Trekta aina ya URSUS likiendelea na kazi yakulima mashamba ya wakulima katika Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro.
Kazi ya uunganishaji matrekta katika Kiwanda cha Kuunganisha Trekta kilichopo Kibaha mkoani Pwani ikiendelea ikiwa ni juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kufufua na kukuza sekta ya Kilimo hapa nchini ambapo matrekta zaidi ya 200 yameunganishwa na kuuzwa kwa wakulima mbalimbali nchini.
Moja ya Trekta aina ya URSUS likiwa limekamilika. 
Matrekta yaliyounganishwa yakiwa tayari kuuzwa.

Sehemu ya majembe ya matrekta ya URSUS yakiwa tayari yameunganishwa Kiwandani Kibaha mkoani Pwani.
Trekta aina ya URSUS likiendelea na kazi yakulima mashamba ya wakulima katika Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro.
 
Mkulima kutoka Wilaya ya Gairo, Haji Salum akifanyia majaribio ya kuendesha trekta aina ya URSUS mara baada yakukabidhiwa trekta hilo alilonunua kutoka Kiwanda cha kuunganisha matrekta kilichopo Kibaha mkoani Pwani. (Picha na MAELEZO)

Na: Lilian Lundo - MAELEZO

Kiwanda cha Kuunganisha Trekta Aina ya URSUS kilichopo Mkoani Pwani kimekuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima wadogo kutokana na masharti nafuu ya ukopeshaji wa trekta hizo.

Kutokana na urahisi wa upatikanaji wa trekta hizo umepelekea kuongezeka kwa idadi ya wakulima wenye trekta ambazo zimekuwa zikiwalimia wakulima wadogo wadogo kwa gharama nafuu.

Akizungumia Trekta hizo, Mkulima wa zao la Mahindi na Alizeti kutoka Gairo, mkoani Morogoro, Haji Salum ambaye alikutwa kiwandani hapo akichukua trekta aliyoinunua kwa mkopo, ameeleza kuwa anafuraha kubwa ya kumiliki chombo hicho ambacho atakitumia kulimia mashamba yake pamoja na wakulima wenzake.

"Ninayofuraha kubwa kupata chombo hiki ambacho sikutarajia kukimiliki katika maisha yangu. Ninamshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kauli mbiu yake ya ujenzi wa viwanda ambayo imetuwezesha hata sisi maskini kumiliki trekta," amesema Salum.

Mkulima huyo anayemiliki heka 120 za mashamba ya mahindi na alizeti mkoani humo amesema, kwa kulima mashamba yake peke yake anauwezo wa kurejesha fedha ambazo zimebaki kukamilisha malipo ya trekta hiyo anayoimiliki.

Mkulima huyo amewashauri Watanzania kujitokeza kwa wingi kununua trekta hizo kwani masharti yake ni nafuu na zipo kwa ajili ya kila Mtanzania hata wale wenye kipato cha chini.

Aidha, mmiliki mwingine wa trekta hizo kutoka Wilaya ya Malinyi, Mkoa wa Morogoro Jacob Mbifile ameishukuru Serikali kwa kupata trekta kwa gharama nafuu ambayo anaitumia kulima mashamba yake pamoja na kuwalimia wakulima wenzake kwa kuchangia kiasi kidogo kwa ajili ya marejesho ya mkopo na uendeshaji wa chombo hicho.

"Kwa sasa tunalima kwa wakati, kutokana na uwepo wa trekta nyingi, tofauti na ilivyokuwa zamani, ambapo wakulima wengi walikuwa wakipata huduma ya kulimiwa kwa kuchelewa kutokana na uchache wa trekta uliokuwepo hivyo kusababisha kuvuna mazao machache kutokana na kuchelewa kupanda," ameeleza Mbifile.

Kwa upande wake, Mkulima wa zao la Mpunga Wilayani humo, Ladislaus Kidunda amesema kabla ya uwepo wa trekta hizo, kulikuwa na uhaba mkubwa wa trekta hivyo kusababisha foleni kubwa ya kusubiri trekta ili kulimiwa.

"Kipindi cha nyuma tulikuwa tukipata huduma ya kulimiwa kwa trekta kwa tabu sana kutokana na wamiliki wa trekta hizo kuwapa kipaumbele wale wenye mashamba makubwa kuanzia heka 10 na kuendelea. Tofauti na ilivyo sasa ambapo wamiliki wamekuwa wengi hata sisi wenye heka mbili au tatu tunaweza kupata huduma hiyo kwa wakati," amesema Kidunda.

Nae Msimamizi Mkuu wa Kiwanda hicho, Godwin Mubi amesema mpaka tarehe 15 Januari mwaka huu, jumla ya trekta 261 zimenunuliwa kwa njia ya mkopo katika mikoa ya Manyara, Mwanza, Dodoma, Ruvuma, Singida na Morogoro na mikoa mingine ikiwa kwenye mchakato wa kununua trekta hizo.

"Tunakopesha trekta hizi kwa kila Mtanzania anayehitaji, ambapo hutakiwa kutoa asilimia 25 ya gharama ya trekta na gharama inayobaki atairudisha kwa kipindi cha miaka miwili. Njia nyingine ni ile ambayo mkulima anaonesha dhamira ya kupata trekta, hivyo hulipia milioni 3 hadi 4 na kiasi kinachobaki hurejesha katika kipindi cha miaka miwili," amesema Mubi.

Aidha Mubi ameeleza, spea za trekta za Ursus zipo na zinapatikana kwa wingi nchini hivyo Watanzania watembelee kiwandani hapo kujua namna ya kumiliki trekta hizo kwani masharti na gharama yake ni nafuu.

Kiwanda cha Kuunganisha Trekta za Ursus ni kiwanda kinachosimamiwa na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ambapo huunganisha Trekta zinazokuja kwa vipande kutoka nchini Poland. Kiwanda hicho kilianza rasmi kufanya kazi Aprili, 2017 ambapo ni moja ya matunda ya kauli mbiu ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya ujenzi wa viwanda.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...