Asubuhi ya Jumatatu, tarehe 8 Desemba 1930 huko Lupaso, kijiji cha Bulongwa, Njombe, alizaliwa mtoto wa kiume mwenye afya tele. Mtoto huyo, ambaye alikuja kuweka historia ya kipekee nchini, si mwingine bali ni TUNTEMEKE MESAKA NNUN'GWA SANGA. Wazazi wake, Bw. na Bi SANGA, walikuwa ni watoto wa Chifu. Watoto wengine wa wazazi hao walikuwa ni RWIJISO, ANNA, GEOFREY na ALFRED (Mwenyekiti wa Simba SC 1979-1982).

TUNTE alianza shule ya msingi mwaka 1942 huko Njombe akiwa na miaka 12 kama ilivyokuwa kwa Mwalimu JK NYERERE.

TUNTE alifanya mtihani wa darasa la 4 na kufaulu na hivyo akaendelea "middle school" hadi 1946 alipofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi  huko na kufaulu.  

TUNTE alijiunga na shule ya sekondari ya Ilboru mwaka 1947 na kumaliza mwaka 1950 ambapo alifaulu vizuri sana. Kidato  cha tano na sita alisoma shule ya "Tabora Boys" kuanzia mwaka 1951 hadi 1952.

Baada ya hapo akasomea ualimu(kazi  iliyokuwa na heshima sana enzi hizo kwani hata Mwalimu NYERERE alikuwa mwalimu pia). TUNTE, baada ya kupata cheti cha ualimu, akaenda kufundisha shule ya sekondari ya Ilboru.

TUNTE, akiwa kijana mdogo wa miaka 26, alikuwa mmoja wa Watanganyika wa kwanza kwenda kusoma Marekani kwani alipata fursa hiyo mwaka 1956.

TUNTE alikuwa kijana  mwenye IQ ya kipekee na malengo yasiyo ya kawaida ambapo alidhamiria kusoma fani mbalimbali kwa kadri itakavyowezekana.

Dhamira hiyo ilimfikisha katika vyuo mbalimbali nchini humo vya Gustav Adolphus, Chicago, Columbia na Princeton.

Dhamira hiyohiyo ya aina yake ndiyo iliyomuwezesha kuwa Mtanganyika wa kwanza na pekee kupata shahada 7 za fani za  Biashara, Uhusiano wa Kimataifa, Utawala, Sheria, Kilimo, Sayansi ya Jamii na Dini. Kuhusu dini alikujakusema mwenyewe bungeni tarehe 24.8.1993 - "Nikiwa Marekani nilijifunza na nayajua sana masuala ya dini kwa upande wa Wakristo, Waislamu na Bhuda".
TUNTE pia alikuwa akifundisha na kutoa mihadhara kwenye vyuo mbalimbali nchini humo na alikuwa na uwezo mkubwa wa lugha akiongea kwa ufasaha Kiingereza, Kiswahili, Kijerumani na Kifaransa. Mwaka 1962, alianza masomo ya PHD huko "Yale University". PHD hiyo ilihusu maendeleo ya utendaji vijijini. Kozi hiyo ilimpasa kwenda pia chuo cha Nuffield, UK na Chuo  Kikuu cha Dsm. 

TUNTE alirejea nchini mwanzoni mwa mwaka 1964 akawa Afisa Uhusiano wa kampuni ya Riddoch Motors (1964-1965). Aidha, kwa mikono yake, akajenga nyumba kijijini Bulongwa.

TUNTE, tarehe 20.9.1964, alifunga ndoa na Bi. BETTY ANN FITZGERALD, mmarekani mweusi aliyezaliwa Marekani mwaka 1939. Ndoa hiyo ya kukata na shoka ilifungwa huko Bulongwa baada ya TUNTE kulipa mahari iliyojumuisha ng'ombe, kondoo, mbuzi na kuku. Kwa hakika ilikuwa harusi ya aina yake ambapo watoto 122 waliovalia nadhifu waliwarushia maua maharusi hao, waliokuwa wamevaa nguo maridadi za kiafrika zilizotengenezwa nchini Ghana, na kuwaimbia nyimbo kedekede za Kikinga na Kizungu. Wazee kwa vijana, kwa wiki nzima, walisheherekea ndoa hiyo huku wakila beche lililopikwa kwenye mapipa 15 na pombe ya ulezi iliyokuwa "ya kumwaga". Ilikuwa ni harusi ya kihistoria ambayo, hadi leo, haina mfano wake Bulongwa! Aidha, harusi hiyo iliweka rekodi ya kuwa harusi ya kwanza Tanzania kuandikwa, kwa mapana na marefu, kwenye gazeti maarufu la Marekani (The New York Times la tarehe 1.11.1964 chini ya kichwa cha habari: "Pittsburgh Girl's Wedding in African village")!.

