Na Kiyungi Moshy,Dar es Salaam.

Kama kuna mwanamuziki ambaye hawezi kusahaulika katika kumbukumbu za wapenda muziki, ni Dk. Remmy Ongalla.

Desemba 13, 2018 alitimiza miaka minane tangu afariki dunia usiku wa kuamkia Jumatatu Desemba 13, 2010 nyumbani kwake Sinza, jijini Dar es Salaam.

Ilikuwa ni siku ya majonzi kwa wapenzi wa muziki wa dansi hapa nchini, Afrika ya Mashariki na Ulimwenguni kwa ujumla baada ya kusikika kwa kifo chake.

Dk. Remmy aliwaacha wapenzi wake na wananchi kwa ujumla katika dimbwi la majonzi yasiyosahaulika kufuatia tungo za nyimbo zake zenye maudhui maridhawa.Nyimbo hizo hadi leo zinarindima katika vituo vingi vya redio hapa nchini hata nje ya mipaka yetu.

Yapo mambo kadhaa aliyoyafanya ambayo yanasababisha watu wengi kutokumsahau nguli huyu.

Dk. Remmy alikuwa wa kwanza kupata ujasiri wa kukemea ngono zembe, akatunga wimbo ‘Mambo kwa soksi’ Lakini jamii ikambeza kwamba wimbo huo haukuwa na maadili mema. Baadaye viongozi wa serikali, vyama na dini na wengine kwa ujumla walielewa nini alichokuwa akisema Dk. Remmy, wakaanza kuhubiri majukwaani tahadhari hiyo.

Alijipatia umaarufu katika jiji la Dar es Salaam hususan maeneo ya Sinza, kufuatia gari lake dogo ‘soloon’ ambalo popote lipitapo watu walilishangaa. Lilikiwa na maandishi nyuma ya gari hilo yakisema ‘ Baba yako analo’?

Dk. Remmy alizaliwa mwaka 1947 katika mkoa wa Kivu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Familia yake iliishi katika eneo lililoitwa Kindu eneo ambalo halikuwa mbali sana kutoka mpakani na Tanzania.
Yaelezwa kwamba mara alipozaliwa, wazazi wake walimuita majina ya Ramadhani Mtoro Ongala.

Baba yake alikuwa mwanamuziki mashuhuri pia alikuwa mpiga ngoma kwa kutumia mkono na pia mbira.Remmy akiwa bado mchanga familia ilihamia katika mji wa Kisangani huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Zipo habari kwamba kabla ya kuzaliwa kwake, mama yake alipata ujauzito mara mbili lakini kwa bahati mbaya kila alipojifungua, mtoto alifariki. Alipopata ujauzito mara ya tatu alienda kwa mganga wa kienyeji kumuomba ushauri afanye nini ili mtoto atakayezaliwa asiiage dunia pia.
Bila kusita mganga wa kienyeji akampa ushauri wake, akamwambia kwanza safari hii asiende kujifungulia hospitali bali akajifungulie maporini. Pia alipewa ushauri kwamba mtoto akishazaliwa asije akamkata nywele zake. Yote hayo yalitendeka.

Yasemekana Remmy alizaliwa akiwa tayari na meno mawili ya mbele, akaonekana kama mtoto wa ajabu.Kuzaliwa akiwa hivyo ikachukuliwa kama ishara ya baadaye kuja kuwa mganga wa kienyeji .

Ili kutimiza maelekezo ya mganga, Dk. Remmy hakuwahi kunyolewa nywele zake kwa miaka yote hadi alipokuja kuokoka akiwa hapa nchini Tanzania.

Mwenyewe aliwahi kusema kwamba mwanzoni alikuwa anajisikia aibu sana kwa kuwa na nywele ndefu namna ile. Lakini baadaye jina na taswira ya mfalme wa reggae ulimwenguni, hayati Bob Marley lilipopata umaarufu nchini Kongo, ndipo alipoupenda mtindo huo wa nywele kwani hata watu wengine pia walianza kuukubali na kuuonea fahari.

Baba yake ndiye aliyeanza kumfunza mambo ya muziki tangia akiwa mdogo kabisa. Jambo lililomfanya aamini kabisa kwamba kama jinsi ambavyo watu wengine wamezaliwa kuwa madaktari, wanasheria, waalimu, wakulima nk, yeye alizaliwa ili awe mwanamuziki.

