Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Professa Abiud Kaswamila akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo mfano wa hundi ya Sh milioni 500,000 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya Afya Samunge na Arash wilayani humo zilizotolewa na NCAA kama sehemu ya mchango wa shughuli za maendeleo.
 Viongozi wa wilaya ya Ngorongoro na Karatu mkoani Arusha wakiwa wameshika hundi za mfano wa fedha zilizotolewa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Sh Bilioni 1 walizokabidhiwa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya wilaya ya Karatu na vituo viwili vya afya wilayani Ngorongoro.
 Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo akimkabidhi Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro Rashid Taka mfano wa hundi ya Sh milioni 500 zilizotolewa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa ajili ya ujenzi wa vituo viwili vya afya katika Kijiji cha Samunge na Arash wilayani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo akimkabidhi Mkuu wa wilaya ya Karatu Theresia Mahongo mfano wa hundi ya Sh milioni 500 zilizotolewa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa ajili ya ujenzi wa vituo viwili vya afya katika Kijiji cha Samunge na Arash wilayani humo. 


NA MWANDISHI WETU, ARUSHA


MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi, Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), Profesa Abiud Kaswamila amekabidhi Sh bilioni 1 za ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Karatu na vituo viwili vya afya wilayani Ngorongoro.

  Mchango huo wa maendeleo kutoka NCAA ulipokelewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo, ambapo wilaya ya Karatu imepokea Sh milioni 500 na Ngorongoro Sh milioni 500.Akizungumza wakati wa kukabidhi mchango huo Prof. Kaswamila alisema, msaada huo utakuwa chachu ya uhifadhi endelevu ikizingantiwa wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo ni wadau wakubwa.

 “Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inayo majukumu makubwa matatu, kuhifadhi maliasili na malikale, kuendeleaza wenyeji na kuendeleza utalii,” alisema Prof Kaswamila na kuongeza:“Katika kuendeleza majukumu hayo chanzo kikuu cha mapato ni utalii, aidha maendeleo ya utalii yatafikiwa iwapo maliasili zilizopo ndani ya hifadhi wakiwamo wanyamapori wanahifadhiwa kwa kushirikiana na wenyeji wa Ngorongoro na jamii inayozunguka hifadhi,” alisema.

Alisema NCAA imekuwa ikichangia miradi ya maendeleo kupitia ujirani mwema ambapo mwaka 2016-2017 ilitumia Sh 359,117,500 na mwaka 2017-2018 Sh 295,000,000 na mwaka 2018-2019 imetenga Sh 1,415,000,000 kufadhili miradi ya ujirani mwema.Kwa upande wake Gambo akipokea hundi hizo kisha kuzikabidhi kwa wakuu wa wilaya husika alisema, tangu nchi ilipopata Uhuru ni wilaya ya Monduli na Arumeru ndio zilizokuwa na hospitali za wilaya.

 Kutokana na juhudi hizo Gambo aliishukuru Bodi ya NCAA kwa kutoa fedha hizo akisema zimekua chachu kwa wananchi wa Kata ya Samunge wilayani Ngorongoro ambao baada ya kusikia habari hizo walianza kuchimba misingi nane ya ujenzi wa kituo chao cha afya kwa kujitolea.“Kwa wilaya ya Ngorongoro Sh milioni 400 zitakwenda kujenga kituo cha Afya Samunge na Sh milioni 100 zitakwenda Kata ya Arash kujenga Kituo cha Afya, wilaya ya Karatu wao watazielekeza zote kwenye ujenzi wa Hospitali ya wilaya,” alisema Gambo.

Aidha Mkuu wa wilaya ya Karatu Theresia Mahongo alishukuru kupokea fedha hizo na kuahidi kuwahamasisha wananchi kuanza kufanya kazi za kujitolea kuanzia wiki ijayo.Naye Mkuu wilaya ya Ngorongoro Rashid Taka alisema, mchango huo umekuwa ni neema kwao kwani umewafungulia ukurasa mpya wa maendeleo ya sekta ya afya.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...