TUNTE alimuona kwa mara ya kwanza Bi. Betty alipoenda kutoa mhadhara huko Pittsburgh, Marekani mwaka 1960 ambako ndio kwao Bi. Betty, msomi mwenye shahada ya uzamili. Baada ya uchumba wa miaka 4, wawili hao ndipo walipooana.

TUNTE akaanza kufanya shughuli mbalimbali za biashara, kilimo, sheria na pia akajiingiza kwenye siasa ambayo ilikuja kumletea matatizo makubwa na Mwalimu NYERERE.

TUNTE, kwa kusoma Marekani kwa muda mrefu, aliamini kwamba siasa ya Ujamaa ni feki na haiwezi kuleta maendeleo na hakuwa akificha msimamo huo licha ya kuwa mwana-TANU iliyokuwa ikiamini katika Ujamaa.

TUNTE alieleza kwamba yeye ndio anafaa kuwa Rais hivyo Mwalimu NYERERE ampishe ili ailetee nchi maendeleo kwa falsafa za ubepari na abadili "mentality" ya wananchi wa Tanzania ambao wengi ni wavivu wapendao kujirusha na kuoneana wivu. TUNTE alidai shahada zake 7 zilimfanya awe na fikra sahihi za kuleta maendeleo kuliko Mwalimu aliyekuwa na shahada mbili tu na muumini wa ujamaa aliouona "unailostisha" nchi!.

Hiyo ilimkera mno  Mwalimu ambaye, kwa kutumia "The Preventive Detention Act, 1962", alimsweka mara moja TUNTE kizuizini kijijiji kwake Bulongwa na kumuamuru kutotoka kijijini hapo hadi apate kibali maalumu. 

TUNTE alikuwa kizuizini Bulongwa kwa miaka mingi na hii ilipelekea ashindwe kumaliza kozi yake ya PHD ambapo miaka ya baadae alipenda kutania:  
"Mimi ni PHD Candidate. Nilirudi nchini ili nifanye utafiti kuhusu PHD yangu lakini nikawekwa  kizuizini kwa miaka mingi hivyo nikashindwa kuikamilisha ndio maana najiita "DR. MTAHINIWA"!.

Mwalimu NYERERE, baada ya miaka mingi, alimsamehe TUNTE  ambaye aligombea ubunge jimbo la Makete mwaka 1980 na kushinda kwa kishindo.

TUNTE, akiwa bungeni, alikuwa mtata sana huku akiwapeleka puta mawaziri na hata maspika.!  

Siku moja bunge lilipokuwa pale Karimjee Hall, Dar Es Salaam, Mh. TUNTE alitinga na suruali ya "jeans" na shati la kitenge. Maofisa wa bunge hawakumruhusu kuingia ndani kwani hilo halikuwa vazi rasmi la bunge. Mh TUNTE akaondoka lakini akarudi na shati zuri lilishonwa kiwanda cha Nguo Urafiki lakini akiwa amevaa kaptura! Walinzi, kwa mara nyingine, wakamzuia lakini hakukubali hivyo ukazuka mtafaruku wa "kufa mtu"!. Mh Spika, ADAM SAPI MKWAWA alipoingilia kati, Mh TUNTE alimjia juu na kutaka amuoneshe Kifungu cha kanuni alichovunja. Hatimaye ilibidi arudi nyumbani!.   

Mh. TUNTE kuna wakati alipewa dakika 15 tu na Mh Spika PIUS MSEKWA aongee lakini akazisisha na kutumia dakika  30. Mh. MSEKWA alipomtaka akae, Mh TUNTE, aliyemzidi Mh. MSEKWA miaka 5 kiumri, alihamaki na kusema- " "Hivi kwenu hakuna Wakubwa? Huoni mambo niyaongeleyao ni muhimu kwa wananchi wetu?"  . Ukumbi mzima wa bunge  ulizizima kwa vicheko na hata Mh MSEKWA mwenyewe aliangua kicheko na hatimaye Mh TUNTE akakaa!. Kwa hakika,  Mh TUNTE hakuwa mtu wa Mchezo-mchezo!.

