Waheshimiwa Madiwani na Wataalamu kutoka katika Manispaa ya Sumbawanga wakiwa kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Mji Njombe mara baada ya kuwasili kwa lengo la kujifunza maswala ya usafi wa mazingira na ukusanyaji mapato. (Aliyesimama) ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Illuminata Mwenda
 Mweka Hazina wa Halmashauri ya Mji Njombe Bi. Dorcas Mkello akiwasilisha mada ya ukusanyaji mapato kwa Wahe. Madiwani na Wataalamu kutoka Manispaa ya Sumbawanga

 Afisa Mazingira Halmashauri ya Mji Njombe Lawi Bernard, akitoa mpango mkakati wa Halmashauri ya Mji Njombe wa utunzaji na uthibiti wa taka ngumu kwa Waheshimiwa Madiwani na Wataalamu kutoka katika Manispaa ya Sumbawanga wakati wa ziara ya mafunzo ya timu hiyo katika Halmashauri ya Mji Njombe. 
 Afisa TEHAMA kutoka Halmashauri ya Mji Njombe Isack Mapunda akitoa ufafanuzi wa matumizi bora ya mashine za ukusanyaji mapato (POS) kwa Waheshimiwa Madiwani na Wataalamu kutoka katika Manispaa ya Sumbawanga wakati wa ziara ya mafunzo ya timu hiyo katika Halmashauri ya Mji Njombe.
Mradi wa ujenzi wa kituo kipya cha mabasi unaofadhiliwa na benki ya dunia kupitia mradi wa uboreshaji na uimarishaji Miji (ULGSP) katika Halmashauri ya Mji Njombe  ni miongoni mwa mradi uliotembelewa na  Waheshimiwa Madiwani na Wataalamu kutoka Manispaa ya Sumbawanga.




=========  ============   ================  ============

MARA BAADA YA KUZIBURUZA HALMASHAURI ZA MIJI KWENYE MASHINDANO YA USAFI, HALMASHAURI YA MJI NJOMBE YAIPIGA MSASA MANISPAA YA SUMBAWANGA.

Hyasinta Kissima-Njombe

Halmashauri ya Mji Njombe imepokea ugeni wa Waheshimiwa Madiwani wakiambatana na Wataalamu kutoka katika Manispaa ya Sumbawanga lengo ikiwa ni kujifunza na kuongeza maarifa kuhusiana na maswala ya mapato na usafi wa Mazingira.

Haya yamebainika wakati wa hafla fupi ya kuwakaribisha wageni hao iliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Njombe, ambapo ugeni huo ulikiri wazi kuwa wamevutiwa kufika Halmashauri ya Mji Njombe kujifunza kutokana na sifa ambazo Halmashauri imekuwa ikijizolea kila mara katika eneo la usafi wa Mazingira pamoja na ukusanyaji mapato.

“Halmashauri ya Mji Sumbawanga kwa mwaka wa fedha 2017/2018 tulikasimia kukusanya bilioni mbili na milioni mia tano, lakini hatukufanikiwa kukusanya asilimia 80 kwa mujibu wa maagizo ya Mhe. Waziri Mkuu tulikusanya asilimia 54 pekee. Kwa upande wa mashindano ya usafi na Mazingira tulishika nafasi ya pili kutoka mwisho kutokana na ukosefu wa vyoo bora na matumizi bora ya vyoo.”Alisema Mstahiki Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Mhe. Justin Emmanuel Malisawa.

Alifafanua kuwa changamoto kubwa ambayo imekuwa ikiwakabili ni kwenye utekelezaji wa sheria ndogo ndogo za Halmashauri na changamoto kutoka kwa wanasiasa ambao wamekuwa wakipinga na kutotekeleza ipasavyo baadhi ya maazimio waliyojiwekea kwenye ukusanyaji wa mapato na utunzaji Mazingira na ndio maana waliona umuhimu wa kuja kujifunza kutoka Njombe.

