NA Vero Ignatus -ARUSHA

MFANYABIASHARA maarufu Jijini Arusha,Kamaljit Hanspaul (58), anayejishughulisha na shughuli mbalimbali na wenzake watatu wamehukumiwa kulipa faini ya Sh Milioni 60 au kwenda jela miaka miwili kila mmoja baada ya kukutwa na hatia ikiwemo kuajiri wafanyakazi watatu raia wa kigeni kufanya kazi nchini bila vibali.

Mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha,washitakiwa wengine ambao uraia uko kwenye mabano Vemula Shivakumar, (27), (India) Sathasivam Krishanth, (29) (India) na Ralph Leonard, (54), (Ujerumani),ambapo watuhumiwa wote wanne walikiri kutenda makosa hayo mwanzoni mwa wiki.

Akisoma hukumu hiyo jana,Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo,Niku Mwakatobe,alisema Mahakama hiyo imemtia hatiani Hanspaul katika mashitaka matatu ambayo ni kuajiri raia watatu wa kigeni ambao hawakuwa na vibali vya kufanya kazi nchini.

Alisema baada ya mshitakiwa huyo kukiri mashitaka hayo Mahakama inamtoza faini ya Sh Milioni 10 kila kosa au kifungo cha miaka miwili,huku washitakiwa wengine wakitozwa faini ya Sh Milioni 10 kila mmoja au kifungo cha miaka miwili baada ya kukutwa na hatia ya kufanya kazi nchini bila vibali.

Washitakiwa wote wanne waliachiwa huru baada ya kulipa faini hiyo Sh Milioni 60,ambapo katika uamuzi wake,Hakimu Niku aliwataka raia hao iwapo wanataka kuendelea kufanya kazi hapa nchini,wafuate taratibu na sheria zilizowekwa.Katika shauri hilo jamhuri ilikuwa ikiwakilishwa na Wakili Khalili Nuda huku utetezi ukiwakilishwa na Wakili Salumi Mushi,ambaye aliiomba Mahakama ipunguze adhabu ikizingatiwa ni mara ya kwanza kwa washitakiwa hao kukutwa na hatia na kuwa washitakiwa watatu ambao ni raia wa kigeni walishaaanza taratibu za kufuatilia vibali vya kufanya kazi nchini.

Naye Wakili Nuda aliiomba Mahakama licha ya watuhumiwa wote kutokuwa na rekodi ya kukutwa na hatia,wanaomba Mahakama iwaadhibu kwa mujibu wa sheria na kuomba iwaagize iwapo wanataka kuendelea kufanya kazi hapa nchini wafuate sheria na taratibu.

Awali katika shauri hilo namba 389 la mwaka huu kabla ya kusomewa hukumu hiyo washitakiwa hao walisomewa maelezo ya awali,ambapo Wakili Nuda alidai mshitakiwa wa kwanza,aliwaajiri Shivakumar, Krishanth na Ralph kufanya kazi kama washauri kwenye kampuni yake ya HansPaul Automechs iliyopo maeneo ya Njiro jijini hapa wakati akijua hawana vibali vya kufanya kazi nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...