Na Felix Mwagara, MOHA-Arusha. 

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewasili jijini Arusha leo, kwa ajili ya kuanza ziara yake ya kikazi ya siku kumi kwa kutembelea Wilaya zote za Mkoa huo akisikiliza kero za wananchi pamoja na kufuatilia maagizo yake aliyoyatoa kwa vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo ndani ya Wizara yake. 
Waziri Lugola anatarajia kuanza ziara hiyo rasmi kesho Februari 13, 2019 jijini humo kwa kukutana na Mkuu wa Mkoa pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na kupokea taarifa ya Kamati hiyo, kabla ya kuanza kuzungumza na Wakuu wa vyombo vyake na baadaye atakutana na Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa, na kumaliza kwa kuzungumza na Baraza la Askari na Watumishi wote wa Wizara hiyo waliopo jijini humo. 

Akizungumza na Mwandishi wa habari hii, leo, Lugola amesema baada ya kuzungumza na Askari na Watumishi wa Wizara yake pamoja na kupokea changamoto zao, atafanya mkutano mkubwa wa hadhara wa wananchi utakaofanyika katikati ya Jiji hilo ili wananchi wengi waweze kufika kwa wingi na aweze kusikiliza kero zao na Waziri huyo kuweza kuzitatua. 

“Nitafanya mkutano mkubwa wa hadhara katika jiji la Arusha, ambapo utaanza saa 10:00 hadi 12:00 jioni, hivyo nawaomba wananchi wa Jiji hili wajitokeze kwa wingi kunisikiliza kile ambacho nimepanga kuwaambia na pia nitawapa nafasi wananchi waulize maswali bila woga, waniambie kero zao nami nitazitatua katika mkutano huo,” alisema Lugola. 

Pia Lugola alisema lengo la ziara hiyo ni kufuatilia maagizo yake mbalimbali ambayo aliyatoa mwaka jana 2018 katika mikutano yake kama yalifanyiwa kazi na viongozi wa Taasisi anazoziongoza au yalipuuzwa, yakiwemo ya dhamana zitolewe saa 24 katika vituo vyote vya polisi nchini, na pia kupiga marufuku tabia ya baadhi ya Polisi kubambikizia kesi wananchi, na pamoja na agizo la pikipiki zote zilizopo vituoni ziondolewe. 

Lugola alisema katika ziara yake aliyoifanya mwaka jana Mkoani Kigoma na mwezi Januari Mwaka huu Mkoa wa Kagera, aligundua wananchi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali hivyo hawezi kulala akiwa ofisini, lazima afanye ziara nchi nzima kuwasaidia wananchi kutatua kero zao ambapo wengi wao wakiwalalamikia Polisi wakiwaonea. 

Waziri Lugola ameongeza kuwa, kupitia mikutano yake ya wananchi mkoani Kigoma na Kagera ndipo ameamua kufanya ziara ya tatu kwa kuutembelea Mkoa wa Arusha ambao changamoto zake zinafanana kwa sehemu kubwa kwa kuwa mikoa hiyo ni ya mipakani na changamoto kubwa ni uwepo wa wahamiaji haramu pamoja na matukio kadhaa ya ujambazi ambayo kwa kiasi kikubwa Serikali inaendelea kuyadhibiti. 

“Wananchi wanapojitokeza kwa wingi inasaidia kusikiliza matatizo yao yanayowakabili, ndio mana nimepanga kufanya ziara kama hizi nchi nzima, hii inasaidia sana kujua matatizo mbalimbali ya wananchi pamoja na kuangalia utendaji kazi wa Taasisi zangu zilizopo ndani ya Wizara hii, na hakika Serikali ya Rais Dokta John Magufuli inawajali wananchi wake ndio mana inawafuata mahali walipo, ili wazungumze na Serikali yao uso kwa uso,” Alisema Lugola. 

Waziri Lugola baada ya kumaliza ziara yake Jijini Arusha, ataenda Wilaya ya Arusha ambayo itakua Februari 14, Meru Februari 15, Arumeru, baadaye Longido, Monduli, Karatu na ataimaliza ziara yake akiwa Wilaya ya Loliondo mkoani humo. 

Katika Wilaya zote atakazozitembelea pia atazungumza na wananchi pamoja na watumishi waliopo ndani ya Wizara yake ambao ni Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Magereza, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, pamoja na Idara ya Probesheni ambayo jukumu lake kuu ni kupunguza msongamano gerezani na kusimamia wafungwa waliopewa adhabu mbadala na Mahakama au wafungwa waliopata msamaha kupitia sheria ya huduma kwa jamii na kutumikia kifungo chao nje ya Gereza.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...