MAWAZIRI saba wametembelea Kijiji cha Kimotorok Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara kwa ajili ya kutatua mgogoro wa ardhi baina ya wananchi wa eneo hilo na hifadhi ya Taifa ya Tarangire na pori la akiba la Mkungunero. Pia mawaziri hao wamesikiliza mgogoro wa ardhi wa kijiji cha Irkushbor cha wilayani Kiteto na hifadhi ya Taifa ya Tarangire na pori la akiba la Mkungunero. 

Mwenyekiti wa mawaziri hao, William Lukuvi ambaye ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema wametumwa na Rais John Magufuli kusikiliza mgogoro huo. 

Waziri Lukuvi alisema baada ya kupokea mapendekezo ya namna ya kumaliza mgogoro huo kutoka pande zote watafikisha suala hilo kwa Rais Magufuli ili atoe maamuzi. 

Alisema wamepokea maoni kutoka kwa wananchi wa vijiji hivyo, viongozi wa serikali ngazi ya mkoa na wilaya, wabunge, hifadhi ya Taifa ya Tarangire na pori la akiba la Mkungunero. 

"Baada ya kupokea mapendekezo haya kwa njia ya maandishi na maoni ya mdomo tumeandika na tutayapeleka kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri na kisha aliyetutuma atayatolea maamuzi," alisema Lukuvi. 

Mawaziri saba waliofika Simanjiro ni Lukuvi, Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo, Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi, Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Sima. 

Akizungumza mbele ya Mawaziri hao saba, Mnyeti alisema amekagua nyaraka zote zilizopo kwenye mkoa huo lakini hajakuta sehemu inatamkwa kuwa pori la akiba la Mkungunero lipo Manyara. 

Mnyeti alisema baadhi ya wafugaji wa kijiji cha Kimotorok wilayani Simanjiro na Irkushbor wilayani Kiteto wanafukuzwa mara kwa mara na wakanyang'anywa mifugo yao zaidi ya 600. 

Mbunge wa jimbo la Simanjiro, James Ole Millya alisema wananchi hao wamenyanyasika vya kutosha kwani kila wakati wanafukuzwa na kuambiwa wapo hifadhini. 

Ole Millya alisema ni wakati sahihi wa kuweka mpaka ili ijulikane mwisho wa wafugaji hao na hifadhi ya Taifa ya Tarangire na pori la akiba la Mkungunero, kuliko mpaka wao kusogezwa kila wakati. 

"Kwa sababu mmekuja na helkopta mnaweza kupita juu na kuona mifugo yetu ng'ombe na mbuzi zinachungwa pamoja na wanyamapori wakiwemo tembo, pumbamilia, swala na nyumbu sisi wamasai ni wahifadhi wazuri," alisema Ole Millya. 

Diwani wa kata ya Loiborsiret Ezekiel Lesenga (Mardad) alimshukuru Rais John Magufuli kwa kuwajali na kuwatetea wafugaji na wakulima nchini. 

Mardad alisema hivi sasa wafugaji na wakulima wa eneo hilo wanalishia mifugo yao na kulima sehemu ambazo walikuwa wanazitumia miaka iliyopita kabla ya kuondolewa kwa kudaiwa wapo sehemu ya hifadhi ya Taifa ya Tarangire na pori la akiba la Mkungunero.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kimotorok Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara baada ya kufika eneo hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti akizungumza mbele ya Mawaziri saba waliofika kusikiliza mgogoro wa ardhi kati ya wakazi wa Vijiji vya Kimotorok Wilayani Simanjiro na Irkushbor Wilayani Kiteto na hifadhi ya Taifa ya Tarangire na pori la akiba la Mkungunero.
Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya akizungumza huku amefunga shuka ya kimasai juu ya manyanyaso waliopata wananchi wa Kijiji cha Kimotorok kutokana na mgogoro wa ardhi na hifadhi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...