Na Veronica Simba - Dodoma

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuchukua hatua za makusudi ikiwemo kuwavua nyadhifa Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Uzalishaji, Mhandisi Abdallah Ikwasa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Usambazaji, Mhandisi Kahitwa Bashaija; kutokana na suala la kukatika umeme sehemu kubwa ya nchi mara kadhaa sasa.

Alitoa maagizo hayo Jumamosi Desemba 15, mwaka huu alipokutana kwa dharura na wajumbe wa Bodi hiyo Makao Makuu ya Wizara jijiji Dodoma.

Akizungumzia sababu za kutaka wakurugenzi hao wawajibishwe, Waziri Kalemani alisema ni kutokana na tatizo la kukosekana kwa umeme sehemu kubwa ya nchi mara nne na kwa kipindi cha muda mrefu unaofikia nusu saa, kwa sababu ambazo zimekuwa zikielezwa kuwa ni kutoka kwa Gridi ya Taifa, wakati nchi ina ziada ya umeme inayofikia wastani wa megawati 250.

Akifafanua zaidi, alisema kutokea kwa tatizo hilo kunamaanisha kuna uzembe katika usimamizi au kutokufuatilia maelekezo ya Serikali, au kunaweza kuwepo na hujuma kwa baadhi ya watumishi wasiokuwa wazalendo. “Nchi inapokuwa gizani hata kwa sekunde moja, maana yake hakuna usalama. Aidha, hakuna sababu ya wananchi kukosa umeme katika mazingira ambapo kuna umeme wa ziada.”

Katika maagizo yake kwa Bodi, mbali na kutaka Wakurugenzi husika wawajibishwe, aliagiza pia wachunguzwe ikiwa ni pamoja na waliohusika kwa namna moja ama nyingine. Aidha, aliitaka Bodi kuunda Timu mahsusi kuanzia siku hiyo (Desemba 15), ili ichunguze na kufuatilia suala hilo, ikihusisha tasnia na taasisi mbalimbali, zaidi ya TANESCO.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (kulia) akizungumza na wajumbe wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) (hawapo pichani) kuhusu hatua za kuchukua kutokana na suala la kukatika umeme sehemu kubwa ya nchi mara kadhaa. Waziri alikutana na Bodi hiyo Desemba 15, 2018 Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wajumbe wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhusu hatua za kuchukua kutokana na suala la kukatika umeme sehemu kubwa ya nchi mara kadhaa. Waziri alikutana na Bodi hiyo Desemba 15, 2018 Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma. Kulia kwa Waziri ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua.
Wajumbe wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wakimsikiliza Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) alipokutana nao na kuwapa maagizo kuhusu hatua za kuchukua kutokana na suala la kukatika umeme sehemu kubwa ya nchi mara kadhaa. Waziri alikutana na Bodi hiyo Desemba 15, 2018 Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...