NAIBU Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Kakunda amezindua mpango wa mashindano ya mbio za baiskeli na kufanikisha kukusanya Sh milioni 280 kati ya Sh milioni 340 zinazotarajiwa kukusanywa kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu nchini.

Mashindano hayo yaliyopewa jina la 'Acacia Imara Pamoja Cycle Challenge', yameandaliwa na Kampuni ya Uchimbaji wa Madini nchini -Acacia kwa kushirikiana na Tasisi binafsi kutoka nchini Canada - CanEducate.

Akizungumza katika uzinduzi wa uchangiaji wa mashindano juzi jijini Dar es Salaam, Kakunda alitoa wito kwa wadau mbalimbali nchini kuchangia mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Novemba 3, mwaka huu katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Kakunda ambaye alimwakilisha Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo alisema malengo ya mashindano hayo yanaenda sambamba na malengo ya serikali katika kurahisisha mazingira ya utoaji elimu nchini. "Tangu Rais John Magufuli aingie madarakani na kufuta ada za shule pamoja na ada za ziada, hadi mwaka jana kumekuwapo na ongezeko la asilimia 44 la uandikishaji wanafunzi wapya wa elimu ya awali, ongezeko la asilimia 33 la uandikishaji wanafunzi wapya wa darasa la kwanza na wanafunzi wapya wanaojiunga na elimu ya sekondari wameongezeka kutoka 366,396 mwaka 2015 hadi 483,216 mwaka 2017", alisema.

Alisema hatua hizo zinahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali kama wanavyofanya Acacia katika kufikia malengo ya serikali.Aidha, Mkurugenzi wa Acacia nchini, Asa Mwaipopo alisema kwa mwaka jana pekee kampuni hiyo imejenga madarasa na kukarabati mabweni yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 100 wa kike katika Shule ya Sekondari Mwendakulima iliyopo wilayani Kahama.

Pia imefanikisha ujenzi wa maktaba sita katika shule zinazozunguka migodi ya kampuni hiyo."Tangu tuanze kushirikiana na CaEducate mwaka 2011 katika kuboresha sekta ya elimu nchini, Acacia imetumia zaidi ya sh milioni 450 zilizofikia shule 20 na wanafunzi zaidi ya 5000.

Meneja Mkuu Uhusiano na Uwezeshaji wa Jamiii kutoka kampuni ya Acacia Bi Noleen Dube akiwashukuru wadau waliojitokeza katika hafla ya uzinduzi wa mpango wa kuchangia elimu nchini kupitia mashindano ya baiskeli yanayofahamika ' Acacia Pamoja Imara Cycle Challenge' yanayotarajiwa kufanyika jijini Mwanza mwezi Novemba. Wengine ni pamoja na Naibu Waziri -Tamisemi, Joseph Kakunda (wa pili kulia), Mkurugenzi wa Acacia, Asa Mwaipopo, (wa tatu kulia) na Rais wa taasisi ya CanEducate ambayo ndio inaratibu mpango huo kwa kushirikiana na Acacia Bw. Rishi Ghuldu.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Acacia, Peter Geleta (wa kwanza kushoto), kulia kwake ni Meneja Uhusiano na Uwezeshaji ya Jamii, Noleen Dube, Mkurugenzi Mtendaji wa Acacia, Mhandisi Asa Mwaipopo na Naibu Waziri - Tamisemi, Joseph Kakunda pamoja na viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa mpango wa mashindano ya mbio za baiskeli, "Acacia Imara Pamoja Cycle Challenge" yenye lengo la kukusanya Sh milioni 340 kusaidia wanafunzi wasiomudu gharama za elimu nchini.
Mmoja wa wanufaika wa Mpango wa kusaidia wanafunzi wasiomudu gharama za elimu katika familia duni zinazonguka migodi ya Acacia, Yunista Marwa akizungumza katika hafla hiyo, namna mpango huo wa CanEducate ulivyomsaidia kuanzia kidato cha pili hadi alipohitimu kidato cha sita.

Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Kakunda akizungumza katika hafla ya kuzindua mpango wa kuchangia mashindano ya mbio za baiskeli yanayotarajiwa kufanyika Novemba 3, 2018 katika uwanja wa Kirumba jijini Mwanza kwa lengo la kuchangia huduma za elimu nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...