Na Moshy Kiyungi
Mwaka 2018 tasnia ya muziki wa dansi hapa nchini,  ilipata pigo la kuondokewa na wanamuziki wakubwa, Halila Tongolanga aliyefariki dunia Julai 04, 2017 na Shaaban Dede Julai 06, 2017.

Nguli hawa walipishana kwa siku mbili kuiaga dunia wakiwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili walikopelekwa kwa nyakati tofauti kwa ajili ya matibabu.

Shaaban Dede baada ya kifo chake, taratibu za maziko yalifanyika, hadi kupumzishwa kwenye nyumba yake ya milele katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.

Dede alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya Kisukari pamoja na Figo, wakati huohuo Tongolanga alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya Figo kwa wiki kadhaa. Halila Tongolanga atakumbukwa zaidi kwa wimbo wake wa “Kila Munu Ave na Kwao”

Katika makala hii imeandikwa historia ya mwanzo wa hadi mwisho wa maisha ya marehemu Shaaban Dede.

Wasifu wake unaeleza kuwa alizaliwa mwaka 1959, katika kijiji cha Kanyigo, mkoa wa Ziwa Magharibi wakati huo.

Yawezekana kabisa vijana wa kizazi hiki hawafahamu Mkoa wa Kagera ulipewa jina hilo baada ya vita vya Tanzania na Uganda.

Kabla ya hapo, mkoa huo ulikuwa na majina ya Ziwa Magharibi. Lakini hata kwa lugha ya Kimombo, ulifahamika kama West Lake Region.

Kazi aliyoifanya katika kipindi chote cha maisha yake ilikuwa ni muziki, bendi yake ya kwanza kuifanyia kazi ilikuwa TANU Jazz ya mjini Biharamulo mkoani humo.

Marehemu Shaaban Dede alikuwa na vipaji vingi vikiwemo vya utunzi na uimbaji pia alikuwa na uwezo mkubwa wa kuongoza wenzake.

Aliingia mjini Tabora mwaka 1977, akitokea Bujumbura nchini Burundi, ambako baba yake mzazi ndiko alikokuwa akiishi.

Dede akaenda kuomba kufanya kazi katika bendi ya Tabora Jazz, lakini hakufanikiwa baada ya kutengenezewa ‘zengwe’ dhidi yake.

Wakati huo ilikuwepo bendi ya Milambo Jazz “Wana Sona Sona’ iliyokuwa ikiongozwa na mwanamuziki Hassani Athumani.

Shaaban Dede alikwenda kuomba kujiunga katika bendi hiyo, akafanikiwa.

Alishirikiana na wanamuziki wengine aliowakuta katika bendi hiyo, akina Kawelee Mutimanwa, Pulukulu Wabandoki Motto, Roga, Kassim Rashid ‘Kizunga’, Hassan Kimbunga, aliyekuwa akicharaza gita la rhythm, Juma Ogan na wengine.

Baada ya kuonesha uwezo wake wa kutunga na kuimba katika bendi hiyo, uongozi wa bendi ya Tabora Jazz, uliombeza mwanzoni, ukamhitaji ajiunge nao.

Uongozi wa Milambo Jazz, ulikubali kwa sharti la kulipa deni la baiskeli aliyokuwa ameibiwa Shabani Dede ikiwa ni mali ya bendi.

Tabora Jazz walilipa deni hilo, Dede akajiunga na bendi hiyo. Hata hivyo  alipiga muziki kwa kipindi kifupi kabla ya kutimkia mjini Dodoma, akajiunga na bendi ya Dodoma International.

Akiwa na bendi hiyo aliweza kutunga nyimbo zikiwemo za ‘Fatuma’ na ‘Mtu ni tabia njema’

Baadae Shaaban Dede ‘alinyakuliwa’ na kiongozi na mpiga solo maarufu katika bendi ya JUWATA, Saidi Mabera, akampeleka katika bendi yake.

Madhumuni yalikuwa ni kuziba pengo lililoachwa wazi na Hassan Rehani Bichuka, aliyetimkia katika bendi ya DDC Mlimani Pack Orchestra mwaka 1990.

Uongozi wa JUWATA uliona sauti yake inashabihiana sana na ya Hassan Rehani Bichuka.

Dede akiwa katika bendi hiyo, alijipatia umaarufu mkubwa kupitia vibao vyake vya ‘Fatuma’, ‘Jenny’, ‘Sauda’,  ‘Mkono wa Birika’ na nyinginezo.

Aliimba nyimbo hizo akishirikiana na Joseph Lusungu, Juma Akida, TX Moshi William na Suleiman Mbwembwe (wote ni marehemu).


Licha ya kujipatia sifa na umaarufu kwa kipindi kifupi, Dede aliamua kuiacha bendi hiyo ya JUWATA akaenda kujiunga bendi ya DDC Mlimani Park Orchestra ‘Wana Sikinde’ ambako ilizidi kujimtambulisha zaidi kimuziki.


Akiwa katika bendi hiyo, alipewa nafasi ya kuwa mmoja wa viongozi  kwa vipindi vinne tofauti.

Dede alitunga nyimbo lukuki, ambazo ziliipatia umaarufu mkubwa bendi hiyo ya DDC Mlimani Park Orchestra.

Baadhi ya nyimbo hizo ni ‘Talaka rejea’, ‘Amua’, ‘Ndugu wagombanapo’, ‘Kumbuka fadhila’, ‘Binamu’, ‘Uchungu wa mwana’, ‘Chozi la huba’, ‘Fumanizi’, ‘Maneno maneno’ na nyinginezo.

Mashirika ya Umma hapa nchini yalianzisha vikundi vya burudani zikiwemo bendi za muziki.

Shirika la Bima Taifa lilikuwa na bendi ya Orchestra Bima Lee. Uongozi wa bendi hiyo uliamua kuongeza wanamuziki wengine mahiri toka bendi ya zingine kuimarisha nguvu.

Shabani Dede alikuwa miongoni mwa waliosombwa mwaka 1983, akiambatana na mpiga gitaa la solo Joseph Mulenga ‘King Spoiler’, Mafumu Bilali, Abdallah Gama na Jerry Nashoni ‘Dudumizi’.

Wanamuziki wengine walioijenga Bima Lee walikuwa akina Athumani Momba, Dancun Njilima na Suleiman Mwanyiro  ‘Compyuta’

Baadhi ya nyimbo alizotoka nazo ni za Aziza, Kununanuna, Dunia duara, Shangwe ya harusi, Bilionea wa mapenzi, Kipepeo na nyingine nyingine nyingi.

Mashabiki wa bendi hiyo walimpachika Shaaban Dede jina la ‘Mzee Tingisha’.

Mkataba ulipomalizika, Dede alirejea katika bendi ya DDC Mlimani Park.

Super Motisha Dede baada ya kuitumika bendi hiyo kwa kipindi kirefu kidogo, alirejea tena kwenye bendi yake Msondo iliyomkaribisha wakati alipokuwa akitokea Dodoma.


Shaaban Dede aliamua kurejea Msondo Ngoma baada ya kuikumbuka na kuwakosa mashabiki wake kwa muda mrefu.

Alikaririwa akisema hakuodoka katika bendi ya DDC Mlimani Park Orchestra ‘Wana Sikinde’ kwa sababu ya kushawishiwa kwa pesa, mtu ama kiongozi yeyote wa Msondo Ngoma, huo ulikuwa uamuzi wake binafsi.

Dede ambaye alipachikwa jina la ‘Kamchape’ na mashabiki wake, alikuwa hodari wa kutunga na kuimba nyimbo za maudhui na ujumbe mzuri katika jamii.

Katika historia yake katika muziki, bendi aliyodumu nayo kwa kipindi kirefu katika maisha yake ni Msondo Ngoma.

Dede alipokuwa katika bendi hiyo alishirikiana kuimba na waimbaji akina Juma Katundu, Twaha Mohamed, Hassan Moshi William ‘TX Junior’ na Hussein Kalembo.

Sauti zao zilikuwa zikienda sambamba na wakung’utaji magitaa ya solo na rhythm ambao ni Ridhiwani Pangamawe na Huruka Uvuruge, Ramadhani Zahoro Bangwe na Mustafa Hamis ‘Pishuu’.

Dede alipokuwa akiimba sauti yake ilipambwa na gitaa zito la besi la akina Ally Lindunga na Saad Ally ‘Sure Boy’.

Kwenye drums alikuwa zikichanganywa na Saad Ally ‘Mashine’ na Arnold Kang’ombe, tarumbeta alikuwa akipulizwa na Roman Mng’ande ‘Romarii’ na Hamis Mnyupe. Tumba zikipigwa na Amiri Said Dongo pamoja na Dorice George.

Dorice ni mwanamuziki mpya wa kike mwenye vipaji vingi, ambaye ni tunda la Chuo cha Sanaa Bagamoyo, bado yupo kwenye majaribio.

Dede aliwahi kufanya kazi na baadhi ya wanamuziki ambao wamekwisha tangulia mbele za haki akiwemo Mjomba Muhidin Maalim Gurumo.

Wengine ni TX Moshi William, Nicko Zengekala, Selemani Mbwembwe, Mnenge Ramadhan, Joseph Maina, Mustafa John Ngosha, Suleimani Mwanyiro, Tino Maselenge ‘Arawa’ na Athuman Momba.

Kwa upande wa upulizaji wa saxophoni alikuwepo Alli Rashidi, aliyefariki dunia siku ambayo bendi hiyo ikitimiza miaka 50, Oktoba 10, 2014.

Kamchape atakumbukwa kwa jinsi alivyokuwa akiipenda bendi hiyo ya Msondo, licha ya kuihama na kwenda kwa wahasimu wao Mlimani Park Ochestra ‘Sikinde’.

Aliporejea katika bendi hiyo ya Msondo Ngoma, alipewa nafasi ya uongozi, wala hakuhama tena hadi kifo kilipomchukua.

Bendi hizi za Mlimani Park na Msondo Ngoma, unaweza zinamashabiki kama ilivyo kwenye klabu za Simba na Yanga.

Marehemu Dede alikuwa na tabia ya kuwapiga madogo mahasimu wake wa Sikinde, ikipanda jukwani.

Bendi hizo zilikuwa na utaratibu wa kupiga muziki pamoja kwenye viwanja vya Sigara TTC Chang’ombe ama viwanja vya Leaders Club.

Katika onesho lao na Sikinde, katika viwanja vya Leaders Club, moja ya nyimbo za Msondo Ngoma, Shaaban Dede na Juma Katundu wakawa wanachomekea vionjo vikiwakejeli mahasimu wao Sikinde.

Alijulikana kwa uimbaji wenye kiwango cha juu kutokana na tungo zake murua, ambazo baadhi zilitokea kuwa gumzo ndani na nje ya nchi.

Miongoni mwa nyimbo za Dede, ambazo zinapendwa na wadau wa muziki wa dansi ni Fumanizi, Kelele za paka hazimzuii mwenye nyumba kulala, Mshenga, Baba mkwe, Amina, Talaka rejea na Kizabinazabina.

Nyimbo hizo na nyinginezo kadhaa, alizitunga wakati akiwa katika bendi ya DDC Mlimani Park kwa muda wa miaka 27, kabla hajarudi katika bendi yake ya zamani ya Msondo Ngoma, mwaka 2014.


‘Kamchape’ atakumbukwa kama mmoja wa wanamuziki nguli kwa sauti yake tamu kupitia nyimbo mbalimbali zilizoshika chati akiwa na bendi mbalimbali, zikiwemo za Bima Lee, Mlimani Park na Msondo Ngoma Music.

Shaaban Dede baada ya kifo chake, taratibu za maziko yalifanyika, hadi kupumzishwa kwenye nyumba yake ya milile kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.

Mazishi hayo yaliweka rekodi ya kuhudhuriwa na mamia ya watu, wakiwemo wanamuziki wakongwe, wa kizazi cha sasa na wadau wa tasnia ya muziki.


Baadhi ya watu waliofanyakazi naye, walimuelezea Dede kwa namna walivyokuwa wakimfahamu.


“Nilimfahamu Dede kwa kipindi kirefu kwani alikuwa mtunzi mzuri na mtu mwenye mchango mkubwa katika tasnia ya muziki. Nimesikitishwa sana na kifo chake na pengo lake halitazibika kwa urahisi” alisema Hassan Rehani Bichuka.


Kiongozi wa sasa wa Mlimani Park, Abdalah Hemba, alikiri kuwa Shaaban Dede ndiye aliyeibua kipaji chake, ambacho kwa sasa kimemfanya awe mwimbaji mahiri na kiongozi wa bendi hiyo kongwe nchini.

Hemba alisema “Dede ndiye alinisaidia kuingia katika bendi hii, hata nimejulikana kupitia sanaa ya muziki. Alikuwa mtambuzi mzuri wa vipaji vya wanamuziki baada ya kuwa nao kwa muda mfupi” alisema Hemba.

Shaaban Dede alikuwa mmoja wa watunzi mahiri wa nyimbo, hasa alipokuwa bendi ya Mlimani Park, ambapo inasemekana alitunga nyimbo zaidi ya 100, akiwa anashika nafasi ya pili nyuma ya Hassan Rehani Bitchuka.

Pia, alikuwa chachu ya ushindani wa kimuziki uliokuwepo kati ya Msondo Ngoma na Mlimani Park, ambapo alikuwa ‘Karata’ muhimu ya ushindi katika kila bendi.

Dede alikuwa anajua nini cha kufanya ili kuwafurahisha mashabiki na kuwapa ile burudani wanayoihitaji.

Nguli huyu ametunga na kuimba ni nyingi zikiwemo za Kilio Cha Mtu Mzima, Kaza Moyo (Msondo), Diana, Tui la Nazi  na Amina (Sikinde) ambazo zinaonesha uhalisia wa maisha ya watu.

Nyimbo hizo na zingine zilijizolea umaarufu katika kumbi mbali mbali za muziki na kuvuta mashabiki wa rika zote.

Ni wazi kuwa Dede ameacha mengi ya kujifunza kwa wanamuziki wa sasa. Nayo ni uvumilivu wa kudumu kwenye bendi kwa miaka mingi, kutunga nyimbo zinazogusa hisia na kuimba kwa sauti yenye mvuto.

Mashabiki wa muziki walikupenda, lakini Mungu amekupenda zaidi.

Kazi uliyoifanya hapa duniani imetosha, itabaki kuwa kumbukumbu kwa vizazi vilivyopo na vijavyo kwa miaka mingi.


Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, Amina.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...