Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA) imeamua kutoa ufafanuzi kwa jamii ya Watanzania kuhusu hali ya ongezekeo la joto katika baadhi ya maeneo hapa nchini huku ikifafanua kwenye baadhi ya mikoa joto limefikia asilimia 34.

Taarifa ya TMA kwa vyombo vya habari ambayo imetoa leo jijini Dar es Salaam imesema kwa kawaida kipindi cha Oktoba hadi Machi kila mwaka jua la utosi linakuwa katika maeneo ya kizio cha kusini mwa dunia na Tanzania ikiwa ni moja ya nchi zilizopo katika kizio cha kusini, huwa na hali ya joto kali katika maeneo mengi ikilinganishwa na miezi mingine. 

"Hapa nchini, vipindi vya jua la utosi vinafikia kilele kati ya mwishoni mwa Novemba na Desemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa). Jua la utosi huambatana na hali ya Joto kali kwa sababu kipindi hicho ndipo uso wa dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na jua kuliko maeneo mengine. Hali hii hushuhudiwa zaidi kunapokuwepo na upungufu wa mvua ambazo zingesaidia katika kupunguza hali ya joto katika kipindi husika,"imesema taarifa hiyo ya TMA.

Imefafanua wastani wa joto kwa Novemba na Desemba ni nyuzi joto 31.5 kwa mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba. Hata hivyo, mpaka kufika mwishoni mwa Novemba 2018 joto limeshafika nyuzi joto 34. Katika baadhi ya maeneo hapa nchini ikiwemo mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Morogoro, Dar es salaam, Pwani pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba ambapo msimu wa mvua za Vuli unaendelea kukumbwa na mtawanyiko hafifu wa mvua hali ya fukuto inachangia katika hali ya joto japo vipimo vya nyuzi joto katika baadhi ya maeneo hayo ni vya wastani.

Imeongeza kuwa vipindi hivyo vya joto kali vinatarajiwa kupungua kadiri mtawanyiko wa mvua za vuli utakavyoimarika Desemba mwaka huu wa 2018 huku ikifafanua kuwa hata hivyo ikizingatiwa kuwa hali ya joto inatarajiwa kujirudia tena Februari 2019, wakati wa kipindi cha pili cha jua la utosi. Aidha, taarifa za mwenendo wa joto, zinaendelea kutolewa katika 

utabiri wa kila siku na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na kwamba wanatoa mwito kwa wananchi kuendelea kufuatilia taarifa hizo na kuchukua hatua stahiki kila inapobidi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...