WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Kangi Lugola
 
 
*Aagiza wachunguzwe, atoa maagizo mazito kwa Katibu Mkuu Mambo ya Ndani

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Kangi Lugola amewasimamisha kazi vigogo watano wanaohusika na wakimbizi katika kambi ya Mtendele na Nduta mkoani Kigoma, baada ya kubainika uwepo wa sare za Jeshi zikiwa kwenye marobota ya nguo za misaada.

Akizungumza leo Januari 13,2019 , Waziri Lugola amesema kumebainika uwepo wa sare hizo kwenye marobota hayo ya nguo za misaada ambazo yalikuwa yanapelekwa katika kambi ya Wakimbizi Mtendeli na Kambi ya wakimbizi ya Nduta mkoani Kigoma.

Amefafanua katika kambi ya Mtendeli kumebainika kuwepo kwa sare za jeshi 1325 na katika kambi ya Nduta kumebainika uwepo wa sare 622 na hivyo kufanya jumla ya idadi ya sare zote kuwa 1947.

"Kwa Serikali hii inayoongozwa na Rais Dk.John Magufuli haiko tayari kuona tukio hilo linaachwa bila kuchukua hatua.Kama nguo hizo zimeweza kubainika maana yake kesho au kesho kutwa zinaweza kuingizwa silaha.Tulitarajia wahusika walitakiwa kubaini nguo hizo mapema kabla ya kuingia kwenye makambi hayo.

" Lazima tuhakikishe nchi yetu iko salama kwa kuhakikisha hakuna ambacho kinaingia nchini kwetu.Hivyo nimeamua kuchukua hatua za kuwasimamisha kazi baadhi ya watumishi wa kambi hizo za wakimbizi,"amesema Waziri Lugola wakati anazungumzia sare hizo.

Amewataja aliosimamishwa kazi ni Mkurugenzi wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi Harson Mseke, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma kwa Wakimbizi upande wa Menejimenti ya Makambi na Makazi, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi anayeshughulikia Usalama na Operesheni.

Wengine ni Mkuu wa Kambi ya Wakimbizi Mtendeli John Mwita pamoja na Mkuu wa Kambi ya Wakimbizi Nduta Peter Bulugu .Pia amesema Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani anatakiwa kumchukulia hatua Mratibu wa Wakimbizi Mkoa wa Kigoma Tony Laiza.

Akizungumzia zaidi tukio hilo la kubainika kwa sare hizo ,Lugola amesema tayari amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ndani ya siku mbili kuanzia kesho kuunda tume kuchunguza sare hizo na kisha baada ya siku 10 awe amempa taarifa ya uchunguzi na uwe umekamilika.

"Nimemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani kuunda timu maalum kuchunguza suala hili na ndani ya siku 10 awe amekamilisha ripoti na kunikabidhi,"amesema Lugola huku akifafanua uwepo wa sare hizo nchi ya Burundi inaweza kuwa na mawazo hasi kwa kudhani huenda Tanzania inawasaidia Wakimbizi kuunda jeshi jambo ambalo si kweli.

Waziri Lugola amefafanua kuwa siku za karibuni kulikuwa na mchakato wa kuwarudisha wakimbizi waliokubali kwa hiyari yao kurudi nchini Burundi na hivyo kubainika kwa sare hizo huweza kutafsiriwa kwamba walikuwa wanataka kuwapa sare hizo kwenda kufanya uasi.

" Lazima tuchukue hatua katika hili,nasubiri ripoti ya uchunguzi itakavyoeleza,"amesisitiza Waziri Lugola huku akiwataka WaTanzania kutoa taarifa zozote ambazo zitasaidia kuifanya nchi yetu kuwa salama .

Na kwamba hata kama kuna misaada inayotolewa na mashirika ya kimataifa kwa ajili ya Wakimbizi walioko nchini isiwe sababu ya kutumika kuingiza sare za jeshi au silaha.

Kamati ya ulinzi na usalama Mkoa wa Kigoma ikiteketeza jumla ya nguo 1947 zinazofanana na sare za jeshi zilizokamatwa kwenye kambi za wakimbizi za Mtendeli na Nduta Wilayani Kibondo hivi karibuni. Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Samson Anga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali mstaafu Emanuel Maganga alisema kuwa nguo hizo zinazofanana na sare za jeshi ziliingizwa kambini na Mkurugenzi wa shirika Danish refugees council kwa ajili ya kugawa kwa wakimbizi katika kambi ya Nduta na Mtendeli Wilayani Kibondo.

Kamati ya ulinzi na usalama Mkoa wa Kigoma ikishusha shehena ya nguo zipatazo 1947 zinazofanana na sare za jeshi zilizokamatwa kwenye kambi za wakimbizi za Mtendeli na Nduta Wilayani Kibondo,kwa ajili ya kuchomwa moto. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...