NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ ameeleza kwamba ustawi wa elimu nchini umetokana na matunda ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12 mwaka 1964.

Hayo ameyasema katika hafla ya kuwapatia zawadi Wanafunzi wa kidato cha nne mwaka 2018 waliofaulu kiwango daraja la I,II kwa shule mbali mbali za Zanzibar, hafla iliyofanyika katika kiwanja cha Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Unguja.

Dk.Mabodi amesema baada ya kufanyika Mapinduzi ya Zanzibar serikali ya wakati huo ikatangaza kuwa suala la elimu ni bure sambamba na kuimarisha miundombinu ya upatikanaji wa elimu kwa wananchi wote bila ubaguzi.

Amesema Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuenzi Tunu ya Mapinduzi kutokana na mambo mema yaliyotekelezwa kwa haraka mara baada ya kufanyika mapinduzi hayo na wananchi wakapata uhuru na kunufaika na fursa ya elimu iliyotolewa kwa ubaguzi kabla ya mapinduzi.

Ameeleza kuwa kwa sasa Zanzibar imekuwa ni kitovu cha wasomi na watu wenye taaluma mbali mbali ambao chanzo cha mafanikio hayo kimetokana na kukua kwa sekta ya elimu nchini.

Katika maelezo yake Dk.Mabodi amewapongeza wanafunzi mbali mbali waliofaulu vizuri masomo yao ya kidatu cha nne pamoja na kuwasihi waliofeli kuwa wasikate tamaa bali wajiendeleze kupitia sekta ya mafunzo ya amali ili wawe na ujuzi.

Amesema katika kuunga mkono suala la elimu CCM imeandaa mpango maalum wa kuwasaidia vijana mbali mbali waliofeli masomo yao katika ngazi tofauti za kielimu ili nao wapate ujuzi wa kujiajiri wenyewe.

Akizungumza Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe.Ayoub Mohamed Mahmoud amewataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili wafaulu vizuri kidato cha sita na kujiunga na vyuo vikuu.Amesema elimu ni jambo muhimu kwa maisha ya binadamu hivyo ni lazima wajitume katika safari yao ya kutafuta taaluma.

Naye Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kaskazini Unguja, Bi.Angelina Adam Malembeka amewasisitiza wanafunzi hao kuwa bado wana safari ndefu ya kutafuta elimu hivyo waendelee kusoma kwa bidii ili wafikie malengo yao.

Jumla ya wanafunzi 1,222 waliofaulu mitihani ya kidato cha nne kwa kiwango cha daraja la kwanza na la pili(I,II) wamepatiwa zawadi mbali mbali na Chama Cha Mapinduzi ikiwa ni sehemu ya kuwapongeza na kuwahamasisha waendelee kusoma kwa bidii na kufaulu katika ngazi mbali mbali hadi Vyuo vikuu.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ akiwahutubia wanafunzi 1,222 waliofaulu kwa kiwango cha daraja la I,II katika mitihani ya Kitato cha Nne mwaka 2018.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’(kulia) akimkabidhi zawadi Mwanafunzi bora wa kiume Zanzibar ndugu Hassan Hamid Ussi aliyefaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza katika masomo ya Sayansi katika mitihani ya kidato cha Nne mwaka 2018.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’(kulia) akimkabidhi zawadi Mwanafunzi bora wa kike Zanzibar ndugu Faiza Shamim Khamis aliyefaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza katika masomo ya Sayansi katika mitihani ya kidato cha Nne mwaka 2018.
WANAFUNZI wa kidato cha Nne mwaka 2018 waliofaulu daraja la Kwanza na la Pili Zanzibar wakiwa katika hafla ya kukabidhiwa Zawadi na Chama Cha Mapinduzi Zanzibar(PICHA NA IS-HAKA OMAR).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...