Na Lydia Churi – Mahakama

Majaji watano kutoka Mahakama Kuu ya nchini China wameitembelea Mahakama ya Tanzania ili kujifunza namna mfumo wa utoaji haki wa Tanzania unavyofanya kazi na pia kubadilishana uzoefu kuhusu masuala yakisheria na utoaji haki.

Majaji hao kutoka jimbo la Zhejiang la nchini China pia wameitembelea Mahakama ya Tanzania kwa lengo la kujifunza zaidi na kubadilishana uzoefu hasa kuhusu adhabu zinazotolewa na Mahakama kwa ajili ya kuirekebisha jamii.

Akizungumza na Majaji hao, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Katarina Revocati amewaambia kuwa Mahakama ya Tanzania ni chombo huru kinachotekeleza majukumu yake kwa uhuru pasipo kuingiliwa na Mihimili mingine. Akizungumzia adhabu zinazotolewa na Mahakama katika kuirekebisha jamii hasa zile za kifungo cha nje, Msajili Mkuu alisema adhabu hizo hutolewa kwa mujibu wa sheria na kwa vigezo mbalimbali ikiwemo kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani na kufanya shughuli za uzalishaji ili kuisaidia jamii.

Alisema Mahakama ya Tanzania imekuwa ikishauri matumizi ya adhabu mbadala ikiwemo kazi za nje badala ya adhabu za kifungo gerezani. Kupitia adhabu hizi, wafungwa watatumika pia kufanya kazi za uzalishaji mali na kuisaidia jamii. Kwa upande wao, Majaji hao kutoka nchini China wamesema wamefika nchini kujifunza mfumo wa utoaji haki unavyofanya kazi na hasa kuhusu adhabu zinazotolewa na Mahakama katika kuirekebisha jamii kwa kuwa mfumo huo pia hutumiwa na Mahakama zao.

Kwa mujibu wa Majaji hao, China inazo fursa nyingi za kuwaendeleza wanasheria kitaaluma na hivyo wametoa wito kwa Mahakama ya Tanzania kutumia fursa hizo katika kuwaendeleza watumishi wake kama ambavyo nchi nyingine zimekuwa zikifanya.
Pichani ni Msajili Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati akiwa katika mazungumzo pamoja na Wahe. Majaji kutoka Mahakama Kuu Zhejiang iliyopo Jamhuri ya Watu wa China walipotembelea Ofisi ya Mhe. Msajili Mkuu, Novemba 16, 2018. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...