Akielezea mafanikio ya Halmashauri ya Mji Njombe ambayo imefikia kwa upande wa usafi wa Mazingira sambamba na ukusanyaji mapato, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe, Bi Illuminata Mwenda amesema kuwa mafanikio hayo yalitokana na utayari na kujitoa kwa Madiwani bila kujali itikadi za vyama vyao na ushirikiano wa Wataalamu.

“Madiwani ndio wanaotaka Halmashauri yao iweje, hivyo ndivyo ninavyofahamu. Mnaweza mkawa na mipango mizuri lakini Waheshimiwa Madiwani wakisema hapana inakuwa ndivyo. Madiwani wetu agenda zao kuu ni mapato na usafi. Na hata katika vikao vya wataalamu tumekuwa tukijadili na kuboresha mapungufu yanayojitokeza na kuweka mikakati thabiti kwenye ukusanyaji mapato na usafi wa Mazingira na tumekuwa tukifanikiwa kwa kiasi kikubwa.”Alisema Mwenda.

Dorcas Mkello ni Mweka Hazina wa Halmashauri ya Mji Njombe ambaye yeye amesema kuwa miongoni mwa mbinu ambazo wamekuwa wakizitumia kwenye ukusanyaji mapato ni sambamba na utoaji wa motisha ya pikipiki kwa watendaji wanaofanya vizuri kwenye ukusanyaji mapato na kutoa milioni 5 kwa kila Diwani kwa kila robo ya mwaka fedha ambazo hukabidhiwa kwa diwani wa Kata husika kwa ajili ya kuchochea maendeleo kwenye Kata yake. Hivyo kupitia fedha hizo, kila diwani amekuwa mlinzi kwenye usimamizi wa mapato kwani wasipofanya hivyo wanaelewa fika fedha hizo hazitapatikana bila kukusanywa kwa nguvu kubwa.

Afisa Mazingira Halmashauri ya Mji Njombe Lawi Bernard amesema kuwa licha ya kuwa na mwamko chanya wa wananchi kwenye uchangiaji wa tozo za taka, Halmashauri kupitia mapato ya ndani imekua ikiona umuhimu wa kuiwezesha idara hiyo na ndio maana kwa mwaka wa fedha 2018/2019 walifanikiwa kutenga fedha kupitia mapato ya ndani na kununua tractor kwa ajili ya kubeba taka na hivyo kuzuia mlundikano wa taka katika maeneo ya Mji kutokana na uwepo wa vitendea kazi vya kutosha.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe Edwin Mwanzinga alisema kuwa, siri ya mafanikio ni umoja baina ya Waheshimiwa Madiwani na wataalamu kwani wamekuwa wakipokea maelekezo ya wataalamu na panapokuwa na mapungufu wamekuwa wakishirikiana kuboresha kwa manufaa ya Halmashauri nzima.

“Wenzangu wa Sumbawanga niwaombe muwe na ushirikiano katika ukusanyaji mapato. Maendeleo ni ya wananchi wote na hayana vyama, naomba pia mfahamu kuwa katika swala la Usafi na Mazingira hamtaweza kufanya vizuri kwa kutegemea Halmashauri itaondoa taka yenyewe, lazima mzalisha taka awe na jukumu la kuondoa taka kwa kuchangia gharama.”Alisema Mwanzinga.

Aidha, Waheshimiwa Madiwani na Wataalamu kutoka Manispaa ya Sumbawanga wameishukuru Halmashauri ya Mji Njombe kwa elimu waliyoipata na wamepongeza ujenzi wa kiwango cha hali ya juu unaoendelea katika kituo kipya cha Mabasi na wameahidi kutengeneza mtandao wa mawasiliano na Halmashauri ya Mji Njombe ili kuendelea kupata ujuzi na mbinu mpya katika maeneo mbalimbali.

Ikumbukwe kuwa Halmashauri ya Mji Njombe kwa miaka miwili mfululizo; 2017/2018 na 2018/2019 imepokea wageni kutoka Halmashauri nane za Mikoa ya Songwe, Singida, Shinyanga na Rukwa kwaajili ya kujifunza mbinu na siri ya ushindi inayotumia Halmashauri ya Mji Njombe katika kuimarisha hali ya usafi katika maeneo yake yote.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...