Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii. 

JUMLA  ya Mashahidi 54 na vielelezo 218 vinatarajiwa kuwasilishwa Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu uchumi, katika kesi ya Uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania  (TRA), Harry Kitillya na wenzake wanne kwa ajili ya kwenda kuanza kusikilizwa.

Mbali na Kitilya washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni  Maofisa wa benki ya Stanbic, Shose Sinare na Sioi Solomon, Kamishna wa Sera ya uchambuzi wa Madeni kutoka Wizara Fedha na Mipango, Bedason Shallanda na msaidizi wake Alfred Misana ambapo wote wanakabiliwa na mashtaka 58 yakiwemo ya utakatishaji fedha.

Hatua hiyo imekuja huku tayari Kitilya na wenzake wawili Shoe na Sioi wakiwa wamekaa gerezani kwa takribani miaka mitatu ambapo walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Aprili 16, 2016. Kesi hiyo imehamishiwa Katika mahakama ya mafisadi leo Februari 12, 2019 mara baada ya washtakiwa kusomewa upya mashtaka yao na kutajiwa Idadi ya mashahidi na vielelezo vitakavyowasilishwa wakati wa ushahidi. 

Baada ya kusomewa maelezo hayo,  Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi aliwauliza washtakiwa kama walikuwa na lolote la kuongeza ambapo wote walidai kuwa hawana cha kuongeza. Kufuatia hayo,  mahakama hiyo imetoa amri ya kuhamishia shauri hilo Mahakama Kuu Kitengo cha mafisadi.

Wakati watuhumiwa wakisomewa maelezo hayo ya mashahidi (Commital) upande wa mashtaka uliwasilishwa na jopo la mawakili watatu, walii wakiongozwa na Wakili Mkuu wa serikali,  Fredrick Manyanda,  wakili wa serikali Mkuu Tumaini Kweka na wakili wa serikali George Barasa.
Aidha upande wa utetezi uliwasilishwa na jopo la mawakili  watatu wakiongozwa na Cuthbert Tenga akisaidiana na Alex Mgongolwa pamoja na Majura Magafu. Miongoni mwa mashahidi wanaotarajiwa kuitwa ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, aliyekuwa mwanasheria Mkuu Wa Serikali, Fredrick Welema.

Katika kesi hiyo, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matatu ya kughushi, moja la kuongoza uhalifu,  49 utakatishaji fedha, mawili ya kutoa nyaraka za uongo, kujipatia fedha kwa njia ya udanyanyifu moja na shtaka moja la kutoa nyaraka kwa nia ya kumdanganya kwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango. 

Wanadaiwa  kati ya Machi 15, 2013 na Januari 10, 2014 ndani ya jiji la Dar es Salaam kwa nia ya kudanyanya washtakiwa wote walijipatia Dola za Kimarekani Milioni sita wakionesha kuwa fedha hizo zilikuwa ni malipo ya ada ya uwezeshaji wa upatikanaji wa mkopo na zililipwa kupitia Kampuni ya Egma T Ltd. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...