Na Ripota Wetu
JESHI la Polisi nchini Indonesia limeomba msamaha kwa kutumia nyoka kumtishia
mtuhumiwa wa wizi baada ya video kusambazwa katika mitandao ya kijamii nchini
humo.
Baadhi ya maofisa wa jeshi hilo la polisi katika video hiyo wameonekana wakicheka
na wengine waliokuwa wakimhoji mtuhumiwa huyo wakionekana kumuweka nyoka
shingoni mwa mshukiwa huyo aliyekuwa amefungwa pingu huku akipiga kelele
mashariki mwa eneo la Papua.
Habari iliyowekwa kwenye Mtandao wa Shirika la Habari la Uingereza(BBC) inadaiwa
kuwa mtuhumiwa huyo alifikishwa polisi kutokana na tuhuma za kuiba simu ya
mkononi.
Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini humo Tonny Ananda
Swadaya amesema haikupaswa kufanyika hivyo lakini ametetea mbinu hiyo akieleza
kwamba nyoka huyo hana sumu na kwamba wamechukua hatua kali dhidi ya
maofisa waliohusika.
Swadaya amefafanua kuwa maofisa hao wa polisi hawakumpiga mshukiwa na
kuongeza walichukua hatua kwa hiari yao kujaribu kumfanya mshukiwa akiri
makosa.
Kwa upande wake Wakili anayetetea haki za binaadamu Veronica Koman ametuma
ujumbe kwenye mtandao wa Twitter ulioonyesha video hiyo, akidai kuwa maofisa hivi
karibuni walimtishia mwanaharakati anayetetea uhuru wa Papua kwa nyoka akiwa
gerezani.
Hata hivyo inaelezwa sauti katika video hiyo iliyosambaa inaarifiwa kusikika ikitishia
kumweka nyoka huyo ndani ya mdomo wa mshukiwa na ndani ya suruali yake.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...