Wahitimu wa taaluma ya Ustawi wa Jamii kutoka Chuo cha Ustawi wa Jamii Kisangara kilichoko wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro wametakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na miiko ya taaluma yao ili kujitofautisha na watumishi wengine kutokana na elimu waliyoipata.

Rai hiyo imetolewa na Kamishina wa Ustawi wa Jamii Kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii) Dkt. Naftali B. Ng’ondi wakati wa Mahafali ya Kwanza ya Chuo cha Ustawi wa Jamii Kisangara kwa wahitimu kwa mwaka wa masomo 2017/2018.

Dkt. Ng’ondi amesema kuwa wataalam mbalimbali wamekuwa wakivamia kazi za Ustawi wa Jamii kwa kudhani kuwa ni kazi holela kuweza kufanywa na mtu yeyote na  kuwakumbusha wahitimu kuwa kazi za ustawi wa jamii ni muhimu na inapaswa kufanywa na wataalam wenye weledi wanatoa huduma kwa kuzingatia maadili na miiko ya kazi.

 Amekipongeza Chuo cha Ustawi wa Jamii Kisangara kwa kuonesha mafanikio chanya kwani kmwaka wa masomo 2016/2017 wakati chuo kinaanza kulikuwa na wanafunzi 56 tu. Lakini kwa mwaka wa masomo 2018/2019 chuo kimedahili wanafunzi 158 ambapo  wanafunzi wa kike ni 115 na wa kiume ni 43 ikiwa ni ongezeko la asilimia 100 katika udahili ukilinganisha na mwaka 2016/17.

Kamishna Ngondi amepongeza jitihada uongozi wa Chuo kwa kufanikisha usajili wa kudumu Chuo na mtaala kutolea mafunzo na huduma bora inayotolewa na Chuo katika kusimamia mafunzo na kuongeza nyenzo mbalimbali za kutolea mafunzo kama kompyuta na projector jambo ambalo limekuwa chachu ya ongezeko la udahili wa wanafunzi.

“Wizara inatambua changamoto zilizopo za uchakavu na miundombinu ya madarasa na mabweni hiyo tutaendelea kuimarisha na kukarabati majengo ya chuo ili kuwa na mazingira bora zaidi ya kusomea na kujifunzia”.alisema Dkt. Ng’ondi.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Kisangara Anna Mwingira amewapongeza wazazi  na walezi kwa kuthamini utoaji wa fursa sawa kwa wasichana na Mtoto wa kike na kuwezesha udahili wa wanafunzi wa kike kufikia asilimia 73 ukilinganisha na asilimi 43 ya wavulana, ongezeko ambalo ni takribani ni mara mbili zaidi ya wavulana.

“Hii ni dalili njema kuwa jamii inaendelea kuelewa azma ya Serikali ya kuwawezesha wanawake ili kuwapa mbinu na stadi za kuweza kutoa mchango katika kufikia uchumi wa kati na wa viwanda’’ aliongeza.

Aidha Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa jamii Kisangara Anna Mwingira alieleza kuwa awali kuanzia mwaka 1986 hadi mwaka 2012 chuo kilikuwa kinatoa mafunzo kwa ngazi ya cheti katika fani ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya mtoto (ECD, Non NTA level). Kuanzia Julai 2012 mafunzo katika fani ya ustawi wa jamii pia yalianza kutolewa katika ngazi ya cheti kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, American International Health Alliance (AIHA) na Taasisi ya Ustawi wa Jamii Kijitonyama (Institute of Social Work D’SALAAM – ISW).

 Mwingira ameleza kuwa Chuo kina usajili wa kudumu kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) uliopatikana mnamo tarehe 29/3/2017 na Na.  REG/BTP/009 kwa kozi ya Ustawi wa Jamii ngazi ya Astashahada hadi ngazi ya Diploma na kwa sasa Chuo kinatoa mafunzo katika fani ya ustawi wa Jamii ngazi ya Cheti na Diploma (NTA Level 4, 5 and 6) na fani ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (ECD) ambayo inasimiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Chuo kinaendesha amsomo kwa kutumia mtaala wake wa fani ya ustawi wa jamii, ambao ulikamilika mwaka 2016/2017.

Naye mmoja wa wahitimu Immaculate Kinama na Elizaberth Kawishe kwa wakati tofauti walibainisha kuwa wamejengewa weledi kwani wanayo maarifa, mbinu na stadi za kuwawezesha kufanya majukumu yao kwa umahiri katika kusaidia wahitaji kama vile watu wenye ulemavu, wazee, watoto na makundi yote yenye uhitaji maalum katika jamii.

Taaluma ya ustawi wa jamii msingi wake ni haki na ustawi katika jamii ili kuhakikisha kwamba hakuna mtu anayeachwa nyuma na kubaguliwa ama kutengwa katika huduma mbalimbali za maendeleo ya jamii husika. Pia, taaluma hii ni muhimu katika kuwasaidia watu walio katika makundi tete mfano wanaonyanyaswa, wanaonyanyapaliwa na maskini sana ili waweze kufaidika na rasilimali au huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu, afya, shughuli za kiuchumi, burudani na shughuli mbalimbali katika jamii na kupata habari kwa mfano kwa watu wasiosikia.

Haya ni Mahafali ya kwanza ya Chuo cha Ustawi wa Jamii kisangara baada ya kupita miaka 33 bila kusanyiko la mahafali. Wahitimu 158 wametunukiwa vyeti katika ngazi ya Astashahada wakiwa na wajibu wa  kuwezesha huduma za ustawi wa jamii katika ngazi ya kata, mashule ya awali, msingi sekondari, na maeneo mengine kama vile Ofisi za Polisi, Mahakama, Magereza na katika jamii kwa ujumla.
 Kamishna wa Ustawi wa Jamii kutoa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto (Idara kuu Maendeleo ya Jamii) Dkt. Naftali B. Ng’ondi akimtunuku cheti kwa mmoja wa wanafunzi wahitimu wa Astashahada ya Ustawi wa Jamii Esher Reubeni katika Mahafali ya kwanza ya Chuo cha Ustawi wa Jamii Kisangara Kilimajaro.
 Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali B. Ng’ondi akiwahutubia wahitimu na halaiki ya watu waliohudhuria kusanyiko la mahafali ya kwanza ya Chuo cha Ustawi wa Jamii Kisangara mkoani Kilimanjaro.
 Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Kisangara kilichoko Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro Anna Mwingira akieleza mafanikio ya Chuo  hicho katika Mahafali ya kwanza ya Chuo cha Ustawi wa Jamii Kisangara Kilimajaro.
 Baadhi ya  ndugu na jamaa wa wahitimu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Kisangara wakifuatilia hotuba ya Mgeni rasmi katika Mahafali ya Chuo cha hichoa ambaye ni Kamishina wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali B. Ng’ondi katika Mahafali ya kwanza ya Chuo cha Ustawi wa Jamii Kisangara Kilimanjaro.
 Kamishna wa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara kuu Maendeleo ya Jamii) Dkt. Naftali B. Ngondi akiwa kwenye picha ya pamoja na uongozi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Kisangara wakati wa Mahafali ya kwanza ya Chuo hicho. Picha na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...