Kwa bahati mbaya baba yake huyo alifariki dunia mwaka 1953, akamuacha Remmy akiwa na miaka sita.

Baadaye alianza shule ya msingi, lakini kutokana na ukosefu wa fedha na kwa sababu mama yake hakuweza kuendelea kumlipia karo za shule, Remmy ilibidi aache masomo shuleni hapo.

Ilipofika miaka ya 1960, Remmy tayari alikuwa ameshafuzu kupiga gitaa.

Mwaka mmoja baada ya kifo cha Baba yake mzazi, mwaka uliofuatia wa 1954, ulikuwa si mzuri tena kwa Remmy. Alkipata pigo la kufiwa na mama yake mzazi jambo ambalo lilimuacha na mzigo wa kuwalea wadogo zake kwani yeye sasa ndio alikuwa mkubwa katika familia licha ya umri wake mdogo.

Bila elimu na ujuzi mwingine wowote, alilazimika kuanza rasmi kujitafutia riziki kupitia muziki. Ujuzi wake wa kupiga gitaa uliongezeka kwa kasi ya ajabu kitu ambacho kilimuwezesha kutumbuiza kwa kupiga ngoma na gitaa katika hoteli na sehemu mbalimbali nchini ya Kongo, akiwa na kundi lake lilokuwa limesheheni vijana wenzake lililoitwa ‘Bantu Success’.

Kwa miongo kadhaa iliyofuatia Dk. Remmy Ongala alizunguka katika sehemu mbalimbali za Kongo akiambatana na bendi kadhaa maarufu za wakati huo nchini Kongo zikiwemo Success Muachana na ile ya Grand Mickey Jazz.

Japokuwa kwa ujumla Dk. Remmy alijifunza mwenyewe kupiga gitaa, lakini aliwahi kukiri kwamba muziki wa kutoka nchini Cuba ambao wakati huo ulikuwa unaanza kujipatia umaarufu barani Afrika, ulimsaidia katika kupata mitindo kipekee katika upigaji gitaa.

Kwa upande wa uimbaji anasema uimbaji wa Joseph Kabasele ‘Grand Kale’ na ule wa Franco Lwambo Makiadi ulimsaidia kupata mitindo yake ya uimbaji kama alivyozoeleka kusikia enzi za uhai wake.

Mwaka 1978 Remmy aliingia jijini Dar es Salaam baada ya kuitwa na mjomba wake mzee Kitenzogu Makassy ili aje ajiunge na bendi maarufu ya wakati huo ya Orchestra Makassy, iliyokuwa chini ya uongozi wa mjomba wake huyo.

Huo ukawa ndiyo mwanzo wa maisha ya Dk. Remmy nchini Tanzania. Akiwa na bendi ya Orchestra Makassy, alitunga wimbo wake wa kwanza uliojulikana kama ‘Siku ya Kufa’, wimbo ambao aliuandika kumkumbuka rafiki yake aliyefariki dunia. Wimbo huo pamoja na ule wa Athumani zilianza kumpatia umaarufu mkubwa na kujulikana kwa haraka hapa nchini.

Hata hivyo mzee Makassy baadaye aliamua kuihamishia bendi yake nchini Kenya. Kitendo hicho cha mjomba wake kilichomfanya Dk. Remmy kwenda kujiunga na bendi ya Matimila baada ya kudumu kwa katika bendi ya Orchestra Makassy kwa takriban miaka mitatu hivi.

Kujiunga kwa Remmy katika bendi ya Matimila, kulimuongezea umaarufu zaid katika anga za muziki nchini Tanzania wakati huo. Jina la bendi hiyo ya Matimila lilitokana na jina la kijiji kimoja kilichoko kusini mwa Tanzania.

Chini ya uongozi wake Dk. Remmy aliisuka upya bendi hiyo na kuibadilisha majina ikaitwa Orchestra Super Matimila.

Miaka iliyofuatia Watanzania walishuhudia umaarufu wa Remmy ukiongezeka kutokana na mashairi ya nyimbo zake ambayo yaliegemea katika kuzungumzia mambo halisi ya kijamii kama vile umasikini, afya, siasa , majanga ya Ukimwi nk.

Mafanikio ya Remmy na kundi lake zima la Orchestra Super Matimila hayakuishia nchini Tanzania kwani katika miaka ya mwishoni ya 1980 walianza kujipatia umaarufu nje ya mipaka ya Tanzania na Afrika hadi Ulaya.

