NA BALTAZAR MASHAKA, SENGEREMA.

MKURUGENZI wa kampuni ya Baraka Mining inayojihusisha na uchimbaji wa madini ya dhahabu, almasi na vito, Baraka Chilu ameahidi kujenga madrasa itakayotumika kufundishia elimu ya dini hiyo, kununua pikipiki na mazuria ya msikitini hapo Kijiji cha Kasenyi wilayani Sengerema.

Pia Chilu ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri ya BAKWATA Sengerema alitoa fedha sh. 500,000 za kulipa posho ya miezi miwili ya mwalimu wa dini ya kiislamu, kati ya fedha hizo kiasi cha sh. 150,000 zitatumika kununulia baiskeli ya kumrahisishia usafiri wa kwenda na kurudi kutoa elimu kwenye shule za msingi na sekondari za Nyamahona.

Mgeni rasmi huyo wa maonyesho ya umahiri wa kuhifadhi Kuran na hadithi za Mtume Muhammad S.A.W.lililofanywa na wanafunzi wa madrasa ya Msikiti wa Kasenyi, alilionyeshwa kuguswa na changamoto ya wanafunzi hao kukosa sehemu sahihi ya kujifunzia elimu ya dini kutokan na risala iliyosomwa na katibu wa madrasa hiyo.

"Fanyeni tathmini ya gharama za ujenzi wa madrasa na nitakuwa tayari kuijenga.Kwa kuanzia natoa sh.500,000 za usafiri na posho ya mwalimu na baadaye nitamletea pikipiki mpya,nitanunua sare za wanafunzi wote 30 pamoja na mazuria ya msikitini,"alisema.

Awali akisoma risala Katibu wa Madrasa ya Msikiti wa Kasenyi,Hamidu Basinda alisema wana changamoto ya ukosefu wa jengo la madrasa kujifunzia, posho na usafiri wa mwalimu, sare za wanafunzi na maji kwa matumizi mbalimbali.

"Tunayo changamoto ya madrasa ya watoto kupata elimu ya dini na mazingira, tunatumia msikiti kutoa elimu hiyo, hakuna usafiri wa uhakika wa mwalimu kwenda kutoa elimu ya dini kwenye shule za umma.Changamoto ambazo zinakwamisha uislamu kustawi Kasenyi,"alisema Basinda.

Alisema licha ya uchumi wao mdogo wamefanikiwa kuboresha Msikiti wa Kasenyi kwa kuweka madirisha ya mbao na umeme kwa fedha walizouza mazao (vyakula anuwai) na kuimarisha nguzo za uislamu. 

Aidha, baada ya mfanyabiashara huyo kuahidi kujenga madrasa, Sheikh wa Msikiti wa Kasenyi Swadiki Mchwampaka ili kuunga mkono ufadhili huo aliwashauri waumini wa msikiti kuchangia nguvu zao.

"Shule ni biashara baina ya waja na Mwenyezi Mungu, tunahitaji kushikamana vizuri katika kuendeleza elimu ya dini (kiroho) na watoto ni haki yao kupata elimu ya mazingira na kiroho pia!Lakini pia ibada ndio msingi wa dini,inaleta heri na kukataa maovu,"alisema Sheikhe Mchwampaka na kuongeza;

"Usafiri umepatikana na tumeambiwa tutasaidiwa kujenga madrasa.Sasa na sisi tuchangie nguvu zetu ili kuunga mkono juhudi za mfadhili,."
Jengo la Msikiti wa zamani wa Kasenyi linalotumika kama madrasa ya kufundishia elimu ya dini ya Kiislamu likiwa nimechakaa na kupata nyufa na hivyo kuhatarisha Maisha ya wanafunzi.
  Mkurugenzi wa kampuni ya Baraka Mining, Baraka Chilu (kulia) akimkabidhi fedha sh.500,000 Sheikhe wa Msikiti wa Kasenyi Sheikhe Swadiki Mchwampaka kwa ajili ya posho ya mwalimu wa madrasa na kununulia baiskeli.Chilu ameahidi kujenga madrasa ya msikiti huo. 
  Sheikhe wa Msikiti wa Kasenyi Swadiki Mchwampaka (kulia) akimuonyesha Mkurugenzi wa Baraka Mining, Baraka Chilu (kushoto) jengo la msikiti wa zamani ambalo limechakaa lakini limekuwa likitumika kama madrasa. Picha na Baltazar Mashaka

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...