Mh TUNTE alikuwa mtu wa msimamo mkali asiyeyumbishwa wala kuogopa kusema alichokiamini na aliheshimiwa sana na Wabunge wenzake na aliposimama bungeni hata waliokuwa nje walikuwa wakirudi ndani kumsikiliza kwani alipenda sana kujenga hoja baada ya kufanya tafakuri tunduizu !.

Wananchi wa Makete walimpenda sana na alishinda ubunge mara zote alizogombea. Aliweza kuongea Lugha za Kikinga, Kibena,  Kihehe na Kinyakyusa kwa ufasaha.

Mwaka 1995 alikuwa mmoja wa wana-CCM waliochukua fomu kugombea Urais. Hii ni kwavile alitaka kutimiza azma yake ya kuliongoza Taifa hili kama alivyomwambia Mwalimu NYERERE ambae aliamua kumuweka kizuizini. Wengine waliochukua fomu walikuwa J. Warioba,  N. Kasaka, M. Bomani, J. Malecela, C. Msuya, H. Kolimba, R. Lugendo, J. Kikwete, E. Lowasa, R. Fred, K. Malima na B. Mkapa aliyechaguliwa kuipeperusha bendera ya chama na hatimaye kuwa Rais wa awamu ya tatu. 

Mh TUNTE alianza kupata matatizo ya macho muda mfupi kabla ya kuanza kikao cha bunge mwaka 1996 Dodoma na akapelekwa hospitali ya Muhimbili ambako alilazwa. Mwezi Julai 1996, alipelekwa London, UK kwani aliishapoteza uwezo wa kuona kwa 95% ambako alifanyiwa operesheni  ya macho.

Wizara ya Afya ikamrudisha nchini kwa kudai ilikuwa imemaliza fungu ililotenga kwaajili ya matibabu yake hivyo akalazwa wodi ya Mwaisela mwezi Septemba 1996 baada ya kurejea nchini mwezi Agosti 1996. Alikuwa hawezi kumtambua mtu kwa kumuona bali kwa sauti tu. Viongozi wa serikali, Mh Dr. OMARI na Mh F. SUMAYE walimtembelea wodini hapo kumjulia hali. 

Mwanzoni mwa mwezi Octoba 1996, Mh TUNTE akatolewa hospitalini. Katikati ya Juni 1997, alikimbizwa hospitali ya Aga Khani ambako alilazwa ICU kwa wiki 2. Mh TUNTE akafariki saa 7 usiku wa Jumatano, tarehe 2.7.1997 akiwa na umri wa miaka 66.

Aliyekuwa Naibu Spika, Mh PHILLIP MARMO alilitangazia bunge kesho yake asubuhi kuhusu msiba huo  mkubwa na kwamba marehemu alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya figo na moyo. Simanzi kubwa ikashamiri bungeni.

Jijini Dar es Salaam, shughuli za mazishi ziliendeshwa na Brigedia Jenerali PETER LIGATE na msiba ulikuwa mtaa wa Mansfield kwa mdogo wake TUNTE, ALFRED SANGA.

Mwili  wake uliagwa Muhimbili jumamosi ya tarehe 5.7.1997 ambapo Rais MKAPA aliongoza mamia ya wananchi kutoa heshima zao za mwisho ambapo alisema:

"Kifo cha Mh. SANGA kimetuondolea kiongozi mashuhuri ambaye ametoa mchango mkubwa wa maendeleo si tu Makete bali nchi nzima kwani alikuwa Mzalendo mwenye uchungu mkubwa na nchi  yake. Hakuwa mwoga bali alikuwa mkweli daima. Nafasi aliyoiacha itakuwa ngumu sana kujazwa na kwamba mchango wake katika taifa hili utaandikwa katika historia ya nchi yetu".

Mwili wake ulisafirishwa kwa ndege na akazikwa kijijini Bulongwa Jumapili tarehe 6.7.1997. Wakati huo alikuwa ameachana na mkewe Bi Betty. Msiba huo ulihudhuriwa na watu wengi huku Wabunge 4 waliwakilisha wenzao.  Wabunge hao walikuwa T. NYIMBO, J. MAKWETA, M. KIBASSA na J. NHUNGA aliyekuwa Katibu wa Wabunge wa CCM.

Huyo ndiye  TUNTEMEKE MESAKA NNUN'GWA SANGA aliyeacha historia ya kipekee nchini!.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...