*Shule ambazo hazifuati waraka wa elimu nazo kuchukuliwa hatua
*Azungumzia ada kubwa kwa shule binafsi, aapa kutafuta suluhu
*Wanafunzi wanaojiunga kidato cha kwanza wapewa siku 90...

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

SERIKALI imetangaza kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria kwa shule zote binafsi ambazo hazifuati waraka wa elimu nchini huku ikitangaza kufanya msako kubaini wote wanaokiuka waraka huo. Pia Serikali imetoa onyo kwa shule zote binafsi ambazo zina tabia ya kupandisha ada kiholela, kukaririsha madarasa wanafunzi kinyume na waraka uliopo pamoja na michango mikubwa inayotoza bila kufuata utaratibu.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mwita Waitara amesema, hiki ni kipindi cha elimu na kuna mambo lazima yawekwe sawa kwa wazazi, walezi, wadau wa elimu na shule kufahamu nini ambacho kinatakiwa kufuatwa. hayo ameyafafanua juzi alipokuwa kwenye kipindi katika kituo cha televisheni cha Taifa (TBC) ambapo alitoa namba yake ya simu ambayo ni 0767221344 na kusema kuwa kupitia namba hiyo amepokea meseji nyingi za wazazi ambazo nyingi ni za malalamiko na hasa kwa shule binafsi ambazo zimekuwa zikifanya unyanyasaji wa hali ya juu kwa wanafunzi, wazazi au walezi.

Waitara ameeleza kuwa TAMISEMI ndio inayosimamia elimu ya msingi na sekondari na ametumia nafasi hiyo kuzungumzia umuhimu wa ushirikiano kwa pande zote akiwa na maana upande wa wazazi na shule husika katika kupanga na kukubaliana mambo mbalimbali yakiwamo ya ada. Pia amesema wakati wanashughulikia changamoto zilizopo, Serikali imetoa siku 90 kwa kila mtoto anayetakiwa kuanza kidato cha kwanza kuripoti ndani ya muda huo na iwapo hatafanya hivyo hatua zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria, na amewatoa hofu wazazi kuwa watoto wote ambao wanatakiwa kuanza kidato cha kwanza ndani ya muda huo wa siku tisini watakuwa shuleni na kuchelewa kuanza masomo hakutakuwa sababu ya kumfanya mwanafunzi kufanya vibaya kwenye masomo yake.

VIPI KUHUSU ADA?

Waitara amesema moja ya malalamiko ambayo ameyapokea ni ada kupandishwa kiholela kwa baadhi ya shule binafsi jambo ambalo amesema ni marufuku shule kupandisha ada kiholela bila kumshirikisha mzazi. "Tunafahamu hakuna muongozo rasmi wa ada kwa shule binafsi , hivyo ipo haja ya kuuibua upya mjadala huu ili tuwe na ada ambayo itakuwa inaeleweka. Kuna shule binafsi ambazo zipo zinazotoza ada kuanzia Sh.milioni 1.5 hadi Sh.milioni sita na hapa ndipo yanapoanza maswali unapoona mwanafunzi anayelipiwa ada hizo anaomba mkopo akiwa Chuo Kikuu.Tunajua huenda kukawa na sababu nyingi lakini nachotaka kusema lazima hili la ada tulizungumze upya na kupata muafaka. Ada ni kubwa sana."amesema Waitara.

Hata hivyo amesema ada ambayo inalipwa ni makubaliano kati ya mzazi na shule lakini ni jambo la ajabu mzazi anapoambiwa ada imepanda bila kushirikishwa, hivyo ameagiza shule zote ambazo zimepandisha ada kiholela ni marufuku kumlipisha mzazi na hivyo ada ambayo anatakiwa kulipa ni ile ambayo walikubaliana na si hiyo iliyopandishwa bila utaratibu wa kushirikisha wazazi au walezi husika.

Amewataka wote wenye malalamiko kuhusu ada kupandishwa kiholela waende kwa maofisa elimu wa wilaya au kwa mkurugenzi ili hatua zichukuliwe kwa shule husika ili kukomesha tabia hiyo."Ni marufuku kumrudisha mwanafunzi nyumbani kwa sababu ya ada, aachwe asome, kama mzazi amelipa ada ya mtoto kwa miaka mitatu au minne kwanini ufukuze mwanafunzi kwa mzazi wake kushindwa kuleta ada. Mwanafunzi aachwe asome wakati mnajadiliana namna ya kulipana hiyo ada."amesisitiza Waitara.

AWEKA WAZI KUHUSU WASTANI
Pamoja na mambo mengine Waitara amezungumzia wastani wa alama za ufaulu kwa wanafunzi wa shule za msingi na shule za sekondari ambapo amefafanua tayari Serikali ilishatoa muongozo na huo ndio unatakiwa kufuatwa kwa shule zote nchini na si vinginevyo.

"Serikali ndio yenye kupima uwezo wa wanafunzi na hivyo kama kuna sababu za mtoto kubakia kwenye darasa kwasababu yoyote ile lazima kuwe na makubaliano ya kimaandishi ambayo ndiyo yatatumika kama kilelezo cha kwanini mwanafunzi amekakariri dasara.

"Kuna shule binafsi ambazo zimeweka wastani wake na wamekuwa wakiutumia huo kuwafanya wanafunzi wasiendelee na darasa linalofuata. Hilo ni kosa kwasababu mwenye kutoa muongozo wa kupima ufaulu ni Serikali tu, hakuna mtu au shule yoyote ambayo inaweza kwenda tofauti.Tutafuatilia shule zote na iwapo tubabaini wamekiuka utaratibu tutachukua hatua za kisheria na ikiwezekana tutafuta usajili wa shule husika." amesema Waitara.

Amesema kuna taarifa anazo kuna baadhi ya shule ambazo zimewarudisha wanafunzi kwasababu ya wastani ambao wameweka kwenye shule zao, hivyo ametoa maagizo wanafunzi hao waachwe waendelee na masomo na warudishwe shuleni kwa kuwa upimaji wa ufaulu kwa elimu ya msingi unafanyika darasa la nne na kwa sekondari inafanyika kidato cha pili, wanafunzi ambao wamefaulu waachwe wasome na hili agizo ni kwa shule zote zikiwemo hizo na binafsi.

Amesema anazo meseji kwenye simu yake ambazo zinazungumzia wanafunzi kurudishwa kwasababu ya kushindwa kufikia alama zilizowekwa."Shule ambazo zinashindwa kufuata muongozo baadhi tunazo na nimetoa maagizo zifuatiliwe ili tuchukue hatua,"amesema Waitara huku akitaja baadhi ya shule(majina tunayo) ambayo amedai yanakiuka utaratibu uliopo.

AONYA SHULE ZINAZOBADILISHA WANAFUNZI DINI
Wakati huohuo Waitara ametoa onyo kwa shule ambazo zimekuwa na tabia ya kubadilisha imani za watoto kwa kigezo cha kuwa sifa ya kujiunga na shule hizo ambapo amesema ni marufuku kama shule inamilikiwa na Wakistro basi Waislamu waachwe wasome na hivyo hivyo kama inamilikiwa na Waislamu, basi Wakristo wasome.

""Hatutaki kusikia mtoto amebadili imani yake ya dini au dhehebu lake kwasababu ya masharti ya shule. Serikali ndio inayotoa muongozo kuhusu elimu nchini, hivyo ni marufuku, wanafunzi waachwe wasome bila kusumbuliwa,"amefafanua Waitara.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...