Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

JANUARI 11,2019 yaani jana tu nami niliungana na mamilioni ya Watanzania kutazama angani wakati wa ujio wa ndege yetu mpya ya Airbus 220-300 inawasili.

Ndege hiyo iliwasili katika ardhi ya Tanzania saa 8:30 mchana ,ilikuwa kwenye Uwanja wa Ndege wa zamani katika Jiji la Dar es Salaam.Hakika ilikuwa raha wakati ndege hiyo mpya na kisasa inawasili .

Kwa kuwa nami ni mkazi wa Dar es Salaam nikaona haitoshi kutazama tu angani wakati naweza kwenda kuiona kwa karibu.Nikaona isiwe taaabu bwana, saa nne asubuhi nikawa nipo uwanjani nasubiri mali mpya ya Tanzania.

Unashangaa ninaposema mali mpya? Huo ndio ukweli wenyewe maana Serikali yetu imenunua ndege hiyo kwa fedha tasilimu.Ni ndege ambayo ndio toleo jipya kwa sasa ni Tanzania tu ndio tunayo kwa Bara zima hili la Afrika.

Unayesoma makala haya ningekuwa nakuona au nakuelezea mbele yangu ningekwambia piga makofi.Ila kwa kuwa unaisoma utachagua mwenyewe unataka kushangilia kwa staili gani.Ujue si jambo dogo kununua ndege tena bila kukopa fedha kwa mtu.

Kabla ya kwenda mbali naomba niwapongeze Watanzania wote kwa kukubali kutenga muda wenu wa kuangalia angani wakati ndege inawasili.Mlikubali kubadili ratiba ya kazi ya macho ya kuona kwa siku ya jana.Uzuri wa Mungu kila mtu alimmilikisha viuongo na kisha kumuacha apange mwenyewe anavitumiaje.

Huenda bila ujio wa ndege hiyo kuna Watanzania macho yao yangekuwa yanaangalia mashamba ya mpunga,yangekuwa yanaangalia shughuli za kilimo au hata yangekuwa yanaangalia marudio ya mechi za mpira ambazo zinaendelea katika ligi mbalimbali duniani.

Kwa jana Watanzania wakasema isiwe tabu macho yote angani.Hongereni kwa uzalendo wenu kwa Taifa letu la Tanzania.Taifa ambalo linakila kitu cha kujivunia.Ni Taifa ambalo lilikosa ndege tu lakini nalo limebaki historia.Tunazo.

Hadi kufika jana sasa tunamiliki ndege zetu wenyewe mpya kabisa sita na ndege ya saba aina ya Dream liner itaingia nchini mwaka huu huu.Usishingae ndio hivyo tena.Kwa lugha za mtaani tunasema kwenye sekta ya ndege Tanzania kumenoga,kumedamshi na hata ukitaka kusema mambo ni moto utakuwa sawa.

Jana kama ambavyo nimetangulia kueleza hapo juu sikutaka kujipunja kwani mapema nilishaingia uwanja wa ndege na ikabaki kusubiri ndege yetu itue.Uwanjani kila ambaye nilikuwa namuangalia usoni alikuwa ametawaliwa na furaha.Ugumu wa Januari hakufanya tushindwe kuonesha furaha iliyopo moyoni.

Tanzania imekubali kuanza katika kuboresha sekta ya anga.Basi wakati tunasubiri ndege ije wananchi waliokuwepo hapo walikuwa wakipata burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali wakiongozwa na bendi ya TOT.

Sauti ya mwanamama Hadija Kopa ilipenya kwenye sikio la kila akiyekuwa uwanjani.Kama unavyomjua Hadija kwa mashauzi yake akiwa ameshika kipaza sauti.Mbona ilikuwa raha.Mama anazeekana uhodari wake.

Ujue bwana pamoja na yote hayo moyo,akili na mwili vyote vinaniambia nachelewa kutoa pongezi kwa Rais wetu mpendwa Dk.John Magufuli.Kwa kuwa moyo wangu unaona nachelewa na mimi sitaki kugombana nao,naomba niseme hivi "Hongera Rais Magufuli kwa uzalendo wako kwa Taifa letu.Hongera Rais kwa mipango na mikakati inayotekelezeka.

" Hongera Rais Magufuli kwa dhamira yako njema kwa Taifa letu,tangu Watanzania tukuchague ili uwe Rais wetu ndani ya miaka mitatu umenunua ndege sita na ya saba itakuja karibuni.Hongera kwa kazi nzuri unayofanya ya kuboresha sekta ya anga.

Hongera Rais Magufuli kwani dhamira yako kuhusu Tanzania mpya tunaiona kwa vitendo.Hongera....Hongera...Hongera Rais,jukumu langu na Watanzania wengine ni kuendelea kukuombea kwa Mungu akupe afya njema na maisha marefu."

Eti unajiuliza hongera zote hizi kwa Rais za nini? Sitaki kumjibu anayeulizwa swali la aina hii maana huenda haishi ndani ya nchi.Watanzania wanaona yanayofanywa na Rais Magufuli. Watanzania ni mashuhuda wa mambo makubwa yanayofanywa na Rais.Kuna ndege sita tayari zipo nchini halafu tusimsifu na kumpongeza.Itakuwa dhambi tena dhambi kubwa.Binafsi sitaki kuwa kwenye dhambi hiyo acha nirudie tena kusema "Hongera Rais wangu."

Najua wako wanaoumizwa na kasi ya maendeleo ambayo Tanzania inayafanya kwa sasa.Hata hivyo watu wa aina hiyo wamechelewa na wataendelea kuumia sana.Walitamani tubaki hatuna ndege waendelee kusema.

Najua wengine ndio mtaji wao wa kuombea kura.Wakati wa kampeni tulikuwa tunawasikia wanasema hooo Rwanda ni nchi ndogo wanandege kibao lakini Tanzania pamoja na ukubwa wake haina ndege.Walikuwa wanapata kura kwa kusema maneno kama hayo.

Unadhani kesho watazungumza lugha gani ya kuombea kura kwa wananchi.Walioona hiyo ndio stahili ya kuombea kura kwa kuorodhesha matatizo yetu.Kwa sasa wameumia.Tena wameumia haswa.Hata hivyo hiyo si ajenda yangu maana naona unakunja sura.

Kwanza Rais wetu ameshasema maendeleo hayana chama.Watanzania wote ni jukumu letu kuijenga Tanzania mpya.Na kweli Watanzania wameamka haswaa.Wamekuwa wamoja na wanachotaka kusikia ni kauli za kuhamasisha maendeleo. Zile kauli za kukejeli mambo ya maendeleo hakuna mwenye muda nazo tena.Kweli Rais amefanikiwa kutuondoa kwenye aibu.Leo kila kinachofanyika kinatokana na fedha zetu.

Kila unachokiona kinafanyika msingi mkubwa ni kodi ya Mtanzania.Hivyo kama tunazungumzia ujio wa ndege mpya maana yake wewe unayelipa kodi fedha yako imetumika kununua ndege.Kwa lugha rahisi unamiliki ndege ambayo umeinunua kwa fedha yako kupitia kodi.

Halafu nikwambie kitu,nilitaka kusahau .Jana wakati ndege inakuja viongozi wa dini walipata nafasi ya kuombea dua kwa akili ya Taifa.Ni jambo la kawaida kuomba dua lakini nikiri Askofu Zacharia Kakobe kabla ya kuomba dua aliomba azungumze japo kidogo.

Kwanza nilianza kujiuliza Askofu Kakobe anataka kuzungumza nini? Ujue Askofu Kakobe kwa miaka mingi amekuwa akionekana zaidi kwenye mikutano ya na vikao vya wapinzani.Amekuwa akitoa matamko ya kuonesha hakuna ambacho kimefanyika.Mzee yule amekiri kazi ambayo Rais Magufuli anaifanya yeye pamoja na ubishi wake lakini amekubali.Ametamka mwenyeweee.Kweli tena.

"Mimi ni mbishi sana katika kukubali,leo mpaka nimekuja hapa Rais amenikuna kwa mambo anayoyafanya kwa akili ya nchi yetu.Anastahili sifa na heshima.Najua hawawezi kukusifu watu wote Rais Na ukiona unasifiwa na kila mtu basi kuna tatizo.Niseme tu unafanya kazi nzuri Rais Na lazima tuseme hadharani kwa kukusifu na kukuheshimu," amesema Askofu Kakobe.

Amezungumza mengi lakini hicho ambacho nimekinukuu ni moja ya kauli zake muhimu ambazo zitadumu kwenye masikio ya Watanzania kwa miaka mingi ijayo.Hongera Askofu Kakobe kwa kueleza ukweli wa kutoka moyoni mwako.Najua wapo watakaokubeza lakini umesema ukweli na kweli itakuweka huru.

Pamoja na yote hayo ukweli ni kwamba Watanzania huu ni wakati wa kuungana na Rais Magufuli kuhakikisha mipango yake ya kuiletea nchi maendeleo inafanikiwa.Nakumbuka wakati anazungumza uwanjani hapo Rais amesema Watanzania tunaweza kufanya mambo makubwa zaidi na kama ndege kuja basi zitaendelea kuja zaidi na zaidi.

Amehimiza Watanzania kuijenga Tanzania mpya.Tanzania ambayo itakuwa na huduma bora katika sekta mbalimbali na kwake anaamini anaiona Tanzania mpya ambayo itakuwa haina tofauti na Ulaya.Rais Watanzania wamekusikia na kiuu ya kila nmoja wetu ni kuiona Tanzania mpya chini ya uongozi wako .

Nikwambie tu Rais wangu huko mtaani Watanzania wanakukubali sana.Wanasema umekuja wakati sahihi na wanaamini huenda ujio wako ni mpango wa Mungu.Naomba kama itakupendeza Mheshimiwa Rais kwa hii kazi nzuri ambayo unaifanya naomba agizia chochote nitakuja kulipa.Najua kwa nafasi yako unaweza kupata chochote na kwa wakati wowote,lakini kwa furaha niliyonayo naomba agiza chochote mimi nitalipa tu.

Tuwasiliane kwa 0713833822.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...