NA BALTAZAR MASHAKA MISUNGWI

WANANCHI wa vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza wametakiwa kulima kilimo chenye tija kitakachowanufaisha kiuchumi na kuondokana na umasikini.

Rai hiyo ilitolewa jana katika Kijiji cha Seeke wilayani Misungwi na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza wakati akizindua msimu mpya wa kilimo cha pamba kwa kugawa mbegu za zao hilo pamoja na kamba za vipimo vya kupandia kitaalamu.Alisema wakulima walime kilimo cha kisasa cha kibiashara, wazingatie masharti na kanuni kumi bora za kilimo, wakifanya hivyo wataongeza uzalishaji na kupata maendeleo ya kiuchumi na kipato.

Mongela alisema kwa kuwa serikali imewaletea mbegu kwa wakati wajitume na kulima kwa bidii kwani bila kujibidisha itawawia vigumu kupata mavuno mengi na kuonya wanaume kuacha tabia ya kukaa kwenye vijiwe vya kahawa badala yake wajikite kwenye kilimo.Aliigiza Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) kuhakikisha inasambaza kwa wakati dawa za viuadudu (viautilifu), vikipungua taarifa itolewe mapema na kuwataka maofisa ugani watoke ofisini waende vijijini wakawasaidie wakulima kwa kuwapa elimu.

Pia aliwataka wakulima ambao hawajakata masuke (miti ya pamba) msimu uliopita kuhakikisha ifikapo Novemba 20 wawe wameyakata na kuyachoma moto kwa kuwa ni chanzo kikubwa cha kuzalisha wadudu.“Pamba ni uchumi wa aina yake na ni muhimu tugeuke turudi tuikotoka tutajirike kwa kuwa mbegu zimeletwa mapema tulime na kupanda kwa wakati.Pia maofisa ugani tutoke twende tukawaelimishe wakulima wapande kwa mistari, wafundishwe jinsi ya kupulizia dawa,”alisema Mongela.

Aidha, afisa kilimo wa Wilaya ya Misungwi, Majid Kabyemela msimu huu wameweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa pamba kwa kubadili mbegu ya UK-91 ambayo uzalishaji wake unaonekana kushuka na wamesambaza tani 350 za mbegu mpya aina ya UKM-08.Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Misungwi Ratifa Malimi alisema siasa ni uchumi hivyo akawashauri wakulima kukipa kilimo cha pamba kipaumbele na wakifaya hivyo watakuwa wameitendea haki ilani ya uchaguzi ya CCM na kufanya maendeleo yasogee baada ya mivutano ya kisiasa.
Mkulima wa Kijiji cha Seeke wilayani Misungwi Charles Faya akipokea mbegu za pamba kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongela kuashiria kuanza kwa msimu wa kilimo cha zao hilo. Picha na Baltazar Mashaka

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...