Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu akiwasili leo Novemba 17, 2018 katika Kiwanda cha samani cha Magereza Arusha kukagua sehemu mbalimbali ambazo moto umeteketeza sehemu ya kiwanda hicho. Kushoto kwake ni Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike.

Na Lucas Mboje, Arusha

KATIBU Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu pamoja na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike leo wametembelea Kiwanda cha Samani cha Arusha, mali ya Jeshi la Magereza ili kujionea athari mbalimbali iliyosababishwa na ajali ya moto iliyotokea juzi Novemba 16, 2018.

Akizungumza eneo la tukio Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu amesema kuwa ni vyema taasisi mbalimbali nchini pamoja na wananchi wakachukua tahadhali za majanga ya moto ili kuepusha hasara zinazoweza kujitokeza kufuatia majanga hayo.

Amesema kuwa Wizara yake itaendelea kuliwezesha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji vifaa vya kisasa ili liweze kukabiliana na majanga ya moto pindi yanapojitokeza. Aidha, Katibu Mkuu huyo, Meja Jenerali Kingu amelitaka Jeshi la Magereza kuhakikisha kuwa linafanya jitihada za haraka za kurejesha shughuli za uzalishaji katika kiwanda hicho ikiwemo kufanyia matengenezo baadhi ya mashine zilizoteketezwa na moto.
Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike(wa pili toka kulia) pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu(kulia), wakiangalia moja ya mashine mbalimbali ambazo zimeteketezwa na moto katika kiwanda cha Samani cha Magereza Arusha. Chanzo cha moto huo inasemekana ni hitilafu ya umeme ndani ya kiwanda hicho.

Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike amevishukru vyombo vya ulinzi na usalama ikiwemo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Jeshi la Polisi Mkoani Arusha sambamba na wananchi waliojitokeza kusaidia katika uzimaji wa moto huo ambao umeunguza sehemu ya kiwanda hicho.

“Nawashukru sana Jeshi la zimamoto na uokoaji Mkoani Arusha, Jeshi la Polisi pamoja na wananchi kwa kazi kubwa waliyoifanya siku ya tukio kwani niliarifiwa kuwa moto ulikuwa mkubwa lakini tunashukuru Mungu hatimaye uzimaji ulifanikiwa pamoja na hasara iliyojitokeza”. Alisema Jenerali Kasike.

Akizungumzia chanzo cha moto huo na hasara iliyojitokeza, Kamishna Jenerali Kasike amesema kuwa taarifa za awali zinaonesha kuwa moto huo ulisababishwa na hitilafu ya umeme ambayo ilisababisha kuteketea kwa baadhi ya mashine za kiwanda hicho pamoja na uharibu wa nyaraka mbalimbali za ofisi katika jengo la utawala.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu (wa kwanza kushoto) akitoa maelekezo mbalimbali kwa Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike(katikati). Kulia ni Kamishna wa Fedha na Mipango, Kamishna wa Magereza, Gideon Nkana ambaye ni Kiongozi wa Kamati Maalum ya kuchunguza tukio hilo.

Wakati huo huo, Kamishna Jenerali Phaustine Kasike ameunda Kamati maalum ya Maafisa watano kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Magereza ambayo itachunguza chanzo cha moto huo pamoja na kuwasilisha taarifa kamili ya hasara iliyojitokeza. Tume hiyo itaongozwa na Kamishna wa Fedha na Mipango wa Jeshi hilo, Kamishna wa Magereza, Gideon Nkana.

Kiwanda cha samani cha Magereza Arusha kilimikishwa rasmi kwa Jeshi la Magereza mwaka 1973 baada ya Azimio la Arusha mwaka 1967 ambapo tangu kipindi hicho kiwanda hicho kinajishughulisha na utengenezaji wa samani mbalimbali za ofisi na samani za majumbani. Pia kiwanda hiki hutumika kuwafundisha na kuwarekebisha wafungwa ili wamalizapo vifungo vyao waweze kujitegemea kupitia ujuzi waliojifunza.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...