Na Estom Sanga-DSM 

Wadau wa Maendeleo na menejimenti ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF- wamekutana jijini DSM kwenye Ofisi Ndogo za Mfuko huo Kujadili pamoja na mambo mengine maandalizi ya zoezi la kufuatilia utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini litakalofanyika mwanzoni mwa mwezi ujao. 

Utaratibu huo wa kufuatilia utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini hufanyika mara mbili kwa mwaka na hujumuisha Maafisa wa Serikali na wadau wa Maendeleo wa ndani na nje ya nchi ambao hupata fursa ya kutembelea baadhi ya maeneo na kukutana na Walengwa na Viongozi wa Maeneo ya Utekelezaji wa Mpango. 

Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF imekuwa ikitekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini –PSSN- ulioanza mwaka 2012 katika baadhi ya Halmashauri za Wilaya kwa majaribio na kisha kutekelezwa nchini kote kufuatia mafanikio ya majaribio yaliyofanyika katika wilaya za Bagamoyo, Kibaha, Chamwino na Mbarali mkoani Mbeya. Kwa sasa Mpango huo unanufaisha Kaya takribani Milioni Moja na Laki Moja Tanzania Bara ,Unguja na Pemba ambako walengwa hupata ruzuku ya Masharti hususani katika nyanja za elimu na afya na ile isiyokuwa ya Masharti kwa lengo la kuboresha maisha ya walengwa . 

Kufuatia utekelezaji wa Mpango huo wa Kunusuru Kaya Maskini, Walengwa wa Mpango huo wameonyesha mabadiliko makubwa hususani katika uboresha ya makazi ,uanzishaji wa miradi ya kiuchumi huku suala la mahudhurio ya wanafunzi wanaotoka kwenye Kaya hizo shuleni na kwenye vituo vya afya yakiboreshwa zaidi. 

Serikali kupitia TASAF kwa sasa iko katika maandalizi ya Awamu ya Pili ya utekelezaji wa Mpango huo ambayo mkazo maalum utawekwa kwa Walengwa kufanya kazi na kuibua miradi itakayowaondolea kero kwa kushirikiana na Wataalamu walioko kwenye maeneo yao huku pia mkazo mkubwa ukiwekwa kwenye shughuli za uzalishaji mali ili waweze kukuza uchumi wao na hivyo kupunguza umaskini .
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bw.Ladislaus Mwamanga (katikati) akimsikiliza kiongozi wa Shughuli za TASAF katika Benki ya Dunia Bw. Mohamed Muderis (mwenye miwani).
Wadau wa Maendeleo na Menejimenti ya TASAF (picha ya juu na chini wakiwa katika mkutano wa kujadili utekelezaji wa Shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini jijini DSM.
Menejimenti ya TASAF akiwa katika mkutano na Wadau wa Maendeleo kwenye ukumbi wa Mikutano wa Mfuko huo kujadili masuala ya utekelezaji wa shughuli za Mfuko huo jijini DSM.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...