Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa madini Tanzania (GST) inapenda kuufahamisha umma kuhusiana na taarifa ambazo zimesambaa kupitia baadhi ya vyombo vya habari, ikiwemo mitandao ya kijamii juu ya uwezekano wa kulipuka kwa Mlima wa Oldoinyo Lengai ulioko Mkoani Arusha. Mnamo tarehe 9/12/2018 vyombo vya habari vya Aljazeera na CGTN vilitangaza taarifa iliyoelezea kuwepo kwa uwezekano wa kulipuka kwa Mlima Oldoinyo Lengai. Taarifa hizo ambazo zilitolewa kwa lugha ya kiingereza na kusambaa kwenye mitandao ya kijamii zilidai kwamba Mlima Oldoinyo Lengai ungeweza kulipuka muda wowote.

Kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na watafiti wa masuala ya jiosayansi ambao wamekuwa wakifanya tafiti za jiosayansi katika eneo la mlima Oldoinyo Lengai hususan kuratibu uwezekano wa kulipuka. Kwa bahati mbaya taarifa zinazopatikana au kutolewa na wataalamu hao huwa sio rasmi kulingana na hatua ya utafiti ambayo inakuwa imefikiwa kwa wakati huo. Taarifa hizo husambaa na kutolewa katika tafsiri nyingi zinazotofautiana na hatimaye kusababisha taharuki na sintofahamu miongoni mwa jamii.

Mlipuko wa volcano ni matokeo ya fukuto la joto kali katika matabaka ya miamba kwenye kina kirefu sana cha ardhi. Fukuto hilo la joto husababisha matabaka ya miamba kuyeyuka na kuwa katika hali ya uji-uji. Kutokana na nguvu za mgandamizo zinazosababishwa na kina cha miamba tabaka hilo la uji-uji (magma) husukumwa na kuelekea juu ambapo hurushwa juu ya uso wa ardhi na hiyo ndiyo volkano. Tabaka hilo la uji-uji huwa lina mchanganyiko wa vitu vingi kutegemeana na kiasili cha miamba iliyohusika katika kuzalisha tabaka hilo. 

Hali kadhalika, linaweza likasababisha kutiririka kwa lava, au kurushwa hewani kwa majivu ya miamba iliyoungua, na vipande vya miamba ambapo huambatana na gesi zenye sumu au kutokea vyote kwa pamoja. Mlima Oldoinyo Lengai ni mlima wenye Volkano ambayo ni ya kipekee duniani kote, ambayo hurusha majivu na lava ya Natrocarbonatite, ambapo majivu huambatana na gesi ya
  
kabon dayoksaidi ambayo husababisha kuwasha au hata kubabuka ngozi na inaweza kusabababisha kushindwa kupumua na hatimaye kupoteza Maisha. Madhara haya ni kwa viumbe wote hai wakiwemo binadamu,wanyama, ndege na wadudu. Lakini pia majivu na lava ya volcano husababisha uchafuzi wa vyanzo vya maji, kuchafua anga, kufukiwa kwa nyumba na mashamba na maeneo ya malisho ya mifugo. 

Mlima wa Oldonyo Lengai ni miongoni mwa volcano hai duniani. Kumbukumbu zinaonesha kwamba Oldonyo Lengai uliwahi kulipuka mwaka 1883, 1904, 1910, 1913, 1915, 1917, 1926. 1940, 1954, 1955, 1958, 1966, 2007, 2008, 2010 na 2013. Kutokana na historia na ukweli kwamba Oldonyo Lengai ni volcano hai, timu za wataalamu kutoka nchi mbalimbali hususan Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya wamekuwa wakifika kwa lengo la kufanya utafiti ambao hadi hivi sasa haujaweza kutoa taarifa ya kina ya kitaalamu kuhusiana na kutokea kwa volcano hiyo.

Ikumbukwe kwamba kutokea kwa mlipuko wa volkano kunategemea mabadiliko ya miamba hususan kiwango cha joto na nguvu ya msukumo na mgandamizo katika kina kirefu cha ardhi hali ambayo hutokana na nguvu za asili. Kutokana na hali hiyo inakuwa ni vigumu kuweza kutabiri muda, (saa na siku) utakaohitajika kwa eneo husika kufikia kiwango cha msukumo kuweza kusababisha kutokea kwa volcano. Aidha volcano inapofukuta kulipuka husababisha matetemeko ya ardhi pamoja na maporomoko ya udongo katika eneo husika. 

Hii hutokana na kupanda kwa uji wa volcano ambao huiunguza miamba katika njia yake na kusababisha miamba hiyo kukatika na hivyo ardhi kutikisika. Kutokana na maelezo hayo, GST inapenda kutoa tahadhari kwa umma pindi wanapoona dalili za kulipuka kwa volcano wachukue tahadhari, ikiwa ni pamoja na kuondoka katika eneo la kuzunguka mlima umbali wa kilomita 50 ili kuepuka madhara ya majivu, gesi na vipande vya miamba vinavyorushwa kutoka kwenye volcano. 

Hata hivyo GST inashauri kwamba eneo la mlima Oldonyo Lengai siyo eneo salama kwa Maisha ya binadamu na mifugo kwavile hewa inayotokana na volcano ya Oldoinyo Lengai ni hewa ya sumu ambayo haiwezi kuonekana kwa macho kwavile haina rangi. Tunapenda kutoa wito kwa mamlaka husika kuchukua hatua stahiki ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea kwa kuhakikisha kwamba watu hawaweki makazi ya kudumu kwenye eneo la mlima Oldonyo Lengai.

IMETOLEWA NA TAASISI YA JIOLOJIA NA UTAFITI WA MADINI TANZANIA
11/12/2018

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...