Tanzania imeshinda tuzo ya utalii kwa kuonekana ni eneo bora zaidi la utalii duniani nchini Urusi kwa mwaka 2018 (The Best Destination to the World in the Category of Exotic Destination 2018).

Leo tarehe 21 Novemba 2018, Balozi wetu nchini Urusi Mhe. Maj. Gen. (Mst). Simon Mumwi atapokea Tuzo hiyo kutoka Jarida la kirusi la “National Geographic Magazine” jijini Moscow kwa niaba ya nchi. 

Tanzania imepata ushindi huo kutokana na kura zilizopigwa kwenye mtandao wa jarida hilo la “National Geographic Magazine” lililoshirikisha wapiga kura 263,000 kwa njia ya mtandao.

Hii ni mara ya tatu katika kipindi cha miaka saba tokea mwaka 2011, raia wa Urusi kupitia jarida hilo wanaichagua Tanzania kama eneo bora zaidi la utalii. Mwaka 2011, Zanzibar ilipata tuzo ya ‘Star Travel’ kama eneo bora zaidi la utalii wa ufukweni katika bara la Afrika na mwaka jana, Tanzania ilipata tuzo ya NGT na Tanzania ilishinda nafasi ya pili katika tuzo hiyo katika kundi la eneo bora la utalii duniani.

“National Geographic Traveller Awards” (NGT Awards) ni tuzo ya kifahari zaidi katika sekta ya utalii nchini Urusi na hutolewa na Jarida la kirusi la “National Geographic Magazine”.

Mafanikio hayo yanatokana na jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kupitia Ubalozi wetu Urusi, Wizara za Utalii za Tanzania Bara na Zanzibar, na Taasisi zote zinazosimamia masuala ya utalii za ndani na nje ya nchi katika kutangaza vivutio vya utalii kwa nchi mbalimbali duniani ikiwemo Urusi.Kupitia juhudi hizi, idadi ya watalii wanaokuja Tanzania kutoka Urusi imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa mfano, idadi hiyo imeongezeka kutoka watalii 4,021 mwaka 2012 hadi watalii 10,060 mwaka 2017. 

Wizara kupitia Ubalozi wetu itaendelea kuongeza juhudi za kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania na tunategemea kwa kushirikiana na wadau wengine katika juhudi hizi, idadi ya watalii kutoka Urusi wanaokuja nchini itaongezeka zaidi.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
21 Novemba 2018

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...