Na Teresia Mhagama

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, ameeleza kuwa, mkandarasi yeyote anayesambaza umeme vijijini, ikitokea amewadanganya wananchi na Serikali kwa kutotekeleza majukumu yake kadri ya makubaliano, atachukuliwa hatua za kinidhamu.

Dkt. Kalemani aliyasema hayo akiwa wilayani Gairo mkoani Morogoro ambapo alifika katika Kijiji cha Kibedya kwa ajili ya kukagua kazi usambazaji umeme na kutoridhishwa na kasi ya mkandarasi.

“Nilipanga kuja hapa mwezi Disemba mwaka jana na ndipo Mkandarasi huyu akaamua kuleta umeme hapa, lakini sikuja na yeye akasimamisha kazi, hivi leo nimekuja kukagua na kukuta nyumba nyingi bado hazijaunganishiwa umeme na nguzo zimelala badala ya kutumika kusambazia watu nishati hii muhimu,” alisema Dkt Kalemani.

Kutokana na hilo, Dkt. Kalemani alitoa agizo kwa Mameneja wa TANESCO wa mikoa na Wilaya kuhakikisha kuwa wakandarasi wa umeme vijijini wanasambaza umeme katika maeneo yote waliyopangiwa vinginevyo Mameneja hao wajiondoe wenyewe kwa kushindwa kusimamia kikamilifu mradi huo.

“ Ili kutekeleza mradi huu kwa kasi, naendelea kusisitiza agizo la Serikali kuwa kila mkandarasi lazima awe na magenge matano ya kazi katika eneo lake, ili kutorudisha nyuma juhudi za Serikali za kuwasambazia umeme wananchi,” alisema Dkt Kalemani.

Akiwa katika Kijiji hicho, Dkt Kalemani aliwasha umeme ambao unatumiwa na wateja wa awali waliounganishwa na kutoa siku 13 kwa Meneja wa TANESCO, Wilaya ya Gairo kuwasambazia umeme wananchi waliosalia ambao tayari wameshalipia huduma ikiwa ni pamoja na vitongoji vya Kijiji hicho.

Aidha, amewataka Mameneja wa TANESCO nchi nzima, kuwafuata wananchi katika maeneo yao ili kutoa huduma kwani Serikali imewapa vitendea kazi kama magari ili kuwasogezea huduma wananchi badala ya wananchi hao kufuata huduma katika ofisi za TANESCO ambazo nyingine ziko mbali na wananchi hao..

Kwa upande wake, Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby, aliishukuru Serikali kwa juhudi zake za kusambaza umeme vijijini kwani Vijiji vyote katika Wilaya ya Gairo vipo katika mpango wa kusambaziwa umeme na tayari vingine vimeshaunganishwa na nishati hiyo.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa huduma ya umeme katika Kijiji cha Kibedya wilayani Gairo mkoa wa Morogoro. Wa pili kulia ni Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby na wa Pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Gairo Siriel Nchembe.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) akizungumza na wataalam wa TANESCO pamoja na mkandarasi anayesambaza umeme vijijini wilayani Gairo mkoani Morogoro wakati alipofika katika Kijiji cha Kibedya wilayani humo kukagua kazi ya usambazaji umeme. Wa Pili kushoto ni Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akizungumza na baadhi ya wananchi katika Kijiji cha Kibedya wilayani Gairo wakati alipofika kukagua mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...