Na Karama Kenyunko globu ya Jamii.

ALIYEKUWA Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura (52), kuaendelea kusota rumande baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kueleza kwamba haina mamlaka ya kumfutia kesi wala kumpa dhamana katika kesi ya Uhujumu uchumi inayomkabili.

Hatua hiyo imefikiwa leo Februari 14.2019 baada Mahakama kupitia Hakimu Mkazi, Mwandamizi Kelvin Mhina kutupilia mbali mapingamizi yaliyowasilisha na upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Majura Magafu akisema mahakama hiyo haina mamlaka ya kufanya chochote katika kesi hiyo hadi hapo itakapopata kibali cha kusikiliza kesi hiyo kutoka kwa DPP.

Katika mapingamizi yao, Magafu aliiomba Mahakama kuitupilia mbali kesi hiyo sababu katika mashitaka yote 17 yalilofunguliwa chini ya Sheria ya Uhujumu uchumi yalitakiwa yafunguliwe kama mashitaka ya kawaida ya jinai ambayo yanamruhusu mshitakiwa kujibu.

Pia alidai kuwa katika maudhui ya hati ya mashitaka hakuna hata kosa moja la uhujumu uchumi kama ilivyoainishwa kwamba ni kesi namba 10 ya uhujumu uchumi.Alidai kwa mujibu wa kifungu cha 129 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai( CPA) kinaipa mamlaka mahakama kukataa kusajili kesi endapo zitakuwa na makosa na kwamba sheria hiyo inampa Hakimu mamlaka ya kuikataa na kuitupilia
mbali.

Katika uamuzi wake,Hakimu Mhina amesema amepitia hoja za pande zote na anatupilia mbali mapingamizi ya upande wa utetezi.Akifanua sababu za kutupilia mbali, Amesema, pamoja na kifungu hicho cha 129 cha CPA, kifungu cha 3 cha Sheria ta Uhujumu Uchumi, kinaondoa mamlaka kwa mahakama ya Kisutu kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi, isipokuwa DPP atakapowasilisha kibali cha kuiruhusu mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo.

Hakimu Mhina amesema Mahakama hiyo ina mamlaka ya kumsomea mashitaka mshitakiwa na kusikiliza maelezo ya mashahidi (Commital) lakini haina mamlaka ya kuondoa kesi hiyo na kwamba masuala ya kisheria yaliyowasilishwa na upande wa utetezi, yanatakiwa kuelekezwa katika mahakama yenye mamlaka ambayo ni Mahakama Kuu.

"Mahakama imefungwa mikono na haina mamlaka ya kuondoa au kufanya maamuzi yoyote katika hati hii ya mashitaka, mpaka kitakapoletwa kibali kutoka kwa DPP," amesema Hakimu Mhina.Hata hivyo, baada ya kueleza hayo alisema upande wa utetezi wana haki ya kukata rufaa dhidi ya maamuzi hayo endapo haujaridhika.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi, Februari 28, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na mshitakiwa amerudishwa rumande.Katika kesi hiyo Wambura anakabiliwa na mashitaka ya kughushi, mashitaka ya kutoa nyaraka za uongo, mashitaka 13 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na mashitaka mawili ya kutakatisha fedha.Wakili wa Serikali, George Barasa alidai kuwa mshitakiwa huyo alitenda makosa hayo katika ofisi za TFF, kati ya Julai, 2004 na mwaka 2015.

Alidai kuwa Julai 6, mwaka 2004, mahali pasipojulikana ndani ya jiji la Dar es Salaam, Wambura alighushi barua ambayo aliiwasilisha TFF akijifanya barua hiyo imeandikwa na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Jek System Limited, E Maganga akidai malipo ya mkopo wa Dola za Marekani 30,000 zilizokopwa na TFF pamoja na riba.

Katika mashitaka ya kutoa nyaraka ya uongo ilidaiwa, mshitakiwa alitoa barua iliyokuwa haina kumbukumbu namba ya tarehe 6/7/2004 akijifanya kwamba ni barua iliyoandikwa na Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Jeck system Ltd. akidai kuwa anadai mkopo wa Dola za Marekani 30,000 pamoja na riba waliokopeshwa TFF huku akijua kuwa siyo kweli.

Katika mashitaka ya tatu hadi la 15, Wambura anadaiwa alijipatia kiasi jumla ya zaidi ya Sh milioni 95 kwa njia ya udanganyifu akidai kuwa fedha hizo ni sehemu ya malipo ya jumla ya kiasi cha fedha mbali mbali na riba kutoka kwa Jeck huku akijua kuwa siyo kweli.Wambura pia anadaiwa Juni 17 mwaka 2015 huko katika ofisi za TFF kwa njia ya udanganyifu, alijipayia Sh milioni 10 kutoka TFF kwa kuonyesha kuwa ni malipo ya Dola za Marekani 30,000 pamoja na riba kutoka kwenye kampuni hiyo ya Jeck jambo ambalo siyo kweli.

Kati ya Agosti 15 na Oktoba 21 mwaka 2014 huko katika ofisi za TFF, Wambura anadaiwa alijipatia Sh 25,050,000 kutoka TFF huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la kughushi.Pia ilidaiwa kati ya Machi 16 na Oktoba 21 mwaka 2015 mshitakiwa alijipatia sh. 75,947,924 kutoka TFF wakati akijua fedha hizo siyo halali zimetokana na shitaka la kughushi.

ALIYEKUWA Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura (52).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...