Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bw. Ephraim Kwesigabo akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya Mfumuko wa Bei kwa mwezi Desemba 2018 leo jijini Dodoma.

Na: Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dodoma

Wastani wa Mfumuko wa Bei wa Taifa kutoka Januari hadi Desemba Mwaka 2018 umepungua hadi asilimia 3.5 kutoka wastani wa asilimia 5.3 kama ilivyokuwa mwaka 2017.

Hayo yamesemwa  jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bw. Ephraim Kwesigabo wakati akitoa taarifa kuhusu mfumuko wa bei wa mwezi Desemba 2018 pamoja na wastani wa mfumuko huo kwa mwaka mzima.

“Wastani huu wa mfumuko wa bei wa mwaka wa asilimia 3.5 ndiyo wastani mdogo kabisa kwa kipindi cha zaidi ya miaka 40 iliyopita ambapo tangu mwaka 1970 mfumuko huo ulikuwa 3.6,” ameongeza Kwesigabo. Aidha, akizungumzia kuhusu mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi Desemba ,2018, Kwesigabo amesema kuwa mfumuko huo umeongezeka hadi kufikia asilimia 3.3 kutoka asilimia 3.0 kwa mwezi Novemba 2018.

“Kuongezeka kwa Mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Desemba, 2018 kumechangiwa hasa na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Desemba, 2018 zikilinganishwa na bei za mwezi Desemba, 2017, mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Desemba, 2018 umeongezeka hadi asilimia 1.0 kutoka asilimia 0.4 ilivyokuwa mwezi Novemba, 2018,” amefafanua Kwesigabo.

Aidha amesema kuwa, baadhi ya bidhaa ya chakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei ni pamoja na nyama kwa asilimia 4.6, samaki wabichi asilimia 8.2, dagaa asilimia 26.2, matunda kwa asilimia 4.3 na mbogamboga asilimia 8.5 baadhi ya bidhaa zisizo za chakula zilizochangia mfumuko wa bei ni pamoja na vitambaa vya kushonea nguo kwa asilimia 2.1, nguo za kiume na za kike kwa asilimia 6.1, nguo za watoto kwa asilimia 3.0, sare za shule kwa asilimia 3.1, dizeli kwa asilimia 27.6, petroli asilimia 10.8 na huduma za malazi kwa asilimia 6.8.

Kwa upande wa nchi za Afrika Mashariki, mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia mwezi Desemba, 2018 nchini Kenya umeongezeka hadi kufika asilimia 5.71 kutoka asilimia 5.58 kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba, 2018 na mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia mwezi Desemba, 2018 nchini Uganda umepungua hadi kufika asilimia 2.2 kutoka asilimia 3.0 kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba, 2018.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...