Waziri wa Madini Doto Biteko (katikati) akieleza jambo wakati wa kikao cha Menejimenti ya Wizara na Taasisi zake. Kulia ni Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara, Prof. Simon Msanjila.
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akizungumza jambo wakati wa kikao hicho.
Baadhi ya Watendaji wa Wizara na Taasisi wakifuatilia kikao hicho
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof. Idris Kikula akizungumza jambo katika kikao hicho.

…………………… 

Waziri Biteko aanza kazi  Awataka watumishi kufanyia kazi maagizo ya Rais Magufuli Amshukuru Waziri Kairuki kuwa, amemfundisha Mengi
Aitaka STAMICO kuanza kutoa gawio kwa Serikali

Waziri wa Madini Doto Biteko amekutana na Menejimenti ya Wizara ya Madini, Taasisi zake pamoja na Wenyeviti wa Tume ya Madini na Bodi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), jijini Dodoma, katika kikao ambacho pia kimejadili namna ya kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli aliyoyatoa wakati akimwapisha Waziri Biteko kushika wadhifa huo Januari 9, 2019.

Biteko amewataka watumishi wa Wizara na Taasisi zake ambao hawayajayasikiliza maagizo yaliyotolewa na Rais Magufuli kuhakikisha kuwa wanayasikiliza ili kuweka uelewa wa pamoja na kushirikiana katika kutekeleza majukumu ya wizara kwa lengo la kuhakikisha kwamba sekta ya madini inaimarika.

“ Tuliulizwa dhahabu inauzwa wapi? Basi tusisubiri tena Rais atuulize inauzwa wapi,” amesisitiza Biteko. Aidha, amesisitiza kuwepo kwa ushirikiano wa pamoja miongoni mwa watumishi wa wizara katika utekelezaji wa majukumu hayo na kusisitiza kuhusu mabadiliko yanayoonekana kupitia sekta ya madini ikiwemo kufanya kazi na kuongeza kuwa, “ Kinachotuunganisha mahali hapa ni kazi na wala si dini ama jambo lingine,”.

Ameongeza kuwa, kiu kubwa ya Rais Magufuli ni kuona kuwa watanzania wote wananufaika na rasilimali madini huku akisisitiza kuwa, kiu yake binafsi ni kuona taswira nzuri inajengeka kuhusu sekta hiyo ikiwemo kufanya kazi kwa weledi na kuongeza kuwa, matokeo bado hayaonekani.

“Vipaji mlivyonavyo mvitumie vizuri vitoe matokeo yanayoonekana. Fanyeni kazi ambazo zitaacha matokeo yatakayo dumu. Natamani ningezungumza na watumishi wote ili kila mmoja aelewe kile ninachosema,” amesisistiza Biteko.

Vilevile, amewataka watendaji kuchukua hatua badala ya kutumia muda mrefu kutafuta miongozo wakati wanapotekeleza majukumu jambo ambalo linachelewesha utekelezaji wa majukumu. “ Unasubiri mwongozo gani ilhali unayo Sheria ya Madini?amehoji Waziri Biteko. Pia, amechukua fursa hiyo kumshukuru aliyekuwa Waziri wa Madini Angellah Kairuki na kueleza kuwa, ni kiongozi ambaye amemfundisha mambo mengi.

“ Namshukuru sana dada yangu, rafiki yangu Angellah. Alinipokea vizuri sana. Hakuna ushirikiano nilioukosa kwake. Amenifundisha mengi ikiwemo kukaa kwenye kikao na kujadili mambo kwa kina,” amesema Biteko. Pamoja na hayo, Biteko ametumia fursa hiyo kumshukuru Naibu Waziri Nyongo kwa kuwa naye pamoja katika kipindi chote ambacho alikuwa Naibu Waziri katika wizara ya madini.

Katika hatua nyingine, Waziri Biteko ameitaka STAMICO kuhakikisha kuwa, inaanza kutoa gawio kwa Serikali na ikiwezana, jambo hilo lifanyike kabla ya mwaka ujao wa fedha. Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, awali akizungumza katika kikao hicho, amewataka watumishi ambao hawakupata fursa ya kusikia maagizo ya Rais Magufuli kufanya hivyo ili kila mmoja asimame kwa lengo moja.

“ Hatukusemwa vizuri. Nchi nzima imesikia na dunia imesikia. Tukiendelea hivi, hatutavumiliwa,” amesisitiza Nyongo. Pia, ameitaka Tume ya Madini kuhakikisha inazingatia na kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Rais Magufuli ikiwemo kutekeleza wajibu wao.

Awali, akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila amesema kwamba, kikao hicho ni cha kwanza na Waziri Mpya ikiwemo Mjumbe wa Bodi ya STAMICO na kuongeza kuwa, kinalenga kutoa utambulisho rasmi wa Waziri Mpya wa Madini na kusikia maelekezo ya Waziri Biteko kufuatia maagizo yaliyotolewa na Waziri.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO, Meja Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo amemweleza Waziri Biteko kuwa, anayapokea majukumu yote yaliyo mbele yake ya kuhakikisha kwamba shirika hilo linatekeleza majukumu yaliyo mbele yake.

Kikao hicho kimefanyika tarehe 11 Januari, 2019

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...