Na Veronica Simba – Tabora
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amekemea kasi duni ya Mkandarasi anayetekeleza mradi wa umeme vijijini wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora na kumtaka ndani ya siku 30 awe ameunganisha umeme vijiji vingine vipya 15. Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ibili wilayani humo, Desemba 14, 2018, alipokuwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, Waziri Kalemani alimwagiza Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wa eneo hilo kumwandikia barua ya onyo la kukusudia kusitisha mkataba Mkandarasi husika endapo atashindwa kutekeleza agizo alilompa.

“Na siyo kusitisha tu; tukisitisha mkataba maana yake hatutakupatia kazi tena na tutakudai malipo ambayo tumekwishakulipa na hata kukupeleka mahakamani. Nataka kasi iongezeke maradufu,” alisisitiza Waziri. Aidha, Waziri aliwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kulipia gharama ya kuunganishiwa umeme ambayo ni shilingi 27,000 tu kwa kuwa ni huduma inayotolewa kupitia Mradi wa Umeme Vijijini (REA) huku akiwatahadharisha kuwa muda wa kutekeleza mradi huo ukipita watalazimika kulipia gharama kubwa zaidi.

Vilevile, aliwataka pindi wakishaunganishiwa umeme, wautumie kwa malengo ya kukuza vipato vyao na kuboresha maisha ikiwemo kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kuchakata mazao wanayolima ambayo ni karanga, pamba na tumbaku. Pia, aliwataka viongozi wa taasisi zinazotoa huduma kwa umma kama shule, vituo vya afya, masoko, polisi, mitambo ya maji, makanisa, misikiti, kutenga pesa na kulipia kiwango hicho cha shilingi 27,000 tu ili kuhakikisha taasisi zao zinaunganishiwa umeme hivyo kutoa huduma bora kwa wananchi.

 Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati) akikata utepe kabla ya kuwasha rasmi umeme katika nyumba ya mkazi wa kijiji cha Ibili wilayani Uyui, Mama Chausiku (mwenye fulana ya njano), Desemba 14, 2018. Kulia kwa Waziri ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Gift Msuya na wa kwanza kulia ni Mbunge wa Tabora Kaskazini, Almasi Maige.
 Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (kulia), akimpongeza Mama Chausiku (mwenye fulana ya njano), baada ya kuwasha rasmi umeme katika nyumba yake (inayoonekana pichani), akiwa katika ziara ya kazi kijijini Ibili, Wilaya ya Uyui, Desemba 14, 2018.
 Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Gift Msuya (aliyesimama), akimkaribisha Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (anayesaini kitabu) mkoani Tabora alipofika kwa ajili ya ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, Desemba 14, 2018.
 Mbunge wa Tabora Kaskazini, Almasi Maige, akimkaribisha Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa kwanza kulia-walioketi) mkoani Tabora alipofika kwa ajili ya ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, Desemba 14, 2018.

KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...