Na Agnes Francis, Blogu ya jamii

WAKATI shirika lisilo la Kiserikali la FEMINA likitimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwake wameeleza kujivunia kwao kwa kufanikiwa kuwafikia vijana wengi zaidi katika kila Wilaya iliyopo Tanzania bara na baadhi ya shule za Visiwani Zanzibar na kutoa elimu ambayo imewasaidia na wengi wao kutoa mirejesho chanya kwa shirika hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi wa habari wa FEMINA Amabilisi Batamula amesema kuwa hadi sasa kuna klabu zaidi ya 2300 ambazo zimesajiliwa na zinapata majarida, pia kuna muunganiko wa klabu zaidi ya 2900 ambazo ni muunganiko wa klabu za Wilaya, Mikoa na Kanda pamoja na klabu za FEMA za walimu walezi wa klabu hizo zipatazo 38.

Batamula amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa shirika hilo wamekuwa wakijikita katika utoaji wa elimu kwa vijana kuhusiana na afya ya uzazi na ujinsia kwa kuwapa stadi za maisha na huwafundisha mbinu ya kusubiri hadi watakapotimiza malengo yao bila kujihusisha na masuala la ngono.

Amesema kuwa FEMINA huwasaidia vijana katika kujikwamua kiuchumi na hiyo ni kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kupata taarifa na wao huzichakata na kuwapa vijana kupitia majarida na kusema kuwa hutoa taarifa kwa vijana juu ya fursa zinazowazunguka na sio kuwapatia fedha wala mitaji.

Pia amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa shirika hilo wamekuwa wanawahimiza vijana kushiriki katika mikutano mbalimbali ya vijiji, kata na Wilaya pamoja na kujua haki na wajibu wao katika jamii na kujitolea katika masuala ya kijamii kama vile kufanya usafi katika hospitali, masoko na kujitolea damu pamoja na kupinga tamaduni potofu zikiwemo mimba za utotoni na ukeketaji.

"Wana klabu wa FEMA jijini Dodoma wamekuwa na utaratibu wa kujitolea damu katika hospitali mbalimbali na hata tatizo la damu likitokea wana klabu hutafutwa na kushiriki zoezi hilo ambalo huokoa maisha ya wengi." ameeleza Batamula.

Kuhusiana na njia wanazotumia kuwafikia vijana kote nchini ameeleza kuwa, FEMINA huwafikia vijana hao kupitia jarida la FEMA linalotoka mara nne kwa mwaka na kusambazwa katika shule zote za sekondari zilizosajiliwa kama wana klabu, pia amesema kuwa wanawafikia vijana hao kupitia vipindi vya redio na televisheni na vipindi vingi hufanyika vijijini ili kuwafikia vijana wengi zaidi.

Amabilisi amesema kuwa lazima wazazi pamoja na walezi wawe wawazi kwa vijana ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha kuhusiana na afya ya uzazi pamoja na kukabiliana na changamoto katika ukuaji wao.

Kuhusiana na mchango wa FEMINA katika klabu za FEMA kote nchini Afisa ufuatiliaji na tathimini kutoka FEMINA Martha Samwel amesema kuwa ufaulu kwa shule zenye klabu za FEMA uameongezeka na hiyo ni kutokana na mirejesho wanayoipata kutoka kwa walimu na walezi wa klabu hizo kwani kupitia klabu hizo wanafunzi wamekuwa wakielimishana na kuhimizana kuhusu masomo na katika baadhi ya maeneo wanafunzi watoro darasani wamerudi shule kutokana na nguvu ya klabu za FEMA.

"Kuna baadhi ya shule zimekuwa na misimamo yao ambapo wanakauli mbiu zao za kutoruhusu mwanaklabu ya FEMA afeli darasani, hii inawapa nguvu na ari ya wao kusoma zaidi na hatimaye kufanya vizuri katika masomo yao" ameeleza Martha.Aidha amesema kuwa mafanikio waliyoyapata kwa miaka 20 ni makubwa sana hasa kwa kuwafikia vijana wengi Tanzania kote na kutoe elimu ambayo imewasaidia kwa kiasi kikubwa hivyo wanajivunia kuwa sehemu ya maisha kwa vijana hao.

Pia amewashauri vijana wengine kujiunga na klabu za FEMA ili waweze kupata elimu ya afya na ujinsia pamoja na elimu ya ujasiriamali ambayo itawasaidia katika kujenga taifa na kujenga nchi ya viwanda kwa kuwa wao ndio nguvu kazi ya taifa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...