Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elias Kwandikwa, amewahakikishia wananchi na watumiaji wa barabara ya Morogoro-Dodoma kuwa mawasiliano ya barabara hiyo sehemu ya maingilio ya daraja la Dumila yamerudi kama ilivyokuwa awali.

Kauli hiyo ameitoa leo mkoani Morogoro, alipofika darajani hapo kujionea athari za mvua zilizosababisha kubomoka kwa daraja hilo na wananchi kushindwa kutumia barabara hiyo kwa takriban masaa saba. 

"Kama mlivyoshuhudia tangu asubuhi tumeanza kazi za kurudisha mawasiliano katika barabara hii, matengenezo yakamilika na wananchi tayari wameshaanza kutumia barabara", amesema Naibu Waziri Kwandikwa.

Aidha, ameupaongeza Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Morogoro, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Kampuni ya ujenzi ya Yapi Merkez na wadau wote waliojitokeza katika kuhakikisha wanashirikiana bega kwa bega ili kurudisha mawasiliano katika eneo hilo.

Ameongeza kuwa katika kuhakikisha mawasiliano ya barabara yanakuwa imara, Serikali ipo katika mpango wa kuboresha barabara hiyo ambapo kwa sasa wataalam wanafanya usanifu wa barabara hiyo na pindi usanifu huo utakapokamilika basi ujenzi wake utaanza mara moja na wataanza na sehemu korofi.

Awali akitoa taarifa kwa Naibu Waziri huyo, Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Steven Kebwe, amesema kuwa uongozi wa mkoa ulifika eneo la tukio na kuanza kushirikiana na TANROADS mkoa kuhakikisha miundombinu hiyo inarejea mapema.Amewataka wananchi kujitolea kupanda matete na magugu maji katika eneo hilo ili kuelekeza maji yanayopita katika mto huo kuelekea sehemu husika.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS mkoa wa Morogoro, Mhandisi Dorothy Ntenga, amesema kuwa kazi zilizokuwa zikifanyika katika maingilio ya daraja hilo ilikuwa ni kuweka mawe makubwa na kokoto sehemu iliyobomoka.Amefafanua kuwa kutokana na sehemu hiyo kuwa na maji mengi na mchanga mwingi, wamefikiria kufanya usanifu wa daraja hilo utakaoleta suluhisho la kudumu.


Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Magari yakionekana kupita katika daraja la Dumila ambalo liliathirika na mvua zilizonyesha usiku wa tarehe 15/1/2019, na kukata mawasiliano katika mkoa wa Morogoro na Dodoma kwa takriban saa 7.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Steven Kebwe, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa (katikati), mara baada ya kuwasili katika daraja la Dumila lililoathirika na mvua zilizonyesha usiku wa tarehe 15/1/2019 na kuvunja maingilio ya daraja hilo mkoani Morogoro.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Morogoro, Mhandisi Dorothy Ntenga, akimueleza Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, hatua zilizochukuliwa na wakala huo katika matengenezo ya maingilio ya daraja la Dumila lililoathirika na mvua zilizonyesha usiku wa tarehe 15/1/2019, mkoani humo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akitazama athari za mvua zilizonyesha na kuharibu sehemu ya maingilio daraja la Dumila, mkoani Morogoro.
Kazi za ujazaji wa mawe na kokoto zilizokuwa zikifanyika katika kurekebisha athari za mvua zilizonyesha na kubomoa maingilio ya daraja la Dumila, mkoani Morogoro. Daraja hilo liko katika hatua za usanifu wa kina wa kuongeza tuta la daraja hilo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...