Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na watumishi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi alipowatembelea ofisini kwao jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga akieleza majukumu ya taasisi yake kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi wa TASAF kilichofanyika Makao Makuu ya TASAF jijini Dar es Salaam chenye lengo la kuhumiza uwajibikaji.
Baadhi ya watumishi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) alipowatembelea ofisini kwao jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb), akiwa katika picha ya pamoja na menejimenti ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mara baada ya kuzungumza na watumishi wa mfuko huo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.

…………………………

Watumishi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wametakiwa kuhakikisha wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wanahudumiwa vizuri kwa kupata ruzuku zao kwa wakati ili kuziwezesha kaya hizo kujikimu kimaisha na kuondokana na umaskini.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati akizungumza na watumishi wa TASAF makao makuu katika ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kufahamu kwa kina majukumu ya TASAF na kujiridhisha namna inavyotekeleza wajibu wake.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema, kwa kuwahudumia vizuri wanufaika hao, TASAF pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itapata baraka za Mwenyezi Mungu ambaye kupitia vitabu vyake vitakatifu ameelekeza kuwasaidia maskini na pia watakuwa mfano bora wa kuigwa na nchini nyingine barani Afrika kwa kutekeleza vema Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amewataka watumishi wa TASAF kuwa tayari muda wote katika kuhakikisha kaya zote maskini zinapata stahili zao kwa wakati na kufurahia matunda na jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kuziwezesha kaya maskini kuondokana na umaskini.

Aidha, Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameitaka TASAF kuhakikisha inaweka taratibu madhubuti za kisheria zitakazowaadhibu na kuwadhibiti wote watakaobainika kufanya udanganyifu kujipatia fedha za mpango wakati hawana sifa za kuwa wanufaika, lengo likiwa ni kujenga nidhamu katika jamii ili fedha za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ziwafikie walengwa kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli anavyotaka.

Katika kutekeleza azma hiyo, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amewataka watumishi wa TASAF kufanya kazi kwa ari na uzalendo mkubwa na kuipongeza TASAF kwa jitihada na mafanikio waliyoyapata katika kuzinusuru kaya maskini mpaka hivi sasa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga amemhakikishia Mhe. Dkt. Mwanjelwa kuwa, atahakikisha anasimamia vizuri utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini kama alivyoelekeza, ili uwe ni mpango bora zaidi katika bara la Afrika, na kuongeza kuwa, hadi sasa, tayari mpango umeonekana kuwa ni miongoni mwa mipango bora barani Afrika kwani umeweza kuboresha maisha ya kaya maskini ambapo utekelezaji wake umewezesha kuzitambua kaya maskini, umesimamiwa vizuri, malipo yanafanyika kwa wakati na hakuna ubadhilifu mkubwa wa fedha zilizotengwa kwa ajili ya wanufaika.

Akithibitisha ubora wa mpango, Bw. Mwamanga amesema, hivi sasa Rais wa Benki ya Dunia katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku, anapozungumzia programu za kupambana na umaskini, haachi kuutaja Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa nchini Tanzania kuwa ni bora na unasimamiwa vizuri.

Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. John P. Magufuli aliyejipambanua kwa vitendo kuwajali wanyonge, imedhamiria kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini kuwafikia walengwa katika kaya zote maskini nchini ili walengwa hao waweze kunufaika na kuboresha maisha yao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...