Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na wananchi wa kijiji cha Mpwayungu wilayani Chamwino baada ya kuhutubia mkutano wa hadhara kijijini hapo, Oktoba 20, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Bilinith Mahengeampeleke Afisa Kilimo wa mkoa Bw. Bernad Abraham  akakague mradi wa umwagiliaji wa Mpwayungu wilayani Chamwino ili kubaini waliohusika na ubadhilifu wa sh. bilioni 1.2 za mradi huo.

Alitoa agizo hilo jana jioni (Jumamosi, Oktoba 20, 2018) baada ya mbunge wa jimbo Mtera, Livingstone Lusinde kumuomba awasaidie kuhusu upotevu wa sh. bilioni 1.2 zilizotolewa kwa ajili ya mradi wa umwagiliaji ambazo matumizi yake hayajulikani.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi wilayani Chamwino, Dodoma alipokea ombi hilo la mbunge wakati akizungumza na wananchi wa Tarafa ya Mpwayungu, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mpwayungu.

Alisema mara baada ya Afisa Kilimo, Bw. Abraham kukamilisha ukaguzi wa mradi huo wa umwagiliaji apelekewe taarifa ili waliohusika na ubadhilifu wa kiasi hicho cha fedha wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alivunja kamati ya kusimamia huduma maji ya kijiji cha Mpwayungu na alimuagiza Mhandisi wa Maji wa wilaya ya Chamwino Bw. Godfrey Mbabaye aunde kamati mpya.

Waziri Mkuu alichua hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na utendaji wa kamati hiyo ambayo ilishindwa kutekeleza majukumu yake ikiwemo ujenzi wa vituo vya kuchotea maji licha ya kukusanya sh. milioni 20 kwa mwezi, mradi huo unavituo vinne tu.

Alisema kitendo cha kamati hiyo kushindwa kuongeza kujenga vituo vingine vya kuchotea maji licha ya kukusanya fedha nyingi kwa mwezi kinasababisha malalamiko kutoka kwa wananchi ambao ndio wanufaika wa mradi huo.

Pia Waziri Mkuu alimuagiza mhandisi huyo aombe taarifa ya akaunti ya benki ya mradi huo ili kubaini katika mfuko wa mradi huo una fedha kiasi na ndipo aunde kamati mpya ya maji ambayo anatakiwa ashirikishe wanawake kwa kuwa wao ndio wahusika wakuu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...