Na WAMJW,Morogoro

Wananchi wa Mkoa wa Morogoro na halmashauri zake wametakiwa kutowaficha wagonjwa wenye ukoma majumbani ili ugonjwa huo uweze kutokomezwa hadi ifikapo mwaka 2020.

Hayo yamesemwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bw. Clifford Tandari wakati wa ufunguzi wa semina ya uhamasishaji wa uongozi wa mkoa wa Morogoro na Wilaya ya mvomero kuhusu maadhimisho ya miaka sitini (60) ya Ushirikiano kati ya serikali na Shirika la German Leprosy and Tb Relief nchini Tanzania(GLRA) pamoja na siku ya ukoma Duniani itakayofanyika Kitaifa wilayani Mvomero mwishoni mwa mwezi huu.

“Serikali inawajali sana wananchi wake hivyo wananchi hampaswi kuwaficha wagonjwa majumbani kwani dawa na vipimo zinatolewa bila malipo kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini” Alisema Tandari
Aidha, alisema kuwa mkoa wake utaendelea kufanya kila liwezekanalo ili kutokomeza ugonjwa wa ukoma mkoani hapa kwani wajibu wao ni kuwasaidia watu hao kupona na kurudi kwenye kazi zao za kila siku watu wagonjwa hao wakishapatiwa dawa wanapona kabisa.

Kwa upande wa ongezeko la wagonjwa wilayani Mvomero Katibu Tawala huyo alisema sababu kubwa ya kuongezeka kwa wagonjwa hao wilayani hapo ni muingiliano hususan kwenye mashamba hivyo inakua rahisi maambukizi kuwa juu”tutafanya jitihada ili kuweza kufikia viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO) ili kutokomeza ugonjwa huu ambapo malengo ni mgonjwa mmoja kati ya watu elfu kumi.

Naye Mratibu wa Taifa wa ugonjwa wa Ukoma kutoka Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Deus Kamara alisema kuwa zipo halmashauri 20 ambazo hazijafikia kiwango cha kutokomeza ukoma nchini hivyo wizara kupitia mpango wa Taifa wa kutokomeza Kifua kikuu na Ukoma, Mikoa inatakiwa kutengeneza mkakati wa kuwasaka,kuwafikia, kuwaibua na kuwaweka katika matibabu stahili pamoja na kuzifikia kaya zote zenye wagonjwa wa ukoma kwa kufanyiwa uchunguzi ili wale ambao hawajaugua kuwapatia tiba kinga ili kutokomeza ukoma katika halmashauri zote ifikapo mwaka 2020.

Wakati huo huo Mwakilishii Mkazi wa Shirika la GLRA Buchard Rwamtoga alisema kuwa shirika hilo mwaka huu linatimiza miaka sitini(60) hapa nchini katika kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutokomeza ugonjwa wa ukoma Tanzania ikiwemo ya kuwajengea makazi bora familia 120 kutoka familia 739 ya watu waliougua ukoma hapa nchini.

“Dhamira yetu ni kuhakikisha kwamba kupitia michango ya wadau mbalimbali,shirika linaweza kusaidia mashirika na taasisi nyingine hasa mpango wa taifa wa kudhitibi ugonjwa wa kifua kikuu na Ukoma kupunguza madhara yatokanayo na magonjwa haya”alisisitiza Rwamtoga.

Alitaja mafanikio waliyoyapata kwa miaka 60 Mwakilishi Mkazi huyo alisema shirika lake wameweza kutoa viatu maalum kwa walioathirika na ukoma pea 94,500 kwa watu 47, 250, miguu bandia magongo na baiskeli kwa watu 2, 655, magari 270 kwa Tanzania bara na Zanzibar,kusaidia masuala ya elimu kwa wanafunzi 3,765 pamoja na kuwezesha vikundi vya kusaidiana vipatavyo 50 vyenye wanachama 677 kwa familia za watu wenye kuishi na ugonjwa wa Ukoma nchini.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya ukoma mwaka huu ni “Tutokomeze ubaguzi ,Unyanyapaa na chuki dhidi ya waathirika wa Ukoma” na kitaifa yatafanyika kwenye kitongoji cha Chazi kijiji cha kigugu Wilayani Mvomero tarhe 27 mwezi huu.
 Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bw.Clifford Tandari akifungua semina ya Uhamasishaji kwa viongozi wa mkoa wa Morogoro na Wilaya ya Mvomero katika kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya ushirikiano kati ya serikali  na shirika la German Leprosy and Tb Relief nchini Tanzania (GLRA).Semina hiyo imefanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
 Baadhi ya wakuu wa idara kutoka mkoa na wilaya wakimsikiliza Katibu Tawala wa Mkoa(hayupo pichani)ambapo wametakiwa kuhamasisha utekelezaji wa kuwaibua wagonjwa wa ukoma kutoka kila kaya ili kufanikisha malengo ya kutokomeza ugonjwa wa Ukoma ifikapo mwaka 2020
 Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bw.Clifford Tandari akifungua semina ya Uhamasishaji kwa viongozi wa mkoa wa Morogoro na Wilaya ya Mvomero katika kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya ushirikiano kati ya serikali  na shirika la German Leprosy and Tb Relief nchini Tanzania (GLRA).Semina hiyo imefanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro.Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mohamed Utay na kushoto ni Mganga Wa Mkoa wa Morogoro Dkt.Frank Jacob
Picha ya pamoja ya viongozi wa mkoa,wilaya,Wizara ya afya na GLRA mara baada ya ufunguzi

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...