Na Estom Sanga-Nachingwea 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Mheshimiwa George Mkuchika amekumbana na kilio cha Wananchi wa wilaya za Liwale na Nachingwea Mkoani Lindi cha kuomba serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF kuwajumuisha kwenye huduma za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili nao waweze kunufaika na huduma za Mpango huo. 

Wakitoa taarifa za Utekelezaji wa Mpango huo kwa Waziri Mkuchika ambaye yuko katika ziara ya kikazi mkoani Lindi,viongozi wa serikali za vijiji na wilaya hizo wamesema mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Mpango huo yameibua hamasa ya Wananchi kujiletea maendeleo na hivyo kupunguza kero ya umaskini. 

“Mheshimiwa Waziri,Mpango huo unatekelezwa katika takribani nusu ya vijiji vya wilaya yetu na kuacha sehemu kubwa ya wananchi bila huduma hiyo muhimu iliyoanzishwa na serikali yetu,tunaomba wananchi wenye sifa za kujumuishwa kwenye Mpango huo wapate fursa hiyo muhimu” amesisitiza Mbunge wa Nachingwea Mwl……… 

Wananchi ambao hawajajumuishwa kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya maskini wamemweleza Mheshimiwa Mkuchika kuwa wao pia wanastahili kupata huduma za Mpango huo kwani pia wanakabiliwa na umaskini na kuwa wako tayari kutekeleza masharti ya Mpango kwani kwa sasa wameona faida zake kutoka kwa Walengwa ambao wameboresha maisha yao kwa kiwango kikubwa. 

Akihutubia mikutano mbalimbali ya Wananchi katika Wilaya za Liwale na Nachingwea ,Mhe. Mkuchika ameweka bayana mipango ya Serikali Kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF –kuwa sehemu ya pili ya Awamu ya Tatu ya Mapngo huo ambayo inatarajiwa kuanza hivi karibuni itahakikisha kuwa vijiji /shehia ambazo hazikujumuishwa katika sehemu ya kwanza ambazo ni asilimia 30 nchini kote zinapata pia fursa hiyo. 

“tutahakikisha kuwa tunawaandikisha Wananchi wote wenye sifa za kunufaika na huduma za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na serikali kupitia TASAF ili vita dhidi ya umaskini iwe endelevu na yenye kasi ya kuridhisha” amesisitiza Mheshimiwa Mkuchika. 

Aidha Waziri huo wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora amekuwa akisisitiza juu ya umuhimu wa viongozi katika ngazi za vijiji,kata,wilaya na hata mkoa kuhakikisha kuwa wanakuwa karibu zaidi na Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na kutoa hamasa kwa Walengwa hao kutumia ruzuku wanayopata kujiletea maendeleo kwani suala la kupambana na umaskini limebainishwa kwa ufasaha kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015. 

Katika hatua nyingine Mheshimiwa Mkuchika ameridhishwa na hatua ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF kuendelea kujenga miundombinu katika sekta ya elimu,afya na maji katika maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa Mpango na hivyo kupunguza adha ya kufuata huduma hizo mbali na maeneo yao kwa Walengwa na Wananchi wengine kwenye maeneo hayo. 

Ameyasema hayo alipokagua madarasa yaliyojengwa na TASAF katika Shule ya Msingi Kongo wilayani Nachingwea ambako pia TASAF imejenga tanki la maji,vyoo,madawati, meza ,makabati na kuweka umeme wa jua(solar panel) katika shule hiyo ya msingi kwa kuwashirikisha walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia utaratibu wa Ajira za Muda.
Waziri Mkuchika akifurahia zawadiya kuku aliyopewa na Walengwa wa TASAF wilayani Nachingwea Mkoani Lindi baada ya kuwahutubia wananchi na walengwa hao.

 Waziri Mkuchika akikagua madarasa yaliyojengwa na TASAF katika shule ya msingi Kongo wilayani Nachingwea mkoani Lindi akiwa kwenye ziara ya kikazi wilayani humo.
 Waziri Mkuchika akizungumza na wanafunzi katika shule ya msingi Kongo wilayani Nachingwea ambako TASAF imejenga madarasa,vyoo,tanki la maji na mfumo wa umeme jua (solar )

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...