NA. WAMJW, Dar es Salaam.

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umejivunia kuongeza wigo wa wanufaika kwa kuwafikia Wananchi mbalimbali ikiwemo Wakulima kupitia vyama vyao vya ushirika kwenye huduma ya Ushirika Afya na watoto kupitia huduma ya Toto Afya Kadi. Mfuko pia umewezesha upatikanaji wa huduma za Madaktari Bingwa katika mikoa ya pembezoni pamoja na kuwezesha upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa katika Hospitali hapa nchini.

Hayo yameelezwa na Meneja Uhusiano wa Mfuko huo Bi. Anjela Mziray wakati wa ziara maalum ya Maafisa Habari wa Wizara ya Afya na taasisi zake katika kampeni maalum ya ‘Tumeboresha Sekta ya Afya’ inayolenga kueleza mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli.

Wakiwa Makao Makuu ya NHIF, Maafisa hao waliweza kutembelea maeneo mbalimbali ya Mfuko huo kujionea namna huduma zinazotolewa na Mfuko huo sambamba na mafaniko waliyofikia katika sekta ya Afya.

Awali akizungumza mambo mbalimbali Bi. Anjela Mziray aliwaeleza Maafisa hao kuwa Serikali inakusudia kuwafikia wananchi wote na huduma bora za afya. Katika kutekeleza hili Mfuko umewezesha Madaktari Bingwa wa magonjwa ya mbalimbali kama ya Wanawake, watoto, moyo, macho, kinywa na pua na mabingwa wa upasuaji kutoa huduma katika mikoa ya pembezoni kwa kipindi maalum.

"Kwa ujumla watu zaidi ya 20,289 wamefikiwa na huduma hii na kati ya hao watu 938 wamefanyiwa upasuaji wa kitalaam na hii ni katika mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa, Lindi, Mara, Manyara, Geita, Njombe na Ruvuma huku baadhi ya mikoa tukienda mara mbili” alieleza Bi. Anjela Mziray.

Aidha, katika mafaniko mengine ya kuboresha upatikanaji wa huduma, Mfuko unashiriki juhudi za Serikali za uwekezaji katika viwanda. Mfuko kwa kushirikiana na baadhi ya taasisi zingine unawekeza katika kiwanda cha uzalishaji wa bidhaa za hospitali zitokanazo na malighafi ya pamba na kiwanda hiko kitajengwa Bariadi Mkoani Simiyu huku kikitarajiwa kuzalisha aina 24 za bidhaa hizo. Wadau wengine wanaoshiriki katika uwekezaji huu ni pamoja na Serikali ya mkoa wa Simiyu, WCF, TFDA, TBS, MSD, TIB, TIRDO na taasisi zingine.

Katika jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata huduma, alieleza kuwa Mfuko kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani umenawezesha wamama wajawazito kupata bima ya afya ili waweze kupata huduma katika hospitali. Mpaka sasa wajawazito wapatao 1,044,000 wameshafikiwa na mpango huu katika mikoa ya Tanga, Mbeya, Njombe, Lindi na Mtwara.

Mfuko huo pia umeweza kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa kutumia mifumo ya Tehama inayowezesha kutambua wanachama katika vituo, kurahisisha ulipaji wa madai ya watoa huduma kwa wakati, kurahisisha usajili wa wanachama na kuharakisha utoaji wa vitambulisho.

Akizungumzia hili Meneja wa Mifumo ya Tehama Bw. Bakari Yahaya alisema kwa sasa mifumo inamwezesha mwanachama kupata ujumbe mfupi kwenye simu yake mara tu kadi yake au ya mtegemezi wake inapotumika kwa matibabu. 

Mfuko huu sasa umefanikiwa kuwa na ofisi zake katika mikoa yote ikiwemo Tanzania Bara na Zanzibar huku wakiboresha mfumo wa mawasiliano kwa kuwa na kituo cha huduma kwa wateja kwa ajili ya kupokea simu za wadau siku zote za juma bila malipo kwa wapigaji. Simu hiyo ni 0800 110063.

Akimalizia maelezo yake alisema, Mfuko umefanikiwa kupata cheti cha ubora wa huduma kwa viwango vya kimataifa ( ISO 9001:2015). "Katika hili tunajivunia kuimarika kwa huduma na ufanisi katika utekelezaji majukumu ya Mfuko kwa manufaa ya wadau wote wa Mfuko" alisema Bi. Mziray.

 Meneja Uhusiano wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bi. Angela Mziray akizungumza wakati wa ziara maalum ya Maafisa habari wa Wizara ya Afya na taasisi zake katika kampeni maalum ya ‘Tunaboresha Sekta ya Afya’ inayolenga kueleza mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli.  leo 11.1.2019, Makao makuu ya Mfuko huo Jijini Dar es Salaam
 Afisa wa kitengo cha Tehama Charles Charles akionesha namna ya mfuko wa kisasa unavyofanya kazi katika kitengo cha tehama
 Msimamizi wa nyaraka wa NHIF, Erasto Msigwa akieleza namna mfumo huo unavyofanya kazi  wa kutunza kumbukumbu kwa njia ya kisasa
Sabrina Mponda wa kitengo cha CALL CENTER akitoa maelezo namna huduma wanayotoa ikiwemo kupokea simu zaidi ya 200 kwa siku katika kituo hicho ambapo wamefanikiwa kuwafikia watanzania mbalimbali 


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...