokua makini katika uratibu, usimamizi na ujenzi wa mradi wa maji mkoani Njombe kumewaweka matatani baadhi ya watendaji wa serikali na wakandarasi waliopewa dhamana ya kujenga na kufikisha majisafi na salama kwa wananchi.

Mradi uliotiliwa shaka wa Ukalawa na Kitole umesubiriwa na wananchi kwa zaidi ya miaka mitano na bado umekua butu kukidhi kiu ya wakazi wa vijiji vya Ukalawa na Kitole. Mradi huo umejengwa na kampuni ya Kihanga Farm International iliyolipwa kiasi cha Shilingi Milioni 532 kati ya Shilingi Milioni 562.

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameelekeza wahusika walioshiriki katika mradi huo wakiwamo Watalaam wa maji wa Serikali popote walipo, Mhandisi Mshauri wa mradi na Mkandarasi wa mradi wasaidie Jeshi la Polisi kupata undani wa taarifa zinazohusu mradi, ikiwamo malipo yaliyofanyika wakati wananchi hawapati maji.

Mhe. Aweso (Mb) katika kikao kilichodumu kwa saa sita kilichowakutanisha watalaam wa maji, na baadhi ya walioshiriki katika ujenzi wa mradi wa maji Ukalawa-Kitole, amesema miradi ya maji sio kichaka cha kupitisha fedha na kusisitiza endapo mhusika yoyote atabainika kushiriki kuhujumu mradi huo, hata kama amestaafu utumishi wa umma, atatafutwa popote alipo na kufikishwa katika vyombo vya sheria. Baada ya kikao kumalizika baadhi ya wahusika kutoka kampuni iliyopewa kandarasi ya Kihanga Farm na wataalam wa maji wa serikali walioshiriki walikabidhiwa kwa vyombo husika ili kusaidia zaidi kwa taarifa muhimu.

Mhe. Aweso (Mb) amesema hakuna faida ya kuwa na mtalaam wa maji anayekabidhiwa mradi bila kujiridhisha na ubora wake kama taratibu zinavyotaka, ambapo imebainika moja ya udhaifu katika mradi wa maji Ukalawa-Kitole ni kwenda kinyume na mkataba, na kutozingatia ushauri wa Mhandisi Mshauri wa mradi na kubadili mfumo wa kusukuma maji kutoka wa kutumia jenereta, kwenda mfumo wa kutumia nishati ya jua (solar) wakati mazingira ya mradi sio rafiki kwa mfumo wa nishati ya jua.

Mhe. Aweso (Mb) ameagiza kutokana na udhaifu ulioonekana katika mradi huo ameagiza timu aliyoiunda akiwa mkoani Mbeya mwezi Oktoba 2018, ipite katika mradi wa maji Ukalawa na mradi wa Lugenge ambao madakio ya maji mawili yamekamilika lakini mradi bado hauridhishi na ukiwa katika asilimia 60 ya kazi pamoja na Mkandarasi kuongezewa muda.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Maji na Umwagiliaji 
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akiongea na watalaam wa maji, pamoja na baadhi ya wahusika walioshiriki katika ujenzi wa mradi wa maji Ukalawa-Kitole katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Christopher Ole Sendeka (kulia). 
1. Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akiwasikiliza baadhi ya wananchi watakaofaidika na mradi wa maji Lugenge mkoani Njombe. 
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Jumaa Aweso (Mb ) akipewa maelezo kuhusu kazi iliyoanza ya utandikaji wa mabomba kutoka katika dakio la maji kwenda katika tanki katika mradi wa maji Lugenge,pichani kati ni MKuu wa Mkoa wa Njombe Mh  Christopher Ole Sendeka 
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akipokea mrejesho wa wananchi kuhusu kero ya maji kando ya tanki la maji lililokamilika la mradi wa maji Lugenge. Mkandarasi kapewa mwezi mmoja kuhakikisha maji yanafika katika tanki hilo. 
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akiangalia mitambo katika mradi wa maji Kibena. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...