Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa hamsini na mbili wa Tanzania Bara wanatarajiwa kushiriki katika programu ya mafunzo ya uongozi kwa kipindi cha wiki moja kuanzia Jumatatu ya tarehe 3 Disemba, 2018 hadi Ijumaa ya tarehe 7 Disemba, 2018, mkoani Dodoma. 

Warsha hiyo ya mafunzo ambayo imeandaliwa na Taasisi ya UONGOZI kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) itafunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) leo. 

Kwa mujibu wa Taasisi ya UONGOZI, programu hii ya mafunzo ya uongozi, ni ya kwanza ya aina yake iliyoandaliwa mahususi kwa ajili ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa. 

“Lengo la programu hii ni kuimarisha uwezo wa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala katika kufanya maamuzi ya kimkakati, kuongoza watu na kusimamia rasilimali nyingine, pamoja na kujijengea sifa binafsi za uongozi,” alisema Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Prof. Joseph Semboja. 

Prof. Semboja pia alisema, “Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa wana nafasi muhimu katika kuwezesha ukuaji na maendeleo ya nchi. Hivyo, tunatarajia kwamba kupitia programu hii, uwezo wao wa kuongoza utaimarika na kuwawezesha kuchangia katika jitihada za kuleta maendeleo endelevu nchini na hatimaye, barani mwetu.” 

Prof. Semboja aliongezea kwamba huu ni mwendelezo wa jitihada za Taasisi ya UONGOZI na Ofisi ya Rais, TAMISEMI zinazolenga kuwafikia viongozi wengi iwezekanavyo wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ili kupanua uelewa wa masuala ya uongozi na kuongeza tija ya shughuli wanazozifanya za kuwatumikia wananchi. Kati ya Mei 2017 na Oktoba 2018, mafunzo ya uongozi yalitolewa kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa na Wilaya, kwa awamu tano tofauti. 

Warsha hiyo ya mafunzo ya siku tano itajumuisha mada kuu zifuatazo; Uongozi Binafsi na Akili Hisia, Mwingiliano na Mahusiano baina ya Viongozi wa Kisiasa na Viongozi Watendaji, Mawasiliano ya Kimkakati, Itifaki, Masuala yanayohusu Ulinzi na Usalama, Usimamizi wa Fedha za Umma na Rasilimali Nyingine, Manunuzi katika Sekta ya Umma na Udhibiti wa Madawa ya Kulevya. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...