Dk.Remmy Ongala aliwahi kusema kwamba kupata mialiko ya nje lilikuja kama mchezo tu. Kasseti yenye nyimbo zao ilichukuliwa na rafiki yake mmoja mzungu aliyekuwa akiondoka nchini Tanzania kurejea kwao Uingereza.

Rafiki yake huyo alipofika huko aliwapatia jamaa wa WOMAD (World of Music, Arts and Dance) Shirika linalopandisha chati wanamuziki na wasanii mbalimbali kutoka katika nchi za dunia ya tatu.

WOMAD walivutiwa na nyimbo zao, hivyo kuwapa mwaliko kushiriki katika maonyesho yao Barani Ulaya ya mwaka 1988.

Baada ya kurudi kutoka Ulaya bendi ya Super Matimila ilitoa album yenye jina la ‘Nalilia Mwana’ ikiwa na mkusanyiko wa nyimbo zao zilikuwemo nyimbo zilizopendwa sana kama vile ‘Ndumila Kuwili’ na ‘Mnyonge Hana Haki’

Mwaka 1989 Super Matimila walirudi tena Ulaya kufuatia mwaliko mwingine wa WOMAD. Ni wakati huo huo ambapo walipata nafasi ya kurekodi kwenye studio ya kisasa zaidi ya Stud Real World Studios, ambayo ilikuwa inamilikiwa na mwanamuziki maarufu aitwaye Peter Gabriel.

Dk. Remmy aliwahi kufafanua kuwa wimbo maarufu ya ‘Kipenda roho’ aliuimba mahsusi kwa ajili ya mkewe ambaye ni ‘mzungu’ Mwingereza ambaye wakati huo tayari walikuwa wameshazaa naye watoto watatu.

Mwaka 1990, Remmy na bendi yake ya Super Matimila walirejea tena katika studio za Real World ambako walirekodi album nyingine yenye nembo ya ‘Mambo’ .

Albam hiyo ilikuwa na nyimbo kama hiyo ya ‘Mambo’ ambayo aliimba kwa lugha ya kiingereza na kuweza kukidhi kiu ya wapenzi wake wasiojua Kiswahili. Zingine ni pamoja na ‘No money, no life’ na ‘One World’.

Umaarufu wake ulizidi kung’ara mwaka 1990 alipoachia wimbo wa ‘Mambo kwa soksi’ ingawa baadhi ya watu waliupinga kwa kusema kwamba haukuwa na maadili mema kwa jamii, ingawa kimsingi alikuwa anawaasa watu hususani vijana kutumia kondomu ili kuepukana na maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi.

Akiwa Super Matimila Dk. Remmy alitoka na nyimbo nyingi zikiwemo za ‘Bibi wa mwenziyo’, ‘Kipenda roho’, ‘Asili ya muziki’ na ‘Ngalula’. Zingine ni pamoja na ‘Mwanza’, ‘Mama nalia’, ‘Harusi’, ‘Hamisa’, ‘Mnyonge hana haki’, ‘Ndumila kuwili’ na ‘Mataka yote’ ambazo zilimuongezea sifa kubwa Dk. Remmy kufuatia maudhui yaliyokuwa yakikidhi jamii.

Baadaye Dk. Remmy Ongala akaanza kusumbuliwa na maradhi ya Kisukari iliyompelekea kuamua kuachana na muziki wa dansi kwa madai ya kwamba umejaa mambo mengi ya kishetani.

Remmy akaokoka, akatubudu dhambi zake na akaanza kupiga muziki akimuimbia Bwana.Kabla ya kifo chake Dk. Remmy alitoa albamu yake ya Injili aliyooiita ‘Kwa Yesu kuna furaha’.

Kabla ya kifo chake, Remmy alikuwa katika hatua za mwisho za kukamilisha albamu yake ya pili, lakini mungu akampenda sana usiku wa kuamkia Jumatatu ya Desemba 13, 2010 nyumbani kwake Sinza.

Eneo hilo alilokuwa akiishi lilipewa jina la ‘Sinza kwa Remmy’ kabla ya kifo chake kufuatia umaarufu wake.

Mungu aiweke roho yake pahala pema peponi, Amina.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba:



0784331200,

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...