*Amtaka kumthibitishia maneno yake kuwa Bunge nichombo dhaifu
*Amtaka ajitafakari ...asema kauli zake nje ya nchi zimemsikitisha 

Na Ripota Wetu, Globu ya jamii 

HATIMAYE Spika wa Bunge Job Ndugai ametoa maagizo ya kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad kufika katika Kamati ya Maadili ya Bunge ifikapo Januari 21 mwaka huu na iwapo atashindwa kufika atapelekwa akiwa kwenye pingu.

Spika Ndugai ametoa kauli hiyo leo Mjini Dodoma wakati anazungumza na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini alipokuwa akielezea namna ambavyo Prof.Assad ametoa kauli ambayo haikustahili kuitoa kwa Bunge.

Siku za karibuni Prof.Assad wakati anahojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa ambapo aliulizwa kuhusu jitihada ambazo ofisi ya CAG inafanya kila mwaka kwa kukagua na kutoa ripoti ambazo zinaoonesha kuna ubadhirifu wa fedha ambapo alijibu kazi yake ni kufanya ukaguzi na kukabidhi ripoti kwa Bunge, hivyo Bunge ndilo dhaifu kwa kushindwa kufanyia kazi ripoti hizo.

Hivyo kauli hiyo ya Profesa Assad kudai Bunge ni dhaifu ndiyo iliyosababisha Spika wa Bunge leo kutangaza kumuita Kamati ya Maadili ili akahojiwe na kamati hiyo na iwapo atakaidi atapelekwa kwa pingu na hiyo itatosha kuthibitisha Bunge si dhaifu.

"Bunge tumepokea kwa masikitiko makubwa kauli ya Profesa Assad.Anataka kuonesha kuwa ripoti ambazo anazitoa kwa Bunge hazifanyiwi kazi au zikifika Bungeni basi hakuna kinachoendelea kwa kuwekwa pembeni bila kufanyiwa kazi.Hii si kweli kabisa,"amesema Spika Ndugai na kuongeza "CAG na maofisa wake wamekuwa wakiingia kwenye Kamati ya Kudumu ua Hesabu za Serikali za Mitaa pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma.

"Ripoti za CAG zikifika kwenye kamati hizo ambazo kimsingi zinaongozwa na upinzani , maofisa wa ofisi ya CAG wanakuwepo kueleza mapungufu waliyobaini wakati wa ukaguzi na hatua ambazo zinastahili kuchukuliwa.Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani kuna jitihada kubwa zimefanyika na zinaendelea kufanyika katika kudhibiti matumizi ya fedha za umma, kuna mabadiliko makubwa yamefanyika kwa ushauri wa CAG,"amesema.

Pamoja na hayo Spika Bunge amehoji ni hatua gani ambazo Profesa Assad anataka zichukuliwe huku akitumia nafasi hiyo kuwataka maofisa wa Serikali kuacha kutoa kauli za kulidhalilisha na kwamba Bunge linaweza kukosolewa lakini si kwa kauli za dharau.Pia amesema si uungwana kuisema nchi yako vibaya ukiwa nje ya nchi huku akitumia nafasi hiyo kumtaka Profesa Assad kujitathimini kwani Bunge haliko tayari kufanya kazi na mtu ambaye anaona chombo hicho ni dhaifu.

"Kwa mujibu wa kifungu cha 4, kifungu kidogo cha kwanza A, cha nyongeza ya nane ya kanuni za Kudumu za Bunge toleo la Januari 2016 suala hili nalipeleka katika kamati ya haki , maadili na madaraka ya Bunge ili walifanyie kazi na kunishauri na kwa maana hiyo kulishauri Bunge.

"Hivyo Profesa Assad anatakiwa kujitokeza Januari 21,2018 aende kujieleza kwenye kamati hiyo ili akathibitishe maelezo yake ambayo ameyatoa mahakamani.Na mnafahamu pamoja hatuna polisi, hatuna nini ila tunaweza kumleta mtu kwa pingu kwani tunataka kumthibitishia sisi sio dhaifu,"amesema Spika Ndugai.
 Baadhi ya Wanahabari wakimsikiliza Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai (Mb), aalipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma   leo kuhusu kauli za kudhalilisha Bunge zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),  Profesa Mussa Assad na Mbunge wa Kawe, Mhe. Halima Mdee. 
 Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai (Mb), akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu kauli za kudhalilisha Bunge zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),  Profesa Mussa Assad na Mbunge wa Kawe, Mhe. Halima Mdee.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...