Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu kifungo cha maisha watuhumiwa nane (8) kati ya 18 waliokuwa wanakabiliwa na tuhuma za kuchoma moto kituo cha polisi Bunju A jijini Dar es Salaam.

Na Karama Kenyunko globu ya Jamii. 

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu kifungo cha maisha jela washitakiwa 8 kati ya 18 akiwemo Mwanafunzi baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuchoma moto Kituo cha Polisi cha Bunju A. Kufuatia adhabu hiyo, vilio vilitawala Mahakamani hapo huku ndugu wa wafungwa hao wakianguka na kuzimia. 

Katika Kesi hiyo,  jumla ya washitakiwa 35 walifikishwa mahakamani ambapo Mahakama ilikwishawaachia huru washitakiwa 17 na kubaki 18 ambapo 8 ndio wametiwa hatiani leo Februari 22 huku 10 wakiachiwa huru.

Washitakiwa waliohukumiwa Leo ni pamoja na Mwenyekiti wa Serikali kitongoji Bunju A,  Yusuph Salehe Sungu  (40), Juma Kozo (32), Rashid Liwima (29), Baraka Nkoko (23), Abuu Issa (36), Abraham Mninga (23), Veronica Ephraem (32) na Ramadhan Said (22).

Aidha washtakiwa kumi walioachiwa leo ni Mrisho Majaliwa (30), Hamis Ndege (37), Seleman Gwae (33), Menge'nya Anthony (28), Rehema Hussein (32) Rajabu Ally (25), Ally Athuman (24), Amina Matipwili (33), Gubila Temba (51) na Mariam Honza (44).
Washitakiwa kwa pamoja walikuwa wanakabiliwa na makosa sita likiwemo la kufanya mkusanyiko usio halali huku kosa la pili hadi la tano yakiwa ni kufanya uharibifu wa mali na kosa la sita ni kuchoma moto kituo cha  Polisi cha Bunju A makosa ambayo  wanadaiwa kuyatenda Julai 10, 2015.

Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi 17 wa upande wa mashtaka waliofika mahakamani hapo kutoa ushahidi wao. ambao unaweza Kuwatia hatiani washitakiwa katika shitaka la kuchoma moto kituo cha Polisi. 

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Simba Amesema, ni ukweli usiopingika kuwa kituo hicho kilichomwa,  hakukuwa na tatizo la umeme na kwamba sababu ni watu kukusanyika kutokana na kifo cha mtoto aliyegongwa na gari.

Mwenyekiti alichochea wananchi waliozingira kuchoma moto kwa kituo hicho kwa kutumia mafuta ya petroli," Amesema. 
Pia amesema ni ukweli kwamba kila kitu kilichokuwepo kwenye kituo hicho kiliteketea kwa moto na kubaki majivu na wakati magari yalipigwa mawe.

Alisema kifungu cha 319 A cha Kanuni ya Adhabu, kinaeleza kwamba washitakiwa wanaotiwa hatiani kwa makosa hayo adhabu ni mpaka kifungo cha maisha na kwamba mahakama yenyewe itaamua ni aina gani ya adhabu ya kuwapa washitakiwa.

Amesema mahakama hiyo ilienda eneo la tukio ilishuhudia kituo kilivyoteketea kwa moto, ikiwa ni pamoja na bunduki,  vifaa vyote vya kituoni hapo na pia kituoni hapo kulikuwa na mahabusu.


"Kitendo walichofanya washitakiwa cha kuchoma moto kituo cha polisi ni cha kinyama na kamwe hawezi kuwaonea Huruma. "Nawahukumu kifungo cha maisha jela" Amesema Hakimu Simba na kuinuka.

Awali katika utetezi wao, idadi kubwa ya washitakiwa waliomba kupewa adhabu ya kifungo cha nje ama kupigwa faini.
Kabla ya kusomwa kwa Hukumu hiyo,  Hakimu Simba aliuliza Kama walikuwa na lolote la kusema dhidi ya washtakiwa ambapo wakili wa serikali, Ester Martin aliomba  mahakama kuwapa washitakiwa adhabu kali ili iwe fundisho kwao na kwa wengine wanafikiria kuja kutenda kosa Kama hilo. 

Amesema kosa walilofanya washtakiwa hao ni kosa kubwa na ambalo linahatarisha usalama wa nchi,  linastahili kulaaniwa na yeyote yule kwani ni tukio linaloweza kuhatarisha amani na taharuki katikati ya raia ambao hawana kosa. 

Baada ya maelezo hayo Hakimu Simba akasema, kituo kilichomwa mapema kabisa majira ya saa tano Saa sita,  ndani kulikuwa na mahabusu, kitendo walichofanya ni kitendo cha kinyama na wala hakistahili Huruma,  sio kitu ambacho tunaweza kuvumilia, hivyo Mahakama  inawahukumu kifungo cha maisha gerezani .

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...