Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alhamisi tarehe 22 Novemba 2018 atafanya ziara ya kushughulikia migogoro ya ardhi nchini kwa kuanza kutembelea shamba la Singu na  Endasagu yaliyopo wilaya ya Babati mkoa wa Manyara kwa nia ya kutatua migogoro katika mashamba hayo baina ya wamiliki na wananchi.

Uamuzi wa Lukuvi kufanya ziara katika mashamba hayo ni moja ya jitihada zake za kushughulikia migogoro ya ardhi kutokana na uwepo kero na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusiana na huduma za ardhi.

Akiwa wilayani Babati, Lukuvi atakagua mashamba ya Singu na Endasagu sambamba na kusikiliza malalamiko ya wananchi kuhusiana na mashamba hayo na baadaye kutafuta ufumbuzi.

Aidha, katika mfululizo  wa kushughulikia migogoro ya ardhi, Lukuvi mara baada ya kurejea kutoka mkoani Manyara atafanya ziara katika halmashauri zote za mkoa Dar es Salaam,Wilaya za Kinondoni, Ilala, Kigamboni, Ubungo na Temeke ambapo mbali na mambo mengine atakagua na kuhamasisha zoezi la urasimishaji ambalo limeonekana kuwa na changamoto katika baadhi ya maeneo.

Vile vile, katika kuhakikisha migogoro ya ardhi inapungua nchini Waziri Lukuvi mwanzoni mwa mwezi Desemba  atakuwa na ziara ndefu itakayohusisha mikoa ya Songwe, Mbeya, Njombe, Iringa na Pwani ambapo wananchi watapata fursa ya kuwasilisha kero za ardhi kupitia programu ya Funguka kwa waziri.

Ziara hiyo ya Waziri Lukuvi ni muendelezo wa ziara zake za kushughulikia migogoro ya ardhi na hivi karibuni alikuwa mkoani Kilimanjaro ambapo aliweza kutatua migogoro ya ardhi ikiwemo ya mashamba makubwa katika wilaya za Hai, Moshi na Same.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...