Timu ya Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Mloganzila (Mloganzila Sports Club) imeichapa mabao 6-0 timu ya Albino United ya Kibamba, mchezo uliyofanyika leo katika kituo cha michezo cha Jakaya Kikwete Youth Park Kidongo chekundu jijini Dar es salaam.

Katika mchezo huo bao la kwanza lilifungwa dakika ya 18 kipindi cha kwanza na mchezaji machachari Jamal Msuya kutoka timu ya Mloganzila.
Wafungaji wa mabao mengine kutoka timu hiyo ya Mloganzila Sports Club ni Ashirafu Katenda, Edger Mtitu na Adam Kingwande wakati magoli mawili yalifungwa na Goodluck Manji.

Katika mechi hiyo wachezaji wa Mloganzila walionekana kumiliki mchezo na kuhakikisha timu yao inaibuka na ushindi mnono.Hadi dakika tisini timu ya Albino United haikuweza kutikisa nyavu za wapinzani wao ambao ni Mloganzila Sports Club.

Awali kabla ya kuanza kwa mechi hiyo Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Tawi la Mloganzila Dkt. Mohamed Juma Mohamed amewapongeza wachezaji wote kwa kushiriki mchezo huo wa kirafiki ambao unadumisha umoja na kulinda afya.

Dkt. Mohamed amewaeleza wachezaji hao kwamba uongozi wa hospitali utaendelea kushirikiana nao bega kwa bega ili kuhakikisha michezo inaendelea kudumishwa.

Vilevile Hospitali ya Mloganzila imewapatia timu ya Albino United msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo mafuta maalum ya kupaka kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) pamoja na vifaa vya huduma ya kwanza.

Naye Mwenyekiti wa timu ya Albino United Mohamed Kidunyo ameushukuru uongozi wa hospitali kwa kukubali kushiriki mchezo wa kirafiki sambamba na kuwapatia msaada wa vifaa hivyo ambavyo ni muhimu katika kulinda ngozi zao hasa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino).


Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Mloganzila, Dkt. Mohamed Juma Mohamed akiwasalimia wachezaji kabla ya kuanza kwa mchezo wa kirafiki kati ya timu ya Muhimbili-Mloganzila na timu ya Albino United ya Kibamba jijini Dar es Salaam
Mchezaji wa timu ya Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Mloganzila, Jamal Msuya akiifungia timu yake bao la kwanza katika mchezo uliochezwa katika Kituo cha Michezo cha Jakaya Kikwete Youth Park , Kidondo chekundu jijini Dar es Salaam.
Mchezaji wa Muhimbili tawi la Mloganzila akipiga kichwa katika mchezo muda mfupi baada ya timu yake kufunga bao la kuongoza katika kipindi cha kwanza
Mmoja wa wachezaji wa timu ya Albino United akikokota mpira baada ya kuwatoka wachezaji wa timu ya Muhimbili tawi la Mloganzila.
Kapteni wa Timu ya Albino United, Suleiman Mussa akiwapatia maelekezo wachezaji wa timu yake wakati wa kipindi mapumziko.
Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Mloganzila, Dkt. Mohamed Juma Mohamed akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji hao
Dkt. Mohamed Juma Mohamed akiwapatia wachezaji wa timu ya Albino United msaada wa mafuta maalum ya kupaka kwa watu wenye ulemavu wa ngozi pamoja vifaa vya huduma ya kwanza. Picha na John Stephen, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...