Na Moshy Kiyungi,Dar es Salaam.

Mwanamuziki Hussein Jumbe anayo historia ndefu katika muziki hadi kuweza kumiliki bendi yake.

Wanamuziki wengi hapa nchini wamepitia mitihani mingi, ikiwemo ya taabu, mashaka na vikwazo kemkemu hadi kuyafika mafanikio.

Hapa uvumulivu wa mtu binafsi unachukua nafasi kubwa ya kuyafikia mafanikio hayo wala siyo kukata tamaa.Husseni Suleiman Jumbe 'Mzee wa Dodo' kama anavyojulikana kwa wengi, ni mifano unaoweza kuyakinisha hayo.

Ni mwanamuziki nguli aliyejaaliwa vipaji adhimu vya sauti ya uimbaji, utunzi uliojaa hisia na zinazosisimua zaidi, ambazo mara nyingi hugusa kila rika la watu.Jumbe alipata elimu yake ya msingi katika Shule za Uhuru Mchanganyiko na Sekondari ya Muslim, zote za Dar es Salaam.
‘Mzee wa Dodo’ aliwahi kutamka kuwa aliamua kujifunza muziki baada ya kuvutiwa na nyimbo za marehemu Marijani Rajab 'Jabali la muziki'."Nilikuwa natembea na radio yangu kwa ajili ya kusikiliza nyimbo za Marijani, enzi hizo akiwa na bendi ya Safari Trippers,” Jumbe alisema.

Vibao vya Marijani Rajab vilivyokuwa vikimpagawisha zaidi ni 'Roza nenda shule', 'Mwalimu Nyerere' na 'Nani mchokozi'.Hussein alisema kwamba kabla nyimbo hizo hazijatoka kwenye redio, alizijua na kwamba alikuwa akiziimba kila alipokwa ameketi, wakati huo ndio kwanza alikuwa bado yuko shule ya msingi.

Jumbe anakumbuka zaidi kuwa kutokana na mapenzi yake kwa Marijani, mara kwa mara alikuwa anatembelea maonyesho yake na kila Jumapili.
Alikuwa hakosi kwenda katika ukumbi uliokuwa ukijulikana kama Princess uliokuwa maeneo ya Mnazi Mmoja kwenye 'bugi dansi' dansi la mchana siku za Jumapili lililoisha saa kumi na mbili jioni, ambapo kiingilio chake kilikuwa shilingi tano tu.

Mnamo mwaka 1979, wakati akiwa darasa la nne, alijiunga kwa siri na kundi la Orchestra Siza, ambalo maskani yake yalikuwa Mtaa Ruvuma, Temeke, jijini Dar es Salaam ambako pia ndiko alikokuwa akiishi yeye.Katika kundi hilo Jumbe alisema kuwa ndiko kwa mara ya kwanza alikokutana na mwanamuziki Roshi Mselela.Roshi alikuwa mtunzi na mwimbaji katika bendi ya Super Matimila, aliyemuelezea kuwa walikuwa wakipatana kupita kiasi, akawa bado anaendelea na muziki kwa siri.

Waswahili wanasema “Siri haitambi mkono wa pili”, mwaka mmoja tu baadae wazazi wake wakagundua ‘janja’ yake ya kujiingiza katika muziki, na kuzembea masomo shuleni, wakamgombeza na kumpiga marufuku kufanya muziki. Hata hivyo, mwenyewe Jumbe anakiri kwamba kuishi bila kujihusisha na masuala ya muziki ilikuwa ngumu kwake.

Mwaka 1981 akajiunga tena kwa siri na kundi lingine la muziki wa dansi la Asilia Jazz, ambalo lilikuwa likimilikiwa na Baraza la Muziki Tanzania (BAMUTA)."Safari hii, baba alipokuja kugundua kuwa naendelea kujishughulisha na muziki, alinichukua na kunipeleka kufanyakazi katika kiwanda cha Plastiki," anasimulia Jumbe na kufafanua kuwa hapo aliajiliwa kama msimamizi wa uzalishaji (Production Foremen).

Huku akicheka, Jumbe akasema kuwa aliacha kazi kiwandani hapo, baada ya kuona anakosa muda wa kwenda kwenye mazoezi ya muziki. Matokeo yake familia yao yote ilimtenga na kumsusa kabisa."Nakumbuka katika kipindi hicho nilichosuswa na familia, nilitaabika kwa dhiki mpaka nilifikia hatua ya kuvaa nguo zenye viraka," anasema Jumbe. 

Alisema kuwa, katika jitihada zake za kuhakikisha hautupi mkono muziki, mwaka 1983 alilikimbia jiji la Dar es Salaam na kwenda Tabora kutafuta bendi atakayoitumikia kwa kujinafasi.Huko akapokewa na mkongwe Shem Karenga ndani ya bendi ya Tabora Jazz, ambako pia alikutana na mwimbaji Mohammed Gotagota ambaye kwa sasa ni marehemu.Aliitumikia bendi ya Tabora Jazz kwa miaka miwili, akachomoka akaenda katika mji wa Musoma, mkoani Mara.

Huko alikaa mwaka mmoja tu wa 1985 na ilipofika 1986 aliamua kurejea Dar es salaam baada ya kupokea taarifa ya msiba wa baba yake mzazi."Nilipowasili, nilikuta tayari baba amekwishazikwa," anaongea kwa huzuni kubwa Jumbe.Alisema kuwa baada ya hapo hakuona haja ya kuwa mbali na familia hivyo alimfuata Hamis Gotagota, aliyekuwa bendi ya Urafiki wakati huo.

Gotagota akamuunganisha kwa uongozi wa bendi hiyo, akakubali kuwa mwimbaji wa bendi hiyo.Bendi ya Urafiki Jazz 'Wana Chakachua' wakati huo ilikuwa ikiongozwa na Juma Mrisho 'Ngulimba wa Ngulimba', ndipo Jumbe alipoanza kudhihirisha makali yake katika utunzi na uimbaji, kwani aliporomosha kibao kizito kilichokwenda kwa jina la “Usia wa Mama”. 

Oktoba 17, 1987 aliitwa na mtu asiyemfahamu ambaye alimueleza kuwa amependezwa na uimbaji wake, hivyo siku hiyohiyo aende makao makuu ya Mlimani Park yaliyoko karibu na Chuo Kikuu Dar es Salaam.

Yule mtu alikuja kumtambua baadae kuwa kumbe alikuwa Hassan Rehani Bichuka 'Super Stereo'.“Wimbo wangu ya kwanza kabisa kutunga nikiwa na Wana Mlimani Park ni ule usemao 'Hisia za mwanadamu'.

Mwaka 1990 bendi ya Mlimani Park Orchestr ilishiriki mashindano ya nyimbo kumi bora, wimbo wake huo ukushika nafasi ya tatu. Nafasi ya kwanza ilinyakuliwa na bendi ya MK Group 'Ngoma za Magorofani’ na ya pili ikatwaliwa na Salna Brothers.Alidumu Mlimani Park kwa muda mrefu na kushiriki kuimba na kutunga vibao vingi vikali ambavyo baadhi yake ni ‘Epuka No2’, ‘Nuru ya Upendo’, ‘Shamba’, ‘Mtoto wa Mitaani’, ‘Chozi la Kejeli’, ‘Nachechemea’ na ‘Isaya Mrithi Wangu’ ambazo kila moja kwa wakati wake ilitikisa vilivyo. 

Mwaka 2002, aliondoka DDC na kujiunga na TOT Plus 'Achimenengule', ambapo kama kawaida yake, akiwa na kundi hilo lililokuwa chini ya Mbunge wa Mbinga Magharibi, Capt John Damian Komba, Jumbe aliporomosha vibao viwili moto wa kuotea mbali.Vibao hivyo ni 'Gunia la mazoezi' na 'Nani Kaiona kesho', ambavyo vyote viko katika albamu moja ya ‘Sarafina’ iliyofyatuliwa mwaka huohuo 2002, ambayo ilikuwa na jumla ya nyimbo sita.

Jumbe alidumu TOT kwa miaka miwili, akatoka na kwenda kujaribu upepo katika bendi ya Msondo Ngoma Music. Huko alikutana na wakongwe we dansi kama vile Muhiddin Gurumo, Suleiman Mbwembwe, Joseoh Maina, Athuman Momba na Tx Moshi William, wote ni marehemu.Akiwa na Msondo, Jumbe alifanya vitu vizito kwenye albamu iitwayo ‘Ajali’ aliposhiriki kuimba kwa takriban nyimbo zote akitumia ufundi wa njia ndogo ya sauti ujulikanao kitaalamu kama 'Minor' na kutunga vibao 'Transfer' na 'Sumu ya Ufukara'.

Tofauti na wanamuziki wengine wengi wanapohama bendi hukashifu alikotoka.Jumbe yupo tofauti kabisa kwa kuwa hadi leo anaisifu Msondo kwa kusema kuwa ni bendi ambayo wanamuziki wake hawana majungu, fitina wala nyoyo za chikichiki. 

"Msondo wenzetu wanapendana halafu lao moja, hawana majungu hata kidogo," anasema Jumbe anapoulizwa kuhusu bendi hiyo inayotumia mtindo wa 'Mambo Hadharani'. 

Hivi sasa, Jumbe ambaye ni baba wa familia mwenye watoto wanane na mkewe Zakhia Jumbe, anayekiri kuwa maendeleo katika muziki ni 'matokeo'. Juhudi zake binafsi ameweza kupata mafanikio makubwa hasa baada ya kuanzisha bendi yake.

Jumbe alisema kuwa tayari anamiliki bendi yake ya Talent, yenye albamu tatu, ambazo ni ‘Kwangu ni Wapi’, ‘Subiri Kidogo’ na ‘Kiapo Mara Tatu’.

Hussein Jumbe alisema hivi sasa wapo jikoni wanapika albamu nyingine itakayokusanya vibao vikali kama ‘Nyumba ya Urithi’, ‘Kaolewa Ramadhani Kaachika

Ramadhani’ na ‘Ukienda Kuomba Mboga’. 

Ndani ya vibao vyote kwenye albamu zilizotangulia za Talent Band, Jumbe ameonyesha ukomavu mkubwa kisanii kuanzia ujumbe hadi ala, kumemfanya afanikiwe kupata maendeleo makubwa zaidi ya alipokuwa mwajiriwa.

Hii ndiyo safari yake Hussein Jumbe katika muziki.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...