WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa siku 16 kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Magreth John awe amepeleka asilimia 20 sawa na sh milioni 114 ya kijiji cha Holili kabla ya Machi 10 mwaka huu, fedha hizo zinatokana na mauzo ya madini ya pozolana.

Ametoa maagizo hayo leo (Jumamosi, Februari 23, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha cha Holili pamoja na wananchi wa kijiji cha Holili, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Kilimanjaro. Kituo hicho kipo katika mpaka wa Tanzania na Kenya.

Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo baada ya wananchi wa kijiji cha Holili kuwasilisha malalamiko yao kupitia mabango wakimuomba awasaidie ili Halmashauri hiyo iweze kulipa fedha zao zinazotokana na mapato ya mauzo ya madini hayo yanayochimbwa kijijini kwao.

“Mkuu wa wilaya (Agness Hokororo) simamia kuhakikisha kiasi hicho cha fedha kinakwenda kwa wananchi na Mkuu wa Mkoa (Dkt. Anna Mgwira) nataka nipate taarifa kuwa fedha hizo zimeshalipwa kwa uongozi wa kijiji husika.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watendaji katika maeneo mbalimbali nchini kuwa wamepelekwa huko kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, hivyo hawana budi kutenga muda wa siku tatu kwa wiki na kwenda maeneo ya vijijini kusikiliza kero zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema hali ulinzi na usalama katika mpaka huo si nzuri, Serikali imeamua kuimarisha ulinzi kwenye mpaka huo, hivyo ni muhimu kwa wananchi washirikiane katika kuulinda mpaka huo.

Hivyo, Waziri Mkuu ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwakamata na kuwachukulia hatua watu wote watakaokamatwa wakipita au kuingiza mizigo kupitia njia zisizo rasmi kwa sababu hao ndio wanaopitisha silaha.

Waziri Mkuu amesema wananchi wa Tanzania na Kenya hawajazuiwa kufanya biashara upande wowote bali wanatakiwa wafuate sheria, kanuni na taratibu zilizopo katika nchi husika ikiwa ni pamoja na kutumia njia rasmi.

Amewataka viongozi na watendaji waliopo maeneo ya mipaka huo wa Holili wawe makini kwa sababu mpaka huo hauko salama na kuna mambo mengi yanayoendelea ambayo yapo kinyume cha sheria.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...