Na Karama Kenyunko globu ya Jamii. 

Mkurugenzi wa UDART, Robert Kisena (46) na wenzake watatu akiwemo raia wa China,  wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashitaka 19 yakiwemo ya utakatishaji na  kusababishia UDART hasara ya zaidi ya BIL. 2.41.

Mbali ya Kisena, washitakiwa wengine ambao wote wamesomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba ni Kulwa Kisena (33), Charles Newe (47) na Cheni Shi (32). Raia wa China. 

Katika mashtaka hayo, lipo shtaka moja La kuongoza uhalifu, shtaka moja la kujenga kituo cha mafuta bila kibali,  shtaka moja la kuuza mafuta sehemu zisizoruhusiwa na shtaka la wizi wakiwa Wakurugenzi, 

Pia wanakabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha, mashtaka manne ya kughushi, mashtaka manne ya kutoa nyaraka za uongo, mashtaka mawili ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na shtaka moja la kuisababishia mamlaka hasara. Washitakiwa hao wamesomewa mashitaka yao na Wakili wa Serikali, George Barasa, Moza Kasubi na Imani Mitumezizi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Katika kosa la kuisababishia UDART hasara, linalowakabili washitakiwa wote inadaiwa kati ya Mei 25, 2015 na Desemba 31, 2016 Washtakiwa  hao kwa mamlaka waliyonayo waliisababishia UDART hasara ya Bil 2.41.

Pia Robert Kisena na Shi, wanadaiwa Mei 26, 2016 wakiwa NMB Bank Ilala kwa pamoja wakiwa Wakurugenzi wa Longway Engineering huku Kisena akiwa Mkurugenzi wa UDART walihamisha Sh. Mil.603 kutoka akaunti ya benki ya UDART kwenda kwenye akaunti ya Longway ambapo ndani ya siku mbili walizitoa fedha hizo huku wakijuwa kuwa fedha ni zao la  kosa la kughushi.
Katika shtaka la kujipatia nyaraka kwa njia ya udanganyifu, imedaiwa,  Robert Kisena na Shi,  Mei 30, 2016  katika Benki ya NMB Ilala walijipatia nyaraka kwa njia ya udanganyifu kutoka katika benki hiyo ikiwa na jina la Fund Transfer Request Form ya Aprili 6, 2016 kwa lengo la kuonyesha kiasi cha Sh.Mil 750 zimelipwa na Kampuni ya Longway kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa Kituo cha Mwendokasi Kimara, Kivukoni, Ubungo na Morocco huku wakijua kuwa siyo kweli.

Katika kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, linamkabili  Robert Kisena na Shi wanadaiwa June 8, 2016 katika benki ya NMB Ilala washtakiwa kwa njia ya uongo walijipatia Mil.594.92 kutoka UDART kwa kuonyesha zimelipwa na kampuni ya Longway ambayo imehusika katika kutengeza vitu mbalimbali.

Pia katika kosa la kughushi,  Kisena anadaiwa April 6, 2016 katika benki ya NMB Ilala alighushi nyaraka yenye tarehe April 6, 2016 kwa lengo la kuonyesha Mil.594 zimelipwa kwa kampuni ya Longway ambayo imejihusisha na uandaaji, utengenezaji wa vitu mbalimbali huku wakijua kuwa siyo kweli. 
Katika kosa jingine la utakatishaji fedha linawakibili washitakiwa wote wanadaiwa kati ya Mei 25, 2015 na December 31, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa wakiwa na lengo hovu walibadilisha thamani ya mafuta ya zaidi ya Bil.1.21 kuwa fedha ambayo ni Bil 1.21 baada ya kuyauza mafuta hayo, huku wakijua mafuta hayo ni zao la kosa la wizi.

Robert Kisena na Kulwa Kisena wanadaiwa kati ya Januari 1, 2015 na December 31, 2017 huko Katika maeneo ya Jangwani Ilala, wakiwa Wakurugenzi wa Kampuni ya Zenon Oil and Gas Ltd 
walijenga kituo cha Mafuta bila ya kupata kibali kutoka EWURA. 

Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote mahakamani hapo kwa kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za Uhujumu uchumi.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na imeahirishwa hadi Februari 23, 2019 washitakiwa wamerudishwa rumande.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...