Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ameshiriki ‘msaragamo’ wa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Ruvu iliyoko Kata ya Ruvu Darajani Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro.

Mheshimiwa Ole Nasha ameshiriki ujenzi huo na Wananchi wa Kijiji cha Ruvu Darajani wakati wa ziara ya kukagua miradi ya Elimu katika Wilaya ya Same ambapo amewataka wananchi kuendeleza jitihada hizo ili kuweza kuweka mazingira mazuri ya wanafunzi kusoma.

Kufuatia jitihada hizo za Wananchi Naibu Waziri Ole Nasha kupitia Wizara yake ameahidi kujenga vyumba viwili vya madarasa, mabweni mawili na matundu ya vyoo katika shule ya msingi Ruvu ikiwa ni kuunga mkono juhudi ambazo wananchi wa kijiji cha Ruvu Darajani wameonesha lakini pia kuwezesha wanafunzi kutulia shuleni na kusoma.

“Serikali ikiona eneo ambalo wananchi wameanza na wana hamasa kubwa ya kujiletea maendeleo haiwezi kusita kuja kusaidia, Wilaya ya Same mmeonesha mfano kupitia utaratibu wenu wa msaragambo tunaunga mkono jitihada hizo kwa kuwajengea vyumba vya madarasa, mabweni na matundu ya vyoo,” aliongeza Naibu Waziri Ole Nasha.

Aidha Naibu Waziri huyo amewataka wananchi wa Kijiji cha Ruvu Darajani ambao wanajihusisha na shughuli za ufugaji kutotumia watoto kuchunga mifugo badala yake kuhakikisha wanatumia fursa ya Elimu bure kuwaandikisha watoto wote wenye umri wa kuanza shule.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Same Rosemary Staki alimweleza Naibu Waziri wa Elimu kuwa changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Ruvu imetokana na ongezeko la Wanafunzi waliohamishiwa shule hiyo kutokana na shule walizokuwa wakisoma miundombinu yake kuathiriwa na mafuriko yaliyotokana na mvua za masika zilizonyesha mwaka huu.

Katika ziara hiyo Naibu Waizri Ole Nasha pia alitembelea shule ya Sekondari Makanya, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Same na Shule ya Sekondari Same ambapo ameridhishwa na namna ukarabati ulivyofanyika katika shule hiyo kongwe.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akishiriki ‘Msaragambo’ wa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Msingi Ruvu iliyoko Kata ya Ruvu Darajani Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro alipofanya ziara kukagua miradi ya Elimu inayotekelezwa katika Wilaya hiyo. 
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akikagua ukarabati wa miundombinu uliofanyika katika Shule ya Sekondari Same iliyoko Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro. Ameridhishwa na namna ukarabati huo ulivyofanyika na kuwataka kutunza miundombinu hiyo ili iweze kutumika kwa muda mrefu.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ruvu Darajani Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro. Amewataka kutumia fursa ya Elimu bure kuhakikisha wanaandikisha watoto wote wenye umri wa kuanza